Familia ya Zindzi yapongezwa kwa kusema hadharani binti yao alikufa kwa Covid-19

Chanzo cha picha, AFP
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amepongeza familia ya Rais wa kwanza wa nchi hiyo Nelson Mandela kwa kusema wazi kwamba binti yao, Zindzi, alikufa kwasababu ya ugonjwa wa virusi vya corona, Jumatatu.
Hilo litafanya jamii kutonyanyapaa wanafamilia waliopata maambukizi, Bwana Ramaphosa amesema.
Zindzi alizikwa Ijumaa asubuhi kando ya kaburi la mama yake ambaye pia alikuwa mwanaharakati aliyepinga ubaguzi wa rangi Winnie Madikizela-Mandela.
Afrika Kusini ni moja ya nchi za Afrika iliyopata maambukizi ya juu ya ugonjwa wa virusi vya corona ikiwa na zaidi ya maambukizi 320,000.
Kumekuwa na zaidi ya vifo 4,600 na serikali imekadiria kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka hadi 50,000 kufikia mwisho wa mwaka huu.
Licha ya kwamba raia wamefahamishwa kuhusu vile virusi vya corona vinavyosambaa, dalili na athari zake bado kumekuwa na taarifa za unyanyapaa dhidi ya waliopata maambukizi.
Rais Ramaphosa amesema nini?
"Ningependa kushukuru familia ya Mandela kwa mfano mzuri wa kushirikisha taarifa hizi na taifa. Hivi ni virusi ambavyo vinaathiri kila mmoja, na hakustahili kuwa na unyanyapaa wowote miongoni mwa waliopata maambukizi," alituma ujumbe kupitia mtandao wa Twitter kabla ya mazishi ya Zindzi Mandela.
Aliongeza kwamba kusema wazi sababu ya kifo chake, ni ishara ya mshikkamano wa juu zaidi kwa mwanamke aliyejitolea maisha yake kwa raia wenzake wa Afrika Kusini."

Pia unaweza kusoma:

Zindzi Mandela ni nani?
Zindzi Mandela, 59, alikuwa mtoto wa sita wa Nelson Mandela na Winnie Madikizela-Mandela, mke wake wa pili.
Waombolezaji waliokusanyika kwa ibada ya kumuaga Zindzi Mandela mjini Johannesburg walimpongeza kama mpiganiaji wa uhuru.
"Adui asiyeonekana ametupokonya baada ya Bi. Mandela hata baada ya kunusurika risasi, mateso na machungu aliyopata kwasababu ya mfumo wa ubaguzi wa rangi," Nomvula Mokonyane, afisa kutoka chama tawala cha African National Congress, amenukuliwa na tovuti ya shirika la habari la EWN.
"Alinusurika utawala wa kinyama kabisa miaka yake ya utotoni, na tulifikiria kwamba pia angenusurika janga hili na adui huyu asiyeonekana tunayekabiliana naye hii leo, kwasababu amepitia mabaya zaidi kuliko hili," amesema Julius Malema, kiongozi wa chama cha upinzani cha EFF, kulingana na taarifa.

Chanzo cha picha, Reuters
Licha ya umaarufu wa baba yake, Bi. Mandela alikuwa mwanaharakati na alikuwa balozi wa Denmark hadi wakati wa kifo chake.
Alikua wakati wa enzi za ubaguzi wa rangi. Baba yake akiwa amefungwa gereza la Robben Island, alivumilia miaka mingi ya mateso na vitisho kipindi cha ubaguzi wa rangi, pamoja na dada yake Zenani na mama yake Winnie.
Zindzi Mandela ndiye aliyesoma taarifa ya baba yake kukataa ombi la aliyekuwa Rais wakati huo, PW Botha aliyetaka Mandela aachiliwe huru kwa masharti katika mkutano wa hadhara Februari 1985.
Tazama:
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa YouTube ujumbe

Kupitia wakfu wake, aliyekuwa askofu wa mji wa Cape Town na mshindi wa Tuzo ya Nobel Desmond Tutu amesema kwamba "hotuba ya Soweto, kwa niaba ya baba yake... iliimarisha maadili na kanuni za kupigania ukombozi".
Bi. Mandela "alikuwa na jukumu muhimu kuashiria ubinadamu na kujitolea enzi ya ubaguzi wa rangi ", aliongeza.
Hivi karibuni alifahamika kwa kuunga mkono mabadiliko ya suala la ardhi Afrika Kusini.
Wawili tu kati ya watoto sita wa Nelson Mandela ndio ambao sasa hivi wako hai: Zenani Dlamini, dada ya Zindzi; na Pumla Makaziwe Mandela, binti wa ndoa yake ya kwanza, na Evelyn Mase.















