Lazarus Chakwera aapishwa, watu 100 pekee wahudhuria sherehe za kuapishwa kwake

Muda wa kusoma: Dakika 1

Rais mpya wa Malawi Lazarus Chakwera ameapishwa kuwa rais wa sita wa taifa hilo katika sherehe iliyohudhuriwa na wageni 100 pekee katika mji mkuu wa nchi hiyo, Lilongwe.

Sherehe za kuapishwa kwake zimekwenda sambamba na maadhimisho ya sherehe za miaka 56 ya uhuru wa Malawi.

Siku ya Jumapili, Rais Chakwera aliamuru shamrashamra hizo zisifanyike kwenye uwanja wa taifa badala yake kwenye viwanja vya makao makuu ya jeshi kutokana na hali ya maambukizi ya virusi vya corona.

Gazeti moja nchini humo zilitoa picha za shughuli za kuapishwa kwa kiongozi huyo.

Malawi mpaka sasa ina wagonjwa wa virusi vya corona 1,742, na vifo 19.

Wawakilishi kutoka nje ya Malawi hawajahudhuria kwa wingi, Tanzania ikiwakilishwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu akiwa kiongozi wa juu kutoka nje ya Malawi.

Aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Peter Mutharika aliyepoteza kiti kwenye uchaguzi wa marudio, hakuhudhuria kwa ajili ya kukabidhi rasmi madaraka kwa mrithi wake.

Bwana Chakewera alimshinda aliyekuwa rais wa nchi hiyo Peter Mutharika kwa asilimia 58.57 ya kura katika uchaguzi wa mwezi Juni.

Mwezi Februari, Mahakama ya katiba nchini Malawi ilifutilia mbali ushindi wa Mutharika katika uchaguzi wa Mei 2019, kutokana na dosari zilizokumba uchaguzi huo.

Nchi iligawanyika vikali wiki kadhaa kuelekea uchaguzi wa marudio.

Malawi ni nchi ya kwanza Afrika kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais na kuandaa duru ya pili ambayo upinzani ukanyakua ushindi.

Kama ilivyotokea Malawi nchini Kenya upinzani ulipinga matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka 2017 na kushinda mahakamani.

Hata hivyo mgombea wa upinzani Raila Odinga alisusia duru ya pili ya uchaguzi.

Rais Lazarus Chakwera sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuleta nchi pamoja kufuatia mgawanyiko uliojitokeza na kumaliza ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Pia ana kibarua cha kukabiliana na ufisadi, kupunguza umaskini na ukosefu wa ajira, mambo ambayo yalikuwa ni miongoni mwa masuala ya msingi katika uchaguzi huo.