Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Tanzania 2020: Hussein Mwinyi na mtihani wa kulinda ushindi wa CCM Zanzibar
Filimbi ya uchaguzi wa vyama vingi ilipopulizwa mwaka 1995, Zanzibar iliingia ulingoni kwa upinzani mkali, na mpaka sasa upinzani huo bado ungalipo.
Katika kinyang'anyiro cha urais wa Zanzibar kwa mwaka huu, chama tawala CCM kimemsimamisha Hussein Mwinyi, kupeperusha bendera yake katika kinyang'anyiro hicho.
Mwinyi ambaye ndiyo mara yake ya kwanza kuwania urais wa 'visiwa vya karafuu' atakumbana na upinzania mkali kutoka kwa Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye anagombea kwa mara ya sita mfululizo.
Suala la mazingira ya ushindani mkali ni la wazi, hata katika mahojiano alofanya na vyombo vya habari vya ndani vya Mwananchi na Azam TV, Mwinyi amekiri kuwa ushindani mbele yake ni mkali huku akijinadi kuwa mwishowe atashinda kama wagombea wengine wa CCM kabla yake.
Je Mwinyi ni nani?
Japo ni mpya katika mbio za urais, Mwinyi ni kiongozi mwandamizi katika siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Safari yake kisiasa ilianzia mwaka 2000, alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mkuranga kwa upande wa Tanzania bara, na kisha mwaka 2005 kuhamia upande wa Zanzibar katika jimbo la Kwahani ambalo ameliongoza kwa miaka 15.
Katika kipindi chake cha miaka 20 ya ubunge amefanya kazi na marais watatu wa Tanzania, hayati Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na rais wa sasa John Magufuli.
Mwaka 2000 alichaguliwa kuwa naibu waziri wa afya na hayati Mkapa, katika miaka 10 ya Kikwete alipanda na kuwa waziri kamili na kuhudumu katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Afya na Ulinzi.
Miaka mitano iliyopita amehudumu kama Waziri wa Ulinzi kwenye serikali ya Magufuli.
Ushawishi wa Mwinyi uliojengeka katika utumishi wake katika miongo miwili iloyopita ulijidhihirisha katika namna ambavyo alinyakua tiketi ya kuwania urais ya CCM.
Safari hiyo ilianza kwa zaidi ya wananchama 30 kuchukua fomu za kuwania, kisha majina matano yakapelekwa mbele ya vikao vya juu vya chama hicho kwa maamuzi. Katika kura za mwisho za uteuzi ndani ya chama, Mwinyi alipata kura 129 sawa na asilimia 78 ya kura zote, mshindani aliyemkaribia zaidi alikuwa na kura 19.
Pamoja na uzoefu wake na ushawishi wake binafsi wa kisiasa, Mwinyi anatokea katika moja ya familia maarufu na kubwa kisisasa nchini Tanzania. Baba yake Mzee Ali Hassan Mwinyi ni rais mstaafu wa serikali za Tanzania na Zanzibar.
Kitaaluma, Mwinyi ni tabibu na amepata elimu yake nchini Tanzania, Misri, Uturuki na Uingereza.
'Msinichagulie shikamoo'
Ushindi wake ndani ya chama ulikuwa wa kishindo, lakini hata wakati wakipongezana kwa kumpata mgombea ambaye chama kinamnadi kuwa ni sahihi, fikra za viongozi wa juu na wanachama wa kawaida zilishahamia katika ushindani dhidi yake.
Rais Magufuli akimnadi Mwinyi baada ya kupitishwa na CCM kuwa mgombea wao wa urais, alituma salamu ama dongo la kisiasa kwa mshindani wao mkuu Zanzibar, Maalim Seif, kwa kuwataka Wazanzibari "...msinichagulie shikamoo."
Suala la umri, limekuwa moja ya hoja za kampen kwa upande wa CCM, kuwa Mwinyi mwenye miaka 53 ni 'kijana' mwenye nguvu bado ya kuifanya kazi ya urais, huku Maalim Seif mwenye miaka 76 wakidai amechoka na anastahili kupumzika.
Hata hivyo kwa Maalim Seif na wafuasi wake wa chama cha ACT-Wazalendo, umri si kigezo. Maalim amemjibu Magufuli kuwa "...shikamoo utaitoa utake usitake" huku wafuasi wake wakitumia salamu hiyo kama kionjo chao: "Shikamoo Maalim."
'Yajayo ni neema tupu'
Katika kujinadi kwa sera na azma ya kuleta mabadiliko visiwani Zanzibar, Mwinyi anatumia kauli mbiu: "Yajayo ni neema tupu."
Baadhi ya vipaumbele vyake ni kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma ambapo ameahidi kushughulikia tatizo hilo kwa staili yarais Magufuli. Kuboresha mazingira ya sekta ya utalii ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar pamoja na kuwanyanyua wajasiriamali na wanawake visiwani humo.
Hata hivyo, kabla ya kufika huko bado ana mtihani mzito wa kuushinda ambao ni uchaguzi wa Oktoba 28. Toka uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995 uchaguzi wa urais Zanzibar umekuwa na kishindo kikubwa.
Chaguzi zote za Zanzibar kasoro mwaka 2010, zimeshuhudia malalamiko ya wizi wa kura na udanganyifu, uvunjifu wa haki za binaadamu na ghasia.
Unaweza pia kusoma:
Mwaka 2010 hali ilikuwa tulivu kutokana na kura ya mabadiliko ya katiba ya kuwezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Baada ya uchaguzi wa 2010, Maalim Seif alichukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na chama chake enzi hizo cha CUF kuunda sehemu ya mawaziri wa baraza la mapinduzi.
Mwaka 2015 matokeo ya uchaguzi yalifutwa, na uchaguzi kurudiwa 2016 japo chama kikuu cha upinzani CUF kilisusia kushiriki.
Kutokana na historia ya uchaguzi Zanzibar, ni wazi kuwa Mwinyi ana upinzania mkali wa kupambana nao kutoka kwa Maalim Seif katika uchaguzi wa sita toka mfumo wa vyama vingi kurejea Tanzania.