Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Burundi: Wachunguzi wa kimataifa kuwekwa karantini
Huku ikiwa imesalia siku 10 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Burundi, serikali imesema kwamba wachunguzi wote wa uchaguzi utakaofanyika tarehe 20 Mei 2020 watalazimika kufuata maagizo ya kukabiliana na virusi vya corona.
Hii ina maana kwamba wachunguzi wote ambao wanalenga kwenda katika taifa hilo ili kusimamia uchaguzi huo watalazimika kwenda karantini kwa siku 14 kuanzia siku watakapowasili nchini humo.
Na huku ikiwa imesalia siku 10 kabla ya shughuli hiyo ya kidemokrasia kufanyika, hatua hiyo inamaanisha kwamba wachunguzi kutoka mataifa ya kigeni hawataweza kuingia nchini humo.
Hatahivyo Ikijibu barua ambayo ilikuwa imeandikiwa na serikali ya Burundi tarehe 24 Aprili , kuhusu masharti hayo ya kukabiliana na corona, Jumuiya ya Afrika mashariki imesema kwamba italazimika kuwatumia maafisa wake waliopo nchini humo kusimamia shughuli hiyo.
Haijulikani iwapo serikali hiyo inatumia masharti hayo kujaribu kuwafungia wachunguzi kutoingia nchini humo.
Lakini kufuatia hatua hiyo Jumuiya hiyo imeitaka serikali ya Burundi kuwaruhusu maafisa hao ambao hawatalazimika kufuata sheria hizo kushiriki katika uchunguzi kwa niaba yake.
Uamuzi huo wa Jumuiya ya Afrika mashariki pia huenda ukaigwa na mataifa ya Ulaya ambayo pia yana hamu ya kuchunguza uchaguzi huo ili ufanyike kwa kidemokrasia .
Hatua hiyo inajiri baada ya polisi nchini humo kuwakamata watu wapatao 64 kutoka chama kikuu cha siasa cha CNL.
Kumekuwa na ghasia pamoja na mauaji dhidi ya wanachama wa chama kikuu katika kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa rais tarehe 20 Mei.
Mgombea wa nafasi ya ubunge Cathy Kezimana, kutoka chama cha National Freedom Council (CNL) alikamatwa wiki iliopita baada ya kufanya kampeni kusini mwa nchi hiyo.
Mapema wiki iliopita, msemaji wa polisi Pierre Nkurikiye alikiambia chombo cha habari cha taifa kuwa vurugu nyingi na uhalifu katika kampeni unafanywa na wanachama wa CNL dhidi ya wapinzani wao CND-FDD, ambacho ni chama tawala.
Bwana Nkurikiye alisema ghasia hizo mpaka sasa zimesababisha wanachama wa chama tawala wawili kuuliwa na wengine 18 kujeruhiwa na mmoja hajulikani alipo na wanachama nane kutoka CNL wamejeruiwa.
"Uhalifu huu umefanywa zaidi na wanachama wa CNL wakiwa wanahamasishwa na viongozi wao .Kutokana na matukio hayo 64 kati yao wamekamatwa wakati uchunguzi ukiendelea." - alisema bwana Nkurikiye.
Msemaji wa CNL, bwana Terence Manirambona, aliiambia BBC kuwa wameshangazwa na maoni ya bwana Nkurikiye kwa sababu hawakutarajia kusikia maneno hayo kutoka kwake kwa kuwa wanategemea vyombo vya usalama kuwa na haki sawa kwa wote".
Bwana Manirambona alisema wanachama wa chama chake wamekuwa wahanga wa vurugu hizo na unyanyasaji ulioanza hata kabla ya kampeni kuanza.
"Tangu kampeni zianze, wanachama wetu wengi walikamatwa kwa madai ambayo hayana ukeli, wawili walipotea na wengi walijeruhiwa katika ghasia hizo ambazo zimeanzishwa na wanachama wa chama tawala ambao waliingilia shughuli zetu," - bwana Manirambona aliiambia BBC.
'Hakuna tisho la kutosha kuahirisha uchaguzi'
Serikali ya Burundi imefunga mipaka yake ili kuzuwia kusambaa kwa virusi, na kuruhusu shehena za malori ya mizigo tu kuingizwa nchini kutoka mataifa jirani.
Ndani ya nchi, watu wameshauriwa kutosalimiana kwa mikono na kunawa mikono mara kwa mara, na maisha yanaendelea kama kawaida.
Taifa hilo limerekodi visa 14 vya Covid-19, na serikali imesisitiza kuwa bado hakuna tisho la kuifanya iahirishe uchaguzi mkuu.
Alipotazama picha za mikutano ya kisiasa, Dkt Olivier Manzi mtaalamu wa mamgonjwa ya maambukiziameiambia BBC kuwa hayo ni maeneo yanayoweza kuwa kitovu cha maambukizi ya virusi vya corona.
Dkt. Manzi ambaye anafanya kazi katika Shirika la Afya Duniani (WHO), ameiambia BBC kuwa mikusanyiko hiyo ni maeneo yanayosambaza kwa kasi virusi vya corona.