Virusi vya corona: Idadi ya watu waliopatwa na virusi yazidi 1000 Kenya

Idadi ya watu waliopatwa virusi vya corona yazidi 1000 Kenya, baada ya visa vipya 66 kupatikana katika kipindi cha saa 24 zilizopita, idadi hii ikiwa ni ya juu zaidi kuwahi kutangazwa ya visa vya maambukizi ya virusi kwa siku tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kiliporipotiwa nchini humo mwezi Machi.

Idadi hiyo inaifanya Kenya kuwa na jumla ya wagonjwa 1,029 vya maambukizi ya virusi vya Corona.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano, Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe amesema kuwa miongoni mwa visa 62 ni Wakenya na wawili ni raia wa kigeni.

Jumatano Kenya ilipokea maabara zinazoweza kuhamishwa na vifaa vya kupima kutoka Ujerumani vitakavyosaidia kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 huku idadi ya visa vya maambukizi ikizidi 1,000 .

Bwana Kagwe ametangaza pia kuongezwa kwa muda wa udhibiti wa matembezi ya kuingia na kutoka katika maeneo ya Eastleigh jijini Nairobi na Makazi ya Old Town yaliyopo katika Kaunti ya mwambao wa Kenya- Mombasa hadi kufikia tarehe 6 Juni.

Katika siku za hivi karibuni Wizara ya Afya nchini Kenya imekua ikitangaza kuongezeka kwa viwango vya juu kwa maambukizi ya Covid-19 katika Kaunti ya Mombasa ambapo jana pekee ilirekodi visa 27, na kulipita jiji la Nairobi ambalo lilirekodi visa 20.

Jumatatu maeneo mapya yalirekodi visa vipya vya virusi vya corona mkiwemo kaunti za Taita Taveta, Garissa na Meru.

Mpango unaolengwa kwa sasa ni kuwapima watu wengi.''Tumepokea vifaa vya kupima ndio maana tumeongeza shughuli ya upimaji'', alisema Katibu tawala wa waziri wa Afya Rashid Aman Jumatatu.

Athari za kuongezeka kwa maambukizi ya corona Kenya:

Kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona kumeilazimisha Kenya Kufunga mipaka yake na mataifa jirani, na kuruhusu magari pekee ya mizigo kuingia nchini humo.

Hatua hiyo ilielekea kuwakera baadhi ya maafisa wa Tanzania ambao walijibu kwa kutangaza kuzuwia magari yanayotoka nchini Kenya kuingia Tanzania.

Hii ilimlazimu Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu, jana kutetea hatua ya Kenya kufunga mpaka na majirani zake akisema kuwa haiwalengi Watanzania.

"Uamuzi ambao Kenya imechukua kuhusu safari za mipakani sio kwasababu ya Tanzania bali adui yetu ni kirusi", alisema Balozi Kazungu, Jumanne.

Katika mazungumzo yake na wanahabari jijini Dar es Salaam Balozi Kazungu alisema Kenya na Tanzania ni nguzo ya uchumi katika kanda ya Afrika Mashariki na kutoa wito kwa raia wa chi hizo mbili kuwa na subira na kudumisha uhusiana mwema kati yao.

Balozi huyo alichukuwa fursa hiyo kuelezea hali ya corona nchini Kenya ambayo iliifanya Kenya kuweka mikakati kudhibiti maambukizi.

Kufikia sasa Kenya ina jumla ya watu 912 walioambukizwa virus via corona.

Bwana Kazungu alisema kuwa tayari nchi mbili zinafanya mazungumzo ili kupata suluhu ya mzozo huo kufikia mwishoni mwa juma.

Hayo yalijiri baada ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kufunga kwa siku 30 mipaka ya chi hiyo na Tanzania na Somalia ili kudhibiti maambukizi ya corona.