Mgogoro kati ya Uturuki na Ugiriki: Ufaransa yatuma jeshi lake bahari ya Mediterrean

Chanzo cha picha, Reuters
Ufaransa imepeleka ndege mbili za kivita aina ya Rafale na meli ya kivita ya mashariki mwa Mediterranean kwasababu ya wasiwasi uliopo kati ya Ugiriki na Uturuki.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameitaka Uturuki kusitisha shughuli ya utafutaji wa mafuta na gesi katika eneo la maji linalozozaniwa.
Meli ya utafiti ya Uturuki ilianza shughuli ya utafutaji mafuta Jumatatu, hatua iliyokasirisha Ugiriki.
Bwana Macron amemuarifu Waziri Mkuu wa Ufaransa Kyriakos Mitsotakis kwamba jeshi la Ufaransa linafuatilia hali hiyo.
Eneo hilo ni tajiri kwa nishati ambayo bado haijavumbuliwa.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema suluhu pekee kwa mzozo wa Mediterranean ni mazungumzo na kwamba nchi yake haikimbilii kwenye ubahatishaji wa kile ambacho hakijawahi kupatikana.
"Ikiwa tutachukua hatua za busara na hekima, tunaweza kufikia muafaka utakaofaidi pande zote mbili, unaotimiza maslahi ya kila mmoja," amesema.
Pia kuna wasiwasi kuhusu Cyprus juu ya haki za utafutaji mafuta za mahasimu wao. Jamhuri ya Cyprus na Ugiriki hazikubali haki zozote kama hizo kwa eneo la Cyprus kaskazini linalodhibitiwa na Uturuki.

Chanzo cha picha, Getty Images
Aidha Ufaransa pia ina uhasama na Uturuki juu ya mzozo wa Libya.
Uturuki imetuma jeshi kusaidia serikali inayotambuliwa na Umoja wa Ulaya huko Tripoli, huku Ufaransa, Urusi, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu, zikiunga mkono vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar.
Urusi na Umoja wa Falme za Kiarabu ndio wauzaji wakubwa wa silaha kwa Jenerali Gen Haftar.
Ufaransa tayari helikopta yake, Tonnerre, inaelekea Beirut ambayo imebeba msaada kwa ajili ya mji huo wa Lebanon baada ya nchi hiyo kukumbwa na janga la mlipuko katika eneo la bandari Agosti 4.
Meli ya kivita ya Ufaransa ya La Fayette imekuwa ikifanya mazoezi na Ugiriki na ipo eneo hilo.
Ndege za kivita za Rafale zilikuwa Cyprus kwa mazoezi na sasa zinaelekea Souda, katika kisiwa cha Ugiriki cha Crete.
Bwana Macron ametuma ujumbe kwa Twitter: "Nimeamua kuimarisha uwepo wa jeshi la Ufaransa kwa muda katika bahari ya Mediterranean, kwa ushirikiano na Ugiriki na washirika wengine wa Ulaya.
"Hali ilivyo Mashariki mwa Mediterranean inatia wasiwasi. Uamuzi wa upande mmoja wa Uturuki kuhusu utafutaji wa mafuta unachochea wasiwasi. Wasiwasi huo lazima ufikie kikomo ili kuwezesha mazungumzo kuwa shwari kati ya nchi ambazo ni majirani na washirika wa Nato."














