Waridi wa BBC: 'Huzuni ilinifanya kuwa mraibu wa ngono'

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Maisha ya utotoni kwa Mary Wanjiku, ni sehemu ya maisha yake ambayo angelikuwa na uwezo angeifuta kabisa, asiikumbuke kamwe.

Ni maisha yaliyojaa masikitiko na vilio. Nusura maisha yake yachukue mwelekeo wa maangamizi lakini kwa bahati alijinusuru kabla ya kuangamia.

Utotoni mwake Wanjiku, ambaye sasa ana miaka 26, alijihisi kuchukiwa na kutodhaminiwa na waliokuwa walezi wake. Alipitia mateso na dhihaka kila siku.

Ilikuwaje maisha yake yakawa ya kero hivyo? Alijinusuru vipi?

Simu ya dharura

Yote haya yalianza baada ya kifo cha mamake, ingawa wakati huo alikuwa bado ni mtoto mdogo.

"Siku mama yangu alipozikwa, babangu mzazi alimpigia nyanyangu simu ya dharura na kumueleza kuwa aje achukue mzigo - kwa mzigo alikuwa na maana ya mimi na dadangu - kabla hajatukatakata vipande," anakumbuka Mary.

Bibi alisafiri kwa dharura hadi mtaa wa Kibera, Nairobi walimokuwa wanaishi Mary na dadake kabla ya mamake kuaga dunia.

Aliwachukua na kusafiri nao hadi kijijini Kandara, Murang'a katika uliokuwa mkoa wa Kati nchini Kenya.

Mary alidhani wamepata kimbilio salama na kwamba bibi angechukua nafasi ya mama mzazi.

Kumbe ilikuwa ndio mwanzo mkoko unaalika maua. Nyumbani kwake, bibi hakuwa na usemi.

"Wajomba na binamu zetu walitutesa sana mimi na dada yangu. Tulivuilia matusi ya kila aina kila siku", Mary anakumbuka.

Anaeleza kuwa akijaribu kusema siku ambazo walilala njaa na si kwamba hakukuwa na chakula nyumbani, si mara moja wala mbili. Ilikuwa kama ada kunyimwa chakula.

Kwa kuwa bibi alikuwa mzee hakuwa na usemi katika mambo mengi yaliokuwa yanafanyika katika boma hilo.

Mary anasema kilichokuwa kimakirihisha zaidi ni mmoja wa wajomba aliyekuwa na tabia ya kuwaelekeza kwenye kaburi la mama yao, eti waufukue mwili wake waule.

Safari ya kaburini

Baada ya muda, alianza kuzuru kaburi la mamake, lakini si kwa kuufuata ushauri wa yule mjomba.

Sababu yake ni kwamba alikuwa akipata faraja na amani kwa kujihisi karibu na mamake mzazi. Alipata wakati wa kupumua, kuyasahau ya dunia na pia kutamani mamake angefufuka wawe pamoja tena.

"Nilikuwa natamani sana mamangu angefufuka. Nilijua tu ni mama ambaye angekuwa na uwezo wa kunilinda na kunipenda bila mipaka," Mary anakumbuka.

Kwa mara kama tatu hivi anasema alizuru kaburi la marehemu mamake akiwa na lengo la kuufukua mwili wake, ila hakufanikiwa kutekeleza lengo hilo.

Shida zilipozidi, Mary alishindwa kuendelea na masomo.

Anasema njaa ilikuwa sababu kubwa. Alionelea ni kheri aajiriwe kama kijakazi, wakati huo akiwa na miaka 16.

Lakini kazi ile ya nyumbani haikudumu.

"Ni kana kwamba nilikuwa na bahati mbaya. Mwajiri wangu alikuwa ni afisa wa polisi. Pale kwake alikuwa ananinyima chakula na kila wakati kuzabwa makofi kwa makosa madogo madogo, niliamua kuiacha kazi ile," anasema.

Hakuwa na kwenda.

Alipoiacha kazi ile, Mary alikutana na swahibu wake kule kule kijijini aliyempa mawaidha ya kuanza kazi kama mhudumu kwenye kilabu.

Pale alikuwa muuzaji wa kahawa ila wakati mwengine angeuza vileo pia. Katika pilikapilika hizo, Mary alikutana na mwanamume mmoja aliyeonyesha nia ya kumpenda na kumjali.

Katika kipindi cha wiki mmoja tu ya kufahamiana, walianza maisha ya mume na mke wakati huo akiwa na miaka 17.

Alichokuwa hajui Mary ni kwamba alikuwa ametumbukia kwenye shimo jingine la mateso na dhiki.

Mpenzi wake, ambaye wakati wa kipindi hicho kifupi cha kuchumbiana alikuwa akimdekeza, aligeuka na kuwa kama chuma baridi.

Yule mumewe Mary alikuwa tayari amempachika mwanamke mwengine mimba, na kwa hivyo hata yule mwanamke mwengine alikuwa anamtembelea mle nyumbani bila kujali uwepo wa Mary.

"Mara nyingi mume wangu alikuwa anawapigia wanawake wengine simu
nikiwa karibu naye. Pia alikuwa na rafiki mwengine wa kike aliyekuwa anamtembelea tulipokuwa tunaishi," anasema.

"Cha ajabu ni kuwa wangekuwa pamoja usiku, huku mimi nikilia pekee yangu."

Mary anasema kuwa hangeondoka kwenye boma la mume wake, baba ya mtoto wake kwani angalao kule kulikuwa na chakula na amani. Lakini mapenzi ya mume hakuyapata.

Kwa kipindi cha miaka mitatu aliishi kwa kunyimwa penzi na mume wake
na ilifika wakati yule mume wake alimfukuza pale nyumbani.

Mary na mtoto wake wa kike walikuwa hawana pa kwenda.

Ni mwanamke mmoja Msamaria mwema aliyempa pa kuishi na vibarua vya hapa na pale kukidhi mahitaji yake ya kila siku.

Uraibu wa ngono

Mary alipoanza kuishi kivyake, mwaka wa 2018 alianza kuwa na tabia isio ya kawaida.

Mary anasema kuwa alitamani kushiriki tendo la ngono na watu tofauti.

Mary anasema kuwa kwa kila siku wakati huo alikuwa hakosi kushiriki ngono.

"Mwili wangu ulikua na shauku sana ya mapenzi, nami nilikuwa na utiifu. Kila mwanamume aliyenitongoza kidogo tu, hata kama tumepatana naye kwa barabara nilikuwa nakubali," anasema.

Anaeleza kuwa ameshiriki tendo la ndoa na wanaume wanaozidi 50, wengi wao wakiwa ni watu ambao hakuwafahamu. Wote alikutanishwa nao na hamu ya tendo la ndoa.

Uraibu huu ulikuwa sugu kwa kiasi cha Mary kutafuta usaidizi kutoka kwa watu.

Usaidizi wa nasaha na pia kuweka maisha yake yakiwa yamejaa shughuli vilimsaidia kuacha hali hii.

"Nihisi kana kwamba hali ya malezi yangu, upweke na kukosa upendwa kulichangia sana mimi kuanza uraibu huu wa ngono," anasema.

"Nilipokuwa nashiriki ngono na mtu nilijihisi nikiwa na thamani na kukubalika. Shida ilikuwa kwamba baada ya ngono wengi walinitoroka," Mary anakumbuka.

Harakati za kuacha tabia hii zimemchukua mwaka mmoja sasa tangu Julai.

Mary anasema katika kipindi hicho, amefanikiwa kutoshiriki tendo la ndoa.

Bi Sadaka Gandi kutoka Dar es Salaam, Tanzania ambaye ni mshauri nasaha anasema kuwa ishara za Bi Mary zinaonyesha wazi mtoto aliyenyimwa penzi la wazazi na ya kukataliwa na watu.

Anasema kuwa wengi wa watoto wanaonyimwa pendo la wazazi hukabiliwa na matatizo ya kutangamana vyema na watu katika jamii wakati wa utu uzima wao.

Bi Sadaka anasema kuwa ule uraibu wake Mary ulikuwa ni ishara ya matatizo ya hisia na mahangaiko ya kutafuta penzi na kukubalika.

Anasema inawezekana mtu mwenye uraibu wa mihemko ya ngono kila wakati kubadilika , kwa kuanza kujielewa na kusahau ya kale, kwa kutafuta njia za kujikubali.

Lakini pia ni muhimu kutafuta usaidizi kutoka kwa daktari wa masuala ya kiakili na kisaikolojia.

Mwanasaikolojia husaidia kuzungumza na mtu kuhusu mambo yaliyojificha katika undani na mtu anapofunguka, hilo husaidia safari ya kujinasua.

________________________________________