Rwanda yampongeza rais mteule wa Burundi, je huu ndio mwanzo mpya?

Siku moja baada ya Serikali ya Rwanda kutuma risala ya pongezi kwa rais mteule wa Burundi Meja Jenerali Everiste Ndayishimiye mjadala umeibuka ikiwa nchi hiyo ina nia ya kukomesha mzozo kati yake na Burundi.

Hii ni baada ya Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Rwanda kutumia fursa hiyo kusema kwamba nchi hiyo iko tayari kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo.

Rwanda na Burundi ni nchi zenye kabila,utamaduni na lugha moja lakini uhusiano wao ulikuwa mbaya tangu mwaka 2015 kufwatia uchaguzi wenye utata wa rais Pierre Nkurunziza anayeondoka madarakani.

Tangu wakati huo nchi hizo mbili zimekuwa zikishutumiana kuunga mkono makundi ya waasi kutoka kila upande.Risala ya pongezi kwa rais mteule wa Burundi jenerali Evariste Ndayishimiye imetumwa na Wizara ya Mambo ya nchi za nje ya Rwanda ambayo imepongeza serikali ya Burundi kwa uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita.

Ni risala iliyozua hisia mbali mbali kwenye mitandao ya kijamii,raia wa Burundi na raia wa Rwanda wakichangia maoni. Badhi yao wamepongeza hatua hiyo.

Kuna waliohoji kwa nini siyo rais wa Rwanda Paul Kagame aliyempongeza rais mteule wa Burundi kama ilivyotokea kwa marais wengine wa mataifa ya Kenya,Tanzania na Uganda na badala yake risala hiyo kuandikwa na wizara ya mambo ya nchi za nje.

Kulingana na risala hiyo,Wizara ya Mambo ya nchi za nje ya Rwanda imesema inatumia fursa hiyo kuikaribisha Burundi kusema kwamba Rwanda iko tayari kurejesha mahusiano yaliyotajwa kuwa ya kihistoria baina ya nchi mbili.

Rwanda na Burundi zilikuwa nchi moja iliyofahamika kama Rwanda-Urundi,mji mkuu ukiwa Usumbura,Bujumbura ya sasa,chini ya ukoloni wa Ubelgiji,zikiwa na kabila zinazofanana,utamaduni na lugha moja.

Mahusiano hayo yalikatika mwaka 2015 Rais wa Burundi anayeondoka madarakani Pierre Nkurunziza alipojichagulisha kwa muhula mwingine madarakani uliozua utata na kufwatiwa na machafuko ya kisiasa.

Tangu wakati huo nchi mbili ziliingia katika kipindi kigumu cha kushutumiana kuunga mkono makundi ya waasi,Burundi iliihusisha Rwanda na jaribio lililoferi la kutaka kumpindua rais Pierre Nkurunziza mara tu baada ya uchaguzi huo ambapo Rais Nkurunziza aliitangaza Rwanda kuwa adui mkubwa wa Burundi.

Rwanda kwa upande wake imekuwa ikiishutumu Burundi kuunga mkono makundi ya waasi yaliyodai mashambulio yaliyotikisa maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Burundi miaka 2 iliyopita.

Pia unaweza kusikiliza: