Qatar inawanyanyasa wafanyakazi wahamiaji katika matayarisho ya Kombe la Dunia mwaka 2022

Wahamiaji wengi ndio wanaotumika kujenga viwanja vitakavyoandaa kombe la dunia mwaka wa 2022.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wahamiaji wengi ndio wanaotumika kujenga viwanja vitakavyoandaa kombe la dunia mwaka wa 2022.

Qatar kwa mara nyingine tena inaangaziwa kwa namna vile inavyolipa mishahara wafanyakazi wahamiaji walio nchini humo kwa ajili ya matayarisho ya Kombe la Dunia mwaka 2022.

Ripoti mpya kutoka Shirika la Human Rights Watch limesema kwamba Qatar imeshindwa kutimiza ahadi yake ya kuimarisha mazingira ya kazi na kumaliza unyanyasaji wa mishahara kote nchini humo.

Wafanyakazi wahamiaji ni karibu asilimia 95 ya nguvu kazi huko Qatar. Kuna karibu wahamiaji milioni 2 wanaofanya kazi nchini humo.

Lakini wengi wao wanafanyakazi chini ya mfumo unaofahamika kama kafala, au mfumo wa ufadhili, ambapo viza za wafanyakazi wahamiaji huwa na waajiri wao, na kuwafanya kuwa katika hatari ya kunyanyaswa.

Katika ripoti yake, Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch, lina nyaraka zinazoonesha kesi moja baada ya nyingine ya unyanyasaji wa malipo katika ajira mbalimbali ikiwemo walinzi, wahudumu wa mahoteli, mabawabu, wanaofanya usafi, wasimamizi wa makampuni na wafanyakazi wa ujenzi.

Wengi ni wajenzi au wanafanyakazi katika viwanja vya michezo, kwenye sekta ya usafiri, mahoteli na miundombinu kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2022.

Mwaka 2017, Qatar iliahidi kwa Shirika la wafanyakazi la Kimataifa kumaliza mfumo wa Kafala. Lakini wafanyakazi waliohojiwa na Shirika la Human Rights Watch wameelezea unyanyasaji ambao bado unaendelea kutekelezwa.

Qatar inawadhulumu wahamiaji

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Qatar inawadhulumu wahamiaji

Hali ikoje nchini Qatar?

Shirika la Human Rights Watch lilizungumza na wafanyakazi wahamiaji 93 wanaofanya kazi kwa waajiri 60 na makampuni tofauti kati ya Januari 2019 na Mei 2020, ambao wote walililalamikia aina fulani ya unyanyasaji kutoka kwa waajiri wao.

Ripoti ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch, imeonesha dhuluma bado zinaendelezwa za malipo kwa wafanyakazi raia wa kigeni walio nchini humo kwa ajili ya kufanikisha Kombe la Dunia 2022.

"Miaka kumi tangu Qatar ijishindie nafasi ya kuwa mwenyeji wa Michuano ya Kombe la Dunia la Soka, FIFA 2022, wafanyakazi raia wa kigeni wangali wanaathirika kwa kucheleweshwa kwa malipo, mishahara kutolipwa kabisa, au hata mishahara kukatwa," asema Michel Page, naibu mkurugenzi wa Human Rights Watch eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

"Tumepata habari za wafanyakazi kukosa chakula kwa sababu ya malipo yao kucheleweshwa, wafanyakazi kukumbwa na madeni, kulipwa mishahara midogo na vilevile kuna wale ambao wamejipata katika mazingira magumu ya kazi lakini wanaogopa kulalamika wasije wakadhulumiwa zaidi." Michel Page ameongeza katika ripoti iliyotolewa.

Kulingana na taarifa hiyo, wafanyakazi 59 walisema kwamba malipo yao yamecheleweshwa, yameshikwa au kutolipwa; Wafanyakazi 9 walisema hawajalipwa kwasababu waajiri waliwaambia kwamba hawana wateja wa kutosha; 55 wakasema hawajalipwa kwa kazi ya ziada licha ya kuwa walifanya kazi zaidi ya saa nane, wengi walifanya zaidi ya saa 10 kwa siku; na wafanyakazi 13 walisema waajiri walibadilisha mikataba yao ya kuajiriwa wakaandaa mikataba tofauti ambayo inawapendelea wao wenyewe.

Wafanyakazi 20 walisema hawakupokea mafao ya kumaliza vipindi vyao vya kuhudumu; huku 12 wakisema waajiri walikata malipo yao bila kuwafahamisha.

Aidha, inasemekana kwamba dhuluma za malipo zimeongezeka tangu kuanza kwa maradhi ya virusi vya Corona.

Baadhi ya waajiri walitumia janga la corona kuwa sababu ya kukatalia ujira au kukataa kuwalipa wafanyakazi wanaokamatwa na kurejeshwa kwao kwa nguvu.

Baadhi ya wafanyakazi walisema hata hawawezi kununua chakula. Wengine wakasema walilazimika kukopa pesa ili waweze angalau kuishi, ripoti hiyo imeongeza.

Uwanja wa Kombe la dunia nchini Qatar

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Uwanja wa Kombe la dunia nchini Qatar wakati unaanza kujengwa

Samuel, ambaye sio jina lake kamili, ni mmoja kati ya Wakenya wanaokadiriwa kuwa 30,000 wanaofanyakazi kama wahamiaji nchini Qatar.

''Waliniahidi Riyali 1200 za Qatar kama mshahara wangu lakini sasa hivi wananilipa Riyali 830 za Qatar. Sikuelewa kwanini lakini sikuwa peke yangu. Wenzangu nilioanza nao kazi siku moja - 18 walikuwa na maswali kama yangu.''

Kulingana na Shirika la Human Rights Watch, Mkenya mwengine ni "Henry," alipopata hakikisho kwamba ametimiza vigezo vyote vilivyohitajika kumruhusu kufanyakazi ya kurekebisha mabomba ya kupitisha maji chini ya ardhi huko Qatar alikuwa na furaha ajabu.

Lakini ili kupata kazi hiyo alichukua mkopo uliokuwa na riba ya asilimia 30 kuweza kumlipa ajenti aliyemuunganisha kupata kazi hiyo. Na pia Henri alifanya kazi hiyo kwa saa 14 kwa siku.

Aidha, kulingana na ripoti iliyotolewa, Henry, 26, alijionea maajabu baada ya kuwasili Doha Juni 2019.

Mwezi wa kwanza tayari hakufanya kazi kwasababu hakukuwa na kazi kwa ajili yake hilo likimaanisha kwamba hana mshahara.

Mwezi wa pili, mwajiri wake alishikilia mshahara wake kama amana ya usalama na hilo likamaanisha kwamba ili aendelee kulisha familia yake ni lazima achukue mkopo zaidi.

Na hatimae mwezi wa tatu akalipwa lakini kilichomshangaza ni kwamba mshahara ulipunguzwa mno.

"Mshahara wangu kamili ulienda wapi? Pesa ya kufanya kazi muda wa ziada ilienda wapi pamoja posho ya chakula? Nilishtuka lakini sikuwa peke yangu - kampuni hiyo ilikuwa imedanganya karibu Wakenya 13 waliokuwa pamoja na mimi," Henry alisema.

Uwanja wakombe la dunia Qatar

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Uwanja wakombe la dunia Qatar wakati unaanza kujengwa

Shirika la Human Rights Watch liliitumia wizara ya wafanyakazi nchini Qatar maswali kadhaa na mambo mengine ambayo lilikuwa limeyapata.

Vilevile shirika hilo liliitumia wizara ya maswala ya ndani, na shirika la soka la Kimataifa FIFA, na kamati kuu ya utekelezaji wa Michuano hiyo nchini Qatar.

''Tulipata majibu kutoka kwa kamati kuu, afisi ya mawasiliano ya Qatar (GCO) na shirika la FIFA, limesema Shirika la Human Rights Watch.

Katika majibu yake, shirika la FIFA kwenye waraka wake liliandika kwamba 'FIFA ina sera thabiti zinazokataza ubaguzi wa namna yoyote na dhuluma za malipo.

''Kupitia juhudi zetu za kulinda haki za wafanyakazi kwenye miradi mingi ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar, FIFA inafahamu umuhimu wa kuwepo njia za kulinda ujira wa wafanyakazi nchini Qatar. Hii ndio maana FIFA na wahusika wengine kwenye maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia imeweka mifumo ya kukomesha dhuluma za malipo kwenye miradi hiyo.''

Vilevile FIFA imeandaa njia za kuwaruhusu wafanyakazi kutoa malalamiko yao ili kampuni zikishindwa kudumisha viwango vyetu basi suala hilo litashughulikiwa na kutatuliwa.

Tangu Qatar ilipoahidi kufanyia marekebisho mfumo wa ''Kafala'' ambao huwazuia wafanyikazi wahamiaji kubadilisha kazi ama hata kuacha kazi bila idhini ya mwajiri wao.

Bado idadi kubwa ya waliohojiwa kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch, wanatafuta haki huku ikiwa imesalia miaka miwili kwa michuano ya Kombe la Dunia la FIFA kuanza nchini humo.