Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je 'utawala wa kidini ' ulioachwa na Nkurunziza utaendelezwa?
- Author, Na Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC News Swahili
Hayati Pierre Nkurunziza aliyekuwa rais wa Burundi aliyefariki dunia ghafla tarehe 8 Juni, atakumbukwa miongoni mwa mambo mengine kama kwa ''uongozi uliotawaliwa na itikadi za kikristo''. Lakini je itikadi hizi zitaendelezwa na mrithi wake Meja Pierre Ndayishimiye?.
Kiongozi huyo wa Burundi alikufa kutokana na ugonjwa ambao serikali ya Burundi iliutaja kama 'mshutuko wa moyo'. akiwa na umri wa miaka 55.
'Uongozi na itikadi za kikristo''
Licha ya kwamba Burundi imekuwa katika vipindi mbali mbali vya ghasia zilizosababishwa vifo na maelfu ya raia kuikimbia nchi yao, huenda wasichokifahamu wengi ni kwamba uongozi wa miaka 15 wa Pierre Nkurunziza umetawaliwa na itikadi za Kikristo.
Alitumia fursa yake ya uongozi kueneza injili ya Kikristo kupitia mikutano ya hadhara na katika sherehe na ziara zake za kitaifa alieneza neno la ''Mungu kwa nukuu za aya na mistari ya kitabu cha Biblia''.
Mafundisho yake ambayo yalijaa utabiri kwa nchi ya Burundi pamoja na watu wake, yaliifanya hadhira yake kujawa na hamasa na hata baadhi kuamini kuwa alikua ni kiongozi aliyewekwa madarakani na Mungu kwa ajili ya kuwaokoa Warundi na matatizo waliyonayo.
Bwana Nkurunziza ambaye binafsi alikuwa ni mfuasi wa dini ya wokovu (mlokole), sawa na mkewe Bi Denise Macumi Nkurunziza walianzisha mikutano na shughuli zote za kitaifa kwa sala na maombi yaliyosheheni nyimbo za injili zilizoimbwa na kwaya zilizoimbwa, ambazo zilimtumbuiza Nkurunziza na umma wakati wote.
Hili halikuwa jambo la ajabu kwani licha ya kuwa Mke wa rais, Bi Denise Nkurunziza ni muhubiri, maarufu kwa maombi na mwalimu wa neno la Mungu, pia ni muimbaji na mtunzi maarufu wa nyimbo za injili na muimbaji wa kwaya.
Itikadi ya ukristo na Covid-19
Kabla ya mauti yake, marehemu Nkurunziza aliwaelezea mara kwa mara Warundi kuwa Burundi imeepushwa na Mungu virusi vya corona:'' Hebu fikiria…mnafikiri ni kwanini Burundi hatuna corona?...ni mkono wa Mungu upo juu ya Warundi. Fikiria mchungaji kutoweza kuwahubiria kondoo wake akiwatazama?. Sisi tunawezaje kuendelea na shughuli zetu , kwenda sokoni, mashambani na kuendeleza biashara zetu ...Kuna aliyevaa barakoa hapa?. Ni mkono wa Mungu unatulinda'', alisikika Nkurunziza akisema katika mojawapo ya mikutano yake ya umma.
Katika mikutano ya umma mara kwa mara kiongozi huyo wa zamani wa Burundi ambaye zamani alikua muasi, alionekana alichanganyikana na umati wa watu na kupuuza maagizo yaliyotolewa na Shirika la afya duniani -WHO ya kuzuwia kusambaa kwa virusi vya corona.
Burundi iliwafukuza wawakilishi wa WHO nchini humo kabla ya uchaguzi na ikawaonya waangalizi wa uchaguzi wa kikanda kuwa watawekwa karantini kwa siku 14 watakapokwenda Burundi kufuatilia uchaguzi wa urais.
Katika mikusanyiko ya kisiasa ikiwemo ya kampeni za uchaguzi yeye na wafuasi wake hawakuchukua tahadhari za kuzuwia maambukizi ya Covid-19 kama vile kuvaa barakoa, wala ile ya watu kukaa umbali wa mita moja na wala kuepuka misongamano ya watu.
Taarifa za awali zilisema kuwa mkewe Bi Nkurunziza,50, alisafirishwa kwa ndege kutoka Bujumbura hadi Nairobi Mei 28 kutibiwa ugonjwa wa ambao mpaka sasa haujawekwa wazi.
Maafisa katika ofisi ya rais nchin Burundi walipinga ripoti kwamba Bi. Nkurunziza alipelekwa Nairobi kutibiwa virusi vya corona.
Aliamini kuwa alikua ni kiongozi aliyewekwa na Mungu.
Wakati mmoja yeye na mkewe Denise waliripotiwa kuosha miguu ya baadhi ya watu waliokua kwenye umati.
Wakati wa uongozi wake sio watu pekee ambao rais aliamini kuwa wanaimani nae:
"Bwana Nkurunziza kusema ukweli anaamini alipata urais kwam mapenzi ya Mungu, kwahiyo huishi maisha yake na serikali kwa kuzingatia maadili haya, alisema aliyekua msemaji wake Willy Nyamitwe.
Licha ya kwamba wakosoaji wake, wakiwemo wafuasi wa vyama vipatavyo 40 vya upinzani pamoja na makundi ya kutetea haki za binadamu walikua na picha tofauti kumuhusu, falsafa yake ya kuongoza nchi kwa itikadi za kikristo ameiendeleza hadi mauti yalipomfika.
Je alikua''uchamungu'' kabla ya kuwa rais?
Kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, Bwana Nkurunziza, ambaye alifuzu Shahada ya Elimu ya michezo katika Chuo Kikuu, alikua mwalimu Chuo Kikuu cha Burundi.
Alianzisha timu yake binafsi, Hallelujah FC, ambapo ''alicheza kama mshambuliaji na mara kwa mara alifunga magoli".
Jina la timu yake pia liliashiria moja ya mambo anayoyaenzi sana : Imani yake ya Ukristo.
Baba yake, ambaye alikua gavana wa zamani aliyeuawa katika mauaji dhidi ya watu wa kabila la Wahutu mwaka 1972, alikua ni Mkatoliki na mama yake alikua mfuasi wa dini ya Anglikana.
Ilikua ni nadra sana kwa Nkurunziza ambaye alikua ni baba wa watoto watano kusafiri nchini mwake bila timu yake ya soka pamoja na kwaya , ambapo alichanganya mechi za timu yake dhidi ya timu za maeneo aliyotembelea na maombi ya kiinjili.
Je falsafa ya uongozi unaoegemea dini itaendelea?
Katika mitaa ya mji mkuu Bujumbura, baadhi wanasema watamkumbuka Bwana Nkurunziza, kwa mahubiri yake na kwa mambo mema aliyoitendea nchi yao.
"Nitamkumbuka kwa ushauri aliotupa. Mara kwa mara alituambia tuipende nchi yetu. Alimuweka Mungu mbele na mtu ambaye anafanya hivyo hawezi kupata matatizo maishani mwake ," alisema mkazi mmoja wa Bujumbura ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Mrithi wake, Rais mteule Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye alikua mshirika wa karibu wa Bwana Nkurunziza.
Kufuatia kifo cha mtangulizi wake, wiki iliyopita Meja Ndayishimiye alitoa hotuba iliyojaa maneno ya kumshukuru Mungu kwa hali ya utulivu iliyopo baada ya kifo Nkurunziza Burundi:
''Kwangu mimi nauona kama muujiza wa Mungu, kuona Warundi wote wametulia, kwa aliyeshuhudia histopria ya Burundi hawezi kuamini hili''. Tutulie kwasababu mzazi wetu hakutuacha peke yetu, inaonekana kuwa tunaona kuwa sisi si yatima, tuko katika familia moja yenye watoto wakubwa wanaojua mema na mabaya, wanaojua ni wapi wanaenda...alitulea mwenyewe [Nkurunziza] akatuondoa katika mioyo ya unyama akatuweka katika kumpenda Mungu, ili tuwe na moyo wa kumpenda Mungu...alipata muda wa kutukuza katika neno la Mungu kutufanya watu katika nchi yetu. Kwahiyo kila mtu wakati huu ajue kuwa tuko nyumbani mwa Mungu. Mungu yuko pamoja nasi, kwani alitufundisha kumuita Mungu nchi akaja Burundi kwahiyo tuko nyumbani mwa Mungu ni Mungu anayetulinda...'' alisema Ndayishimiye.
''Mimi na mtangulizi wangu tulimtolea Mungu nchi...tulifanya agano na Mungu akaja nchini mwetu'',aliongeza rais mteule Nayishimiye.
Kutokana na hotuba ya Bwana Ndayishimiye na ushirika wa karibu aliokuwa nao na Pierre Nkurunziza, baadhi wanahisi kuwa huenda akaendeleza falsafa ya uongozi unaoambatana na itikadi za kidini sawa na mtangulizi wake.
Hata hivyo huenda ikawa ni mapema sana kubaini iwapo Meja Ndayishimiye ataendeleza mtindo wa mtangulizi wake wa kuwarai Warundi kwa kutumia injili, au ataamua kubuni mtindo wake mwenyewe wa uongozi baada ya kula kiapo rasmi kama rais mpya wa Burundi Alhamisi wiki hii.