Jack Ma: Bilionea anayejaribu kumaliza virusi vya corona na kurejesha hadhi ya China kuwa juu

Mwanzilishi mwenza wa Alibaba Group Jack Ma

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanzilishi mwenza wa Alibaba Group Jack Ma

Tajiri zaidi China alifungua akaunti yake ya Twitter mwezi uliopita, katikati ya mlipuko wa janga la corona. Hadi kufikia sasa, wanaomfuata wamejitolea katika kampeni ya kuwasilisha vifaa vya kitabibu dhidi ya ugonjwa wa covid 19 kwa karibu kila nchi kote duniani.

"Dunia moja, kupambana kwa pamoja!" Kujitolea ni moja ya ujumbe wa kwanza wa Jack Ma "Pamoja, tutafanikiwa!" alisema.

Mfanyabiashara huyo tajiri ndio kichocheo cha operesheni inayoendelea ya kusambaza vifaa vya kimatibabu ambayo hadi kufikia sasa zaidi ya nchi 150, zimepokea barakoa na mashine za kupumua.

Lakini wakosoaji wa Ma na hata baadhi ya wanaomuunga mkono hawajaelewa nia yake. Je tajiri huyu amejitoa kama Rafiki wa chama tawala cha China cha Kikomunisti? Au je ni mshirika binafsi anayetumiwa na chama hicho kwa nia za propaganda?

Anaonekana kufuata sheria za kidiplomasia za China, hasa wakati anapochagua ni nchi gani itafaidika na msaada wake, lakini nguvu yake inayoendelea kuongezeka huenda ikamuweka kwenye njia panda dhidi ya viongozi wenye wivu katika ngazi ya juu ya kisiasa nchini China.

Mabilionea wengine pia wameahidi kutoa msaada zaidi katika kukabiliana na janga la virusi vya corona - huku mkurugenzi na mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Twitter Jack Dorsey akiahidi kutoa $1bn (£0.8bn). Shirika la Marekani linalofuatilia michango inayotolewa na mashirika ya kutoa misaada limemuweka Alibaba katika nafasi ya 12 katika orodha ya wachangiaji wakubwa binafsi katika kukabiliana na janga la corona.

Lakini orodha hiyo haijumuishi usambazaji wa vifaa vya msingi ambavyo baadhi ya nchi wanavichukulia kuwa na umuhimu mkubwa hata kuliko pesa katika kipindi hiki cha kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.

Jack Ma (kulia) akiwa na Rais wa Marekani Donald Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mfanyabiashara Ma ni kichocheo cha operesheni inayoendelea ya kusambaza vifaa vya kimatibabu ambayo hadi kufikia sasa zaidi ya nchi 150 zimefaidika

Hakuna mwingine kati yao zaidi ya Ma ameweza kusambaza vifaa vya msingi kwa wanaohitaji moja kwa moja. Kuanzia Machi, Jack Ma mwanzilishi wa kampuni ya Alibaba alianza kusambaza bidhaa za msingi za kukabiliana na corona kwa Afrika, Asia, Ulaya, Amerika Kusini na hata kwa nchi zenye siasa nyeti kama vile Iran, Israel, Urusi na Marekani.

Ma pia amewasilisha msaada wa mamilioni ya pesa katika utafiti wa chanjo dhidi ya virusi vya corona na kijitabu kidogo cha wataalamu wa tiba kwa madaktari katika mji wake wa Zhejiang kimefasiriwa kutoka Kichina hadi nchi zingine 16. Lakini meli za usambazaji wa vifaa vya kimatibabu ndio kumekuwa mada katika vyombo vingi vya habari duniani na kumfanya Ma hata kuendelea kuwa maarufu.

"Ana uwezo na pesa na uwezo wa kupata ndege itakayoondoka mji wa Hangzhou nchini China hadi Addis Ababa, au popote kule anapotaka iende," anaelezea mwandishi wa wasifu wa Ma, Duncan Clark. "Huu ni utaratibu; hivi ndivyo ilivyo kwa kampuni, watu wake na mji wake."

Mtu Rafiki

Jack Ma anafahamika kama mwalimu wa lugha ya Kiingereza mwenye haiba kubwa ambaye alianzisha kampuni kubwa ya teknolojia. Alibaba kwasasa anafahamika kama "Amazon ya Mashariki".

Ma alianzisha kampuni ndani ya nyumba yake ndogo pwani ya China mji wa Hangzhou, katikati ya eneo la kiviwanda 1999. Tangu wakati huo, Alibaba amekuwa akiendelea kukua na kuwa miongoni mwa washikadau wakuu katika nchi hiyo ambayo ni ya pili kiuchumi duniani, akiwa amekumbatia zaidi nyanja ya kimtandao China, benki na burudani.

Thamani ya Ma ni zaidi ya dola bilioni 40.

2018, alijiondoa rasmi kama mwenyekiti wa kampuni ya Alibaba na kusema kwamba sasa ataangazia zaidi masuala ya misaada. Lakini Ma amedumisha nafasi yake kama mwanachama wa kudumu katika bodi ya kampuni hiyo. Utajiri wake na umaarufu wake umemfanya kuendelea kuwa maarufu nchini China.

Maelezo zaidi

Inaonekana kana kwamba ufadhili wa Bwana Ma unafuata miongozo ya chama tawala cha China: Hakuna ushahidi wowote kwamba ufadhili wa Jack Ma au kutoka kwa kampuni yake ya Alibaba umekwenda kwa nchi zenye uhusiano rasmi na China kama vile Taiwan, majirani wao na mahasimu wa masuala ya kidiplomasia. Ma alitangaza kupitia Twitter kwamba alikuwa anafadhili nchi 22 za Amerika Kusini.

Nchi ambazo zimekuwa zikiunga mkono Taiwan lakini pia zimetoa wito wa kusaidiwa kwa vifaa vya kimatibabu - kuanzia Honduras hadi Haiti - ni miongoni mwa nchi chache ambazo hazionekani kuwa miongoni mwa 150 zilizopokea msaada wa Jack Ma. Wakfu wake ulikataa kutoa orodha ya nchi ambazo zimepokea msaada tayari na kuelezea kuwa kwa wakati huu wakfu huo hauko tayari kushirikishana taarifa za kiwango hicho.

Hatahivyo, michango hiyo ambayo tayari imeshatolewa bila shaka imepokelewa kwa nia njema na kujenga urafiki. Mbali na matatizo ya uwasilishaji wa vifaa hivyo kwa nchi za Cuba na Eritrea, meli zote zilizosafirisha vifaa vya kimatibabu kutoka China zimepokelewa vizuri. Hilo linampa Ma, umaarufu hata zaidi kuliko ilivyo kawaida. Chombo cha habari cha China kinachomilikiwa na serikali, kimekuwa kikimtaja Ma, karibia kila mara kama ilivyo kwa kiongozi mkuu wa nchi hiyo, Xi Jinping.

Jack Ma

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jack Ma

Ni ulinganisho usio wa kawaida. Ma anaendelea kupongezwa, huku rais Xi akikabiliwa na maswali chungu nzima kuhusu namna alivyokabiliana na virusi hivyo punde tu ugonjwa wa virusi vya corona ulipoingia.

Serikali ya China imetuma msaada wa kimatibabu na ufadhili mwengine kwa kiasi kikubwa tu kwa nchi zilizokabiliwa vikali na janga la corona hususan, Ulaya na Kusini-Masharki mwa Asia. Hatahivyo, juhudi hizo wakati mwengine zimekosolea. China imeshtumiwa kwa kutuma vifaa vyenye kasoro kwa nchi kadhaa.

Inasemekana kwamba kwa baadhi ya nchi vipimo ilivyotuma vya kupimia vilikuwa vinatumiwa vibaya lakini nchi zingine zilipokea msaada wa vifaa ambavyo havikukidhi kiwango kilichowekwa.

Tofauti na msaada wa Jack Ma, umekuwa ukiimarisha hadhi yake.

"Itakuwa sawa kusema kwamba msaada wa Ma umefurahiwa kote barani Afrika," anasema Eric Olander, mhariri wa tovuti ya China Africa Project.

Ma ameahidi kutembelea nchi zote Afrika licha ya kwamba amekuwa mgeni wa mara kwa mara barani humo tangu alipostaafu.

Kuwa katika njia panda

Lakini Je hatua ya Ma ya kutoa msaada kwa nchi mbalimbali kunamfanya kujiweka katika hatari ya kukosolewa nchini China? Xi Jinping hafahamiki kama mtu ambaye huwa yuko tayari kuwekwa katika angalizo moja na mwengine na bila shaka serikali yake imekuwa ikilenga watu mashuhuri hapo kabla. Katika miaka ya hivi karibuni, muigizaji mashuhuri, mwanahabari tajika na wajasiriamali wengine mabilionea, wamepotea kwa kipindi kirefu sana.

Baadhi yao ni pamoja na wanahabari ambao wameishia kuwa wafungwa. Wengine wameachiliwa baada ya kuzuiliwa kwa muda na serikali, kuadhibiiwa na wanapotoka wanaahidi kuwa waaminifu kwa chama.

"Kuna uvumi kwamba [Jack Ma] alijuzulu 2018 kama mwanachama wa kampuni ya Alibaba kwasababu alionekana kama mjasiriamali wa nyumbani ambaye umaarufu wake ungepita ule wa chama cha Kikomunisti," anaelezea Ashley Feng, mtafiti mshiriki katika kituo cha Usalama wa Marekani mjini Washington DC. Ma alishangaza wengi baada ya kuamua kujiuzulu ghafla mnamo 2018. Amekuwa akikanusha uvumi wa kwamba China ilimlazimisha kuachia wadhfa huo.

Jack Ma katika mkutano Hangzhou mwaka 2019

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jack Ma katika mkutano Hangzhou mwaka 2019

Duncan Clark, mwandishi wa wasifu wa Bwana Ma, pia naye anafahamu kuhusu taarifa za kwamba alilazimishwa kujiondoa kwenye kampuni ya Alibaba baada ya kisa kilichotokea Januari 2017. Bilionea huyo wa China alikutana na Rais Donald Trump akiwa tu ndo ameteuliwa katika eneo la Trump Tower, kuzungumzia masuala ya kibiashara. Rais wa China hakuwahi kukutana na Donald Trump hadi miezi ya baadae.

"Kulikuwa na wasiwasi mkubwa wakati huo kwamba Jack Ma alikuwa amefanya haraka mno," Clark anasema. "Nafikiri pande zote mbili zilijifunza kuwa na uhitaji wa kuwasiliana na kuratibu mambo."

Kiukweli ni kwamba, Ma pia ni mwanachama wa Kikomunisti: Tajiri huyo amekuwa mwanachama wa chama cha Kikomunisti tangu miaka ya 1980, alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu.

Lakini Ma amekuwa na uhusiano wa paka na panya na chama hicho, nia yake chamani ikifahamika kama "mwenye kupenda lakini asiyekuwa tayari kuoa".

Duncan Clark anasema kwamba Ma tayari ana nafasi yake ya juu nchini China kwasababu ya mchango wa kampuni yake ya Alibaba kiuchumi. Hatahivyo, kufahamikiana kwake na viongozi mbalimbali duniani, kunamfanya kuwa na manufaa zaidi kwa Beijingi wakati ambapo nchi hiyo inajitahidi kurekebisha twasira yake iliyokuwa imeingia dosari.

Ma akiwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ma akiwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

"Ameonesha uwezo wa kuwasiliana na viongozi kadhaa katika nchi za nje, kuwa na marafiiki na kushawishi wengine. Yeye ni Dale Carnegie wa China na bila shaka hilo limeonekana kuudhi baadhi ya watu serikalini nchini China lakini kwa kipindi hiki juhudi za kila mmoja zinahitajika," Clark amesema.

"Wanachukua nafasi ya uongozi, kama jukumu lililochukuliwa na Marekani," anasema. "Mfano mzuri ni mlipuko wa janga la Ebola 2014. Marekani ilituma madaktari na kila kitu Afrika magharibi kusaidia kukabiliana na virusi kabla ya kuachia jukumu hilo lwa nchi za Afrika magharibi."

Wafadhili wa China wamejukua jukumu ongozi katika kukabiliana na virusi vya corona.

Na huu sio wakati muafaka wa China kusimama katikati ya njia ya Jack Ma.

"Unajua, hili ni janga kote duniani kwasasa, Duncan Clark anasema. "Lakini pia ni wakati wa kutathmini uhusiano wa China na sehemu nyengine ya dunia. Kwahiyo, nchi hiyo inahitaji mtu yeyote ambaye anaweza kuisaidia kukabiliana na shinikizo hilo."