Wafahamu wazaliwa wa kizazi cha watumwa Nigeria wasioweza kuwaoa wanaowapenda

Mwanamke anayetoa pete yake na mwanamume nyuma yake amehsikilia kichwa chake

Chanzo cha picha, Getty Images

Wachumba wawili wa Nigeria walijito uhai mwezi huu baada ya wazazi wao kuwazuia wasioane kwasababu mmoja wao anatokana na kizazi cha watumwa.

"Wanasema hatuwezi kuoana… yote ni kwasababu ya imani za kale,"ulisema ujumbe kwenye kijikaratasi walichokiacha nyuma.

Wachumba hao waliokuwa ndio mwanzo wameingia miaka thalathini, kutoka Okija kusini- mashariki mwa jimbo la Anambra, ambako utumwa ulifutwa rasmi mwaka 1900, sawa na ilivyokuwa sehemu zingine zote za Nigeria zilizokuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Uingereza wakati huo.

Lakini kizazi kilichotokana na watumwa walioachiliwa huru miongoni mwa jamii ya Igbo bado kilisalia na utambulisho wa mababu zao na wanazuiliwa kitamaduni kuoa ama kuolewa na Waigbo wanaowachukulia kama ''kizazi cha watumwa''.

"Mungu alimuumba kila mtu bila ubaguzi, kwanini binadamu wanabaguana kutokana na makosa yaliofanywa na mababu zao," walisema wachumba hao.

Wachumba wengi wa jamii ya Igbo hukumbwa na ubaguzi kama huo ambao hawakutarajia.

Miaka mitatu iliyopita Favour, 35, ambaye anapendelea kutotumia jana lake, alikuwa anajiandaa kuolewa na mwanamume aliyechumbiana naye kwa miaka mitano, kabla ya jamaa zake Waigbo kubaini kuwa anatokana na kizazi cha watumwa.

"Walimwambia kijana wao kwamba hawataki kuniona," alisema Favour, ambaye pia ni wa jamii ya Igbo.

Mwanzoni mchumba wake alipuuza suala hilo lakini baadae shinikizo kutoka kwa wazazi na ndugu zake zilimshinda hadi akaamua kukatiza uhusiano wao.

"Nilihisi vibaya. Nilisikitika sana. Moyo wangu uliniuma sana," alisema.

Wamefanikiwa maishani lakini hawana 'hadhi'

Ndoa sio kizingiti pekee kinachokabili kizazi cha watumwa.

Pia wamepigwa marufuku kuchukua nafasi ya uongozi katika jamii au hata kuongoza kundi la wasomi, na mara nyingi wanazuiliwa kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa ama hata kuwakilisha jamii katika bunge.

Oge Maduagwu anasafiri kusini mashariki kuwashinikiza viongozi wa kitamaduni kubadili fikra

Chanzo cha picha, Adaobi Tricia Nwaubani

Maelezo ya picha, Oge Maduagwu anasafiri kusini mashariki kuwashinikiza viongozi wa kitamaduni kubadili fikra

Hata hivyo hali hiyo haiwazuii kupata elimu wala kufikia malengo yao ya kiuchumi.

Ubaguzi huo uliwasukuma wengi wao kukubali Ukristo na elimu rasmi iliyoletwa na Wamishonari, wakati ambapo wenyeji wengine walikuwa bado wana mashaka na wageni.

Baadhi ya watu waliotokana na kizazi cha watumwa ni miongoni mwa watu walio na ufanisi mkubwa katika jamii lakini licha ya ufanisi wao bado wanachukuliwa kuwa watu walio na hadhi ya chini

Mwaka 2017, Oge Maduagwu mwenye umri wa miaka 44 alianzisha mkakati wa kukabiliana na ubaguzi wa kitamaduni katika jamii yake (Ifetacsios).

Katika kipindi cha miaka mitatu amekuwa akisafiri katika majimbo matano ya kusini mashariki mwa Nigeria, kutetea haki sawa kwa kizazi cha watumwa.

"Ubaguzi unaowakabili Wamarekani weusi ni sawa na ubaguzi unaokabili kizazi cha watumwa hapa," alisema.

Bi Maduagwu sio kizazi cha watumwa, lakini alishuhudia ukosefu wa usawa utotoni mwake alipokuwa anakua katika jimbo la Imo na alipata msukumo wa kukabiliana nao alipoona madhila aliyopitia rafiki wake wa karibu aliyezuiliwa kumuoa mchumba wake kwasababu anatokana na kizazi cha watumwa.

Wakati wa ziara zake, Bi Maduagwu alikuwa anakutana kando na watu walio na ushawishi katika jamii na baadae kuwakutanisha na kundi la watu wanotokana na kizazi cha watumwa ambapo anakuwa mpatanishi katika mazungumzo hayo.

"Wanaume walikaa chini na kutunga sheria hizi," alisema. " Sisi pia tunaweza kukaa chini na kuzifanyia marekebisho."

Kizazi cha watumwa miongoni mwa jamii ya Igbo kimeorodheshwa katika makundi mawili makubwa - Waohu na Waosu.

Mababu wa ohu, walimilikiwa na binadamu huku wale wa osu wakimilikiwa na miungu- watu waliojitolea kulinda makaburi ya kijamii

"Osu ni hatari kuliko utumwa," alisema Ugo Nwokeji, profesa wa elimu ya Kiafrika katika chuo kikuu cha California, Berkeley, ambaye anafikiria Waosu waliorodheshwa kama watumwa na wamishonari.

"Watumwa wanaweza kujikomboa dhidi ya utumwa na kuwa huru lakini kizazi cha Waosu kwa miaka na mikaka hakijajinasua kutokana na utumwa wa mababu zao."

2px presentational grey line

Makaazi ya kabila la Igbo nchini Nigeria

Ramani inayoonesha jimbo la Igbo nchini Nigeria
2px presentational grey line

Ubaguzi dhidi ya Waosu umetajwa kuwa mbaya zaidi.

Japo Waohu wametengwa kama watu wa nje - ambao hawajulikani walikotokea wala kufahamika mahali mababu zao walikoishi ama kushikiliwa kama watumwa - kuvunja uhusiano wao na Waosu kunaogopewa kutokana na ubaguzi wa kijamii na pia adhabu kutoka kwa miungu wanaodaiwa kuwamiliki.

Mchumba wa Favour aliambiwa na baba yake kwamba Maisha yake yatakatizwa endapo atamuoa Muosu

"Walimuingiza uwoga," anasema. "Aliniuliza kama nataka afariki."

'Uhamasishaji zaidi vijijini'

Hofu kama hizo zimefanya kuwa vigumu kutekeleza sheria dhidi ya ubaguzi ambazo zipo katika katiba ya Nigeria, ikiwa ni pamoja na Sheria ya mwaka 1956 iliyowekwa na wabunge wa Igbo kwa lengo maalum la kufutilia mbali ubaguzi dhidi ya Waohu ama Waosu.

"Hatua za Kisheria pekee hazitoshi kukabiliana na utamaduni wa kijamii," alisema Anthony Obinna, Askofu mkuu wa kanisa Katoliki katika Jimbo la Imo, na ambaye pia amekuwa akipigania kukomeshwa kwa ubaguzi. "Unahitaji uhamasishaji vijijini."

Katika wakati wake mwingi , Bi Maduagwu anawahamasisha watu njia tofauti ambazo wameshirikiana na Waosu bila kuzingatia kanuni za kitamaduni bila "miungu kuwachukulia hatua".

"Leo hii sisi ni wapangaji katika nyumba zao, tuko kwenye orodha ya waajiriwa wao, tunakopa pesa kutoka kwao," anasema.

Ushirikiano kama huo na Waosu haukuwepo siku za nyuma.

Hakuna data rasmi inayoonesha idadi kamili ya kizazi cha watumwa katika eneo la kusini-mashariki mwa Nigeria.

Watu mara nyingi wanaficha utambulisho wao, lakini ni vigumu kufanya hivyo katika jamii ndogo ambako kizazi cha kila mmoja kinajulikana. Baadhi ya jamii zina ohu ama osu, lakini zingine hazina.

Katika miaka ya hivi karibuni, kuongezeka kwa shinikizo la kutaka kutambuliwa kutoka kwa waohu na Waosu kumesababisha mzozo na machafuko katika jamii nyingi.

Wazawa wengine wa kizazi cha watumwa wameanzisha uongozi wao na makundi ya wasomi.

2px presentational grey line

Karibu miaka 13 iliyopita, Waosu katika jimbo la Imo waliunda kikundi kilichofahamika kama Nneji, kumaanisha "kutoka kwa tumbo moja".

Kundi la Nneji liliwapa maelfu ya wanachama wake miongoni mwa mafao mengi kama vile fursa ya watu wao kuoa au kuolewa kutoka kila pembe ya dunia ili kuwaepushia madhila ya kukataliwa nyumbani kwa kuwa wametokana na "kizazi cha watumwa".

"Watu wanakuja kwako ikiwa wanataka usaidizi kutoka kwako," anasema mfanyakazi Ogadinma, katika familia tajiri ya osu, ambaye mamake ni mfawidhi wa kundi la Nneji.

"Lakini watu hao hao, wakati watoto wenu wanataka kuoa watoto wao, wanalalamika kuwa mtu huyo ni Muosu."

Oge Maduagwu

Chanzo cha picha, Oge Maduagwu

Maelezo ya picha, Oge Maduagwu anatumai kwamba maandamano ya Black Lives yatasaidia kubadili mienendo ya kabila la Igbo

Askofu mkuu Obinna, ambaye amekosolewa kwa kufungisha ndoa ya watu wanaodhaniwa kuwa "mchanganyiko", anasema: "Nimelazimika kulinda wanandoa wengine kushambuliwa na wazazi na jamaa zao."

Ogadinma, ambaye pia hakutaka BBC kutambulisha jina lake ili kulinda usalama wa familia yake, alikabiliwa na ubaguzi alipoamua kuwania wadhifa wa kisiasa karibu miaka 10 iliyopita.

Pingamizi zilimiminika kutoka kwa watu waliosema "hafai" kuwania - na kiongozi wa kitaifa wa chama chake ambaye alikuwa Myoruba, alishindwa kumuunga mkono na kuamini hakuwa na nafasi ya kupata ushindi.

"Aliniambia bayana: 'Kuna kitu nimeambiwa na WaIgbo kukuhusu, na ambacho hakitaruhusu watu wako kukupigia kura."

Ubaguzi kwa misingi ya ukoo sio jambo la kawaida katika jamii za Yoruba ama Hausa, makabila mawilii makubwa nchini Nigeria. Lakini umeripotiwa miongoni mwa makabila mengine madogo katika nchi za Afrika Magharibi, kama vile Mali na Senegal.

Kundi la Bi Maduagwu sasa lina wafanyakazi wanna na makumi ya watu wanaofanya kazi ya kujitolea.

Haijakuwa rahis kwao kuwashawishi viongozi wa kijamii lakini baadhi yao wameanzisha mchakato wa kufutilia mbali utamaduni wa kutokuwa na usawa katika jamii zao.

Anasema awali aligutushwa sana na mashambulio katika mitandao ya kijamii kutoka kwa watu amabo walipinga harakati zake.

"Nililazimika kujiunga na makundi kadhaa ya Waigbo ili kusambaza ujumbe wangu na Wengi wao walinitukana na kuniambia huo ni utamaduni ambao hautawahi kubadilika."

Sababu ya Nollywood

Ogadinma anahofia wanafunzi wa Nigeria kutoka maeneo tofauti duniani na ambao wamesoma kitabu hicho shuleni huenda wakaamini imani ya kitamaduni waliyosoma kuhusu Waosu

"Ikiwa kila kizazi cha watoto wa Nigeria wanasoma kuhusu Waosu, huoni itaathiri mawazo yao?" alisema .

Filamu za Nigeria maarufu Nollywood pia zimechangia ubaguzi kwa kiwango fulani, kwa mujibu wa Aloysius Agbo, Askofu wa Kianglikana katika jimbo la Enugu, ambaye Pia anapigania kukomeshwa kwa ubaguzi wa kitamaduni

Film za Nigeria zina kitu maalum kinachoonesha tamaduni hizo ikiwa ni pamoja na kituo maalum cha Africa Magic.

"Wanatumia vita hivyo kuangazia masuala ya kitamaduni lakini nadhani hawajui athari zake kijamii." Askofu Agbo anasema

Lakini katokana na maandamano ya hivi karibuni ya Black Lives Matter (BLM) sehemu tofauti duniani, Bi Maduagwu ana matumaini kwamba watu wengi kutoka jamii ya Igbo watabadili mtazamo wao kuhusu mila za zamani zilizopitwa na wakati.

"Iikiwa watu watatafakari ilipoanzia safari ya Wamarekani weusi basi maandamano ya BLM yatakuwa na tija katika kazi yetu," Bi Maduagwu alisema.

"Waafrika wanastahili kujitathmini kwa undani kuona kinachofanyika nyumbani kwetu."

Adaobi Tricia Nwaubani ni mwanahabari na muandishi wa vitabu kutoka Abuja