Siku ya akinababa duniani: Maisha ya baba muendeshapikipiki anayelea watoto wadogo peke yake

Kennedy Mwangi Wanderaanasema alitorokwa na mke wake aliyekua mlevi wa kupindukia baada ya kukosana nae kidogo

Chanzo cha picha, Lynn Ngugi/Tuko

Maelezo ya picha, Kennedy Mwangi Wandera anasema alitorokwa na mke wake aliyekua mlevi wa kupindukia baada ya kukosana nae kidogo
    • Author, Na Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC News Swahili

Kennedy Mwangi Washira ni baba Mwendeshapikipiki anaewalea watoto wawili baada ya kuachwa na mke wake ambaye alikua mlevi wa kupindukia. Katika siku ya hii ya Baba au Akinababa duniani, amezungumza na BBC huhusu maisha yake ya malezi na kutoa ushauri akinababa wengine wanaopitia changamoto za kuwalea watoto wao peke yao.

''Mke wangu tulipokutana alikuwa ni mwanamke mzuri sana tukazaa nae mtoto wetu wa kwanza wa kime Erick Mburu na tukapata mtoto wa pili wa kike Jane wairimu, lakini baada ya kupata watoto hawa alianza kuwa mlevi wa kupindukia...nilikua ninakuta mke wangu amelewa chakari, mlango uko wazi na wakati mmoja tulipokosana kidogo akatoroka .'' Anasema Washira

Washira anasema alimuachia mvulana akiwa na umri wa miwili na msichana akiwa na miezi miwili, tangu wakati huo amekua akiwalea peke yake huku akifanya kazi ya kuendesha pikipiki ili aweze kupata riziki ya kuwalea.

''Huwa ninaamka mapema nawatengenezea maziwa au uji laini ninachuja unga na kuwapatia halafu nawalaza. Yule ambaye atakua hajalala ndiye ninaeondoka nae kazini... ninamuacha mwingine'', anasema Bwana Washira na kuongeza kuwa baada ya kuwabeba abiria kwa muda wa saa moja hurejea nyumbani na mtoto mmoja na kuhakikisha anabadilisha nepi zao, kuwapatia chakula na kinywaji na kuhakikisha tena mmoja wao amelala na kuondoka na mwingine kwenye pikipiki.

Washira, humbeba mtoto mmoja ndani ya koti lake na kwenda nae kazini kila siku huku akimuacha mwingine amelala

Chanzo cha picha, Lynn Ngugi/Tuko

Maelezo ya picha, Bwana Washira, humbeba mtoto mmoja ndani ya koti lake na kwenda nae kazini kila siku huku akimuacha mwingine amelala.

''Maisha yangu yamekuwa ni magumu sana, lakini ninajitahidi kung'ang'ana kuwalea watoto wangu kadri niwezavyo, sitamuachia mtu mwingine, mama yao alichagua pombe akawasahau watoto''.

''Watu wengi wamekua wakinifuata kutaka wawachukue watoto wangu eti wanipatie pesa, baadhi hata wakileta fomu za kuwaasili wakitaka nisaini wawachukue, lakini nimekataa kabisa'' anakumbuka.

''Wewe ni mwanaume utaweza kweli kuwalea watoto hawa wachanga na usitupatie tukupe pesa?, wananiuliza, lakini huwa ninawakatalia, nitawalea tu''. anasema Bwana Washira.

Kennedy Mwangi Wandera ahulazimika kuwafahamisha wateja ni kwanini amembeba mtoto wake kwenye pikipiki

Chanzo cha picha, Lynn Ngugi/Tuko

Maelezo ya picha, Kennedy Mwangi Wandera ahulazimika kuwafahamisha wateja ni kwanini amembeba mtoto wake kwenye pikipiki

Anasema, anapoendesha pikipiki humfunika mtoto wake kwa jaketi lake zito na kumfunga kwa kanga/leso ili kumzuwia asipigwe na baridi na upepo mkali.

''Wakati mwingine hata wateja wangu hawagundui kuwa nimembeba mtoto ninapowabeba kwenye pikipiki yangu kutokana na jinsi ninavyomfunika gubigubi, labda pale anapolia ndio wanashangaa na kuniambia: ''Haa! inakuaje unambeba mtoto mchanga kwenye pikipiki?, inabidi niwaeleze kuwa mimi ndiye ninaemlea kwasababu mama yao alitoroka nikabaki nao, na lazima maisha yaendelee...kusema kweli huwa wanashangaa sana'', anasema .

''Wakati wa mvua inakua vigumu sana kwangu kutoka niwaache, inabidi nisiende kazini...inanibidi nikae nao nyumbani''. Anasema Bwana Washira.

Kennedy Mwangi Wandera akiendesha pikipiki huku amembeba mtoto wake Jane Muthoni pamoja na mteja

Chanzo cha picha, Lynn Ngugi/Tuko

Maelezo ya picha, Kennedy Mwangi Wandera akiendesha pikipiki huku amembeba mtoto wake Jane Muthoni pamoja na mteja

Hali ya malezi ya peke yake imemuwea ngumu zaidi Bwana Washira hususan wakati huu ambapo anasema kuna maradhi ya corona na sheria zimewekwa za kuzuwia matembezi.

''Mtoto wangu huyu wa kiume ana tatizo la matege kwasababu ya ukosefu wa vitamini D, hakuwa anatolewa nje na mama yake kuota jua limpige, miguuni ili miguu yake ipate nguvu. Kwa hiyo hua walau kila siku ninamyoosha miguu halafu nampeleka nje na huyu mdogo kwa saa moja wapate jua la vitamini D''

''Wazazi wangu wananisikitikia sana, lakini wako mbali wananiambia corona ikiisha niwapelekee watoto wangu wawalee Nyahururu, lakini kwa sasa nitabaki nao'', anasema.

Bwana Washira anasema kwa sasa hana fedha, lakini baadae akipata uwezo anaweza kujaribu kuoa mke mwingine atakayemsaidia kuwalea watoto.

''Ningepata uwezo kidogo ningemtafuta yaya wa kunisaidia kuwalea, lakini kwa sasa sina pesa ya kumlipa'' anasema.

Ushauri kwa akinababa

Kennedy Mwangi anawashauri akinababa wenzake wawe wavumilivu wanapopatwa na changamoto kuachana na wake zao na kubaki na watoto.

Kennedy Mwangi Washira anawashauri akinababa wanaopatwa na changamoto ya kuwalea watoto wao peke yao wasiwatupe, wang'ang'ane kuwalea

Chanzo cha picha, Kennedy Mwangi Washira

Maelezo ya picha, Kennedy Mwangi Washira anawashauri akinababa wanaopatwa na changamoto ya kuwalea watoto wao peke yao wasiwatupe, wang'ang'ane kuwalea hata kama ni peke yao

''Ninafahamu kuwa wanaume wengi hawawezi kufanya ninayofanya wananiambia wangekimbia wawaache watoto, lakini mambo ni kujikaza, kwa hali na mali. Siku ukipatwa na tatizo kama hili usiwatupe watoto wako...ng'amg'ana nao uwalee na Mungu atakusaidia watakua na utabarikiwa'', anashauri Bwana Washira.

Siku ya baba au siku ya akibaba ni siku ya kuwakumbuka na kuwaheshimu akina baba na uhusiano wetu mababa zetu pamoja na ushawishi walionao akinababa katika jamii. Katika nchi za kikatoliki za Ulaya, siku hii imekua ikisherehekewa Machi 19 kama siku ya mtakatifu Joseph tangu zama za kati. Siku hiyo ilianzishwa na Sonora Smart Dod na huadhimishwa katika Jumapili ya tatu ya mwezi wa Juni kwa mara ya kwanza mwaka 1910. Husherehekewa kwa siku tofauti katika maeneo mengi ya dunia mara nyingi katika miezi ya Machi na Juni.