Virusi vya Corona: Kwa nini Wamarekani weusi wameathirika zaidi na virusi?

Pallbearer exit a funeral in Brooklyn

Chanzo cha picha, Reuters

Kwa Wamarekni wengi, jinsi suala la rangi ya mwili linavyojitokeza kwa misingi ya idadi ya wanaokufa kwa virusi vya corona ni jambo lisiloshangaza.

Miji ya Chicago, New Orleans, Las Vegas, Maryland na South Carolina ni miongoni mwa ile ambayo imeanza kutoa takwimu zao kwa misingi ya rangi, na kubainika wazi kwamba walioathirika zaidi ni watu weusi.

Huku sababu ya hili ikiwa huenda imechangiwa na tatizo la muda mrefu la ukosefu wa usawa kiasi kwamba limezoeleka, sababu zingine huenda hazikutarajiwa na pengine zingeweza kukabiliwa.

Fuatilia simulizi za watu watatu wakizungumzia walichopitia baada ya kuathirika na janga la corona kwa namna mbalimbali - simulizi zao zinaelezea kwa nini watu weusi wapo katika hatari zaidi.

Short presentational grey line

'Virusi vinateketeza jamii'

"Dada yangu Rhoda alikuwa kiongozi wa familia. Alikuwa wa kwanza katika familia yetu kwenda Chuo Kikuu, kupata shahada na kuwa mwalimu katika shule ya umma," anasema Mchungaji Marshall Hatch wa Chicago.

"Alikuwa mtu mkarimu na rafiki. Mtu mkweli. Mwenye haiba."

Mchungaji Hatch alikuwa karibu sana na dada yake ambaye mara nyingi alikuwa anashiriki kanisani katika majukumu mbalimbali. Lakini Rhoda mwenye umri wa miaka 73 aliaga dunia Aprili 4, baada ya kuwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku 8.

Siku mbili kabla ya kifo chake, rafiki mkubwa wa Mchungaji Hatch, Larry Harris, pia alikufa. Alikuwa na umri wa miaka 62. Wote walikuwa wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Reverend Marshall Hatch

Chanzo cha picha, Submitted photo

Maelezo ya picha, Mchungaji Marshall Hatch na dada yake Rhoda

Ukweli ni kwamba hadi kufikia sasa watu wanne wa karibu na Mchungaji Hatch wamekufa kutokana na virusi hivyo na anauzungumzia kama ugonjwa unaoathiri zaidi Wamarekani weusi walio jirani na eneo la West Garfield Park anakoishi.

"Tumekuwa tukijaribu kutafuta mahali pa kumzika dada yangu siku ya Jumamosi lakini huu umekuwa mtihani mgumu sana," Mchungaji anasema.

"Lakini ni kama tungeweza kutabiri toka mwanzo kwamba iwapo janga kama hili litatokea, lingeathiri zaidi wale wanaopitia wakati mgumu kiuchumi."

Kulingana na takwimu za sensa, West Garfield Park tayari kiwango cha maisha anachotarajiwa kuishi mtu mweusi ni cha chini kwa miaka 16 ikilinganishwa na eneo la wazungu ambalo lipo umbali wa maili tatu kutoka hapo.

Takwimu zilizotolewa hadi kufikia sasa zinaonesha kuwa asilimia 68 ya vifo vinavyosababishwa na corona katika mji huo ni vya watu weusi licha ya kuwa ni asilimia 30 ya idadi ya watu wa Chicago.

Watu wan eneo analoishi Mchungaji Hatch ni vigumu sana kupata bima ya fya na pia mara nyingi wanaishi wengi katika sehemu moja ikilinganishwa na jamii nyengine.

Raia weusi vijana wamekuwa wakiandika ujumbe kwenye mitandao ya jamii kwamba wananyanyaswa na walinzi madukani au hata kuagizwa kuondoka iwapo watapatikana wakitumia nguo kuziba pua na mdomo.

Short presentational grey line

'Hata nikipata maradhi, bado nitafanyakazi'

"Wateja ninaowahudumia, huwezi kujua wana maradhi gani."

Clarionta Jones, mwenye miaka 24 kutoka New Orleans, 24, anahofu ya kuambukizwa virusi vya corona lakini anahisi kwamba machaguo aliyo nayo ni machache. Anafanyakazi katika duka moja ambalo linaorodheshwa kuwa miongoni mwa ambayo ni muhimu sana na linaendelea kutoa huduma.

Coronavirus
Banner

"Mimi peke yangu ndo nimebaki mwenye kipato nyumbani kwetu, na licha ya kuwa wakati huu ambapo watu wanafutwa kazi na waajiri wao, wametuambia kwamba ni lazima tulipe kodi ya pango ya mwezi Aprili," Clarionta amesema.

"Ukweli wa Mungu, iwapo nitaumwa, nitakunywa tu dawa na niendelee kwenda kazini. Sitaki kukosa malipo yangu, nina watoto wawili. Yaani sina budi."

Clarionta anasema kwamba mkuu wake kazini amewaambia kuwa ni mwiko wao kuhudumia wateja wakiwa wamevalia barakoa na glavu. Hakuwa na uwezo wa kumuuliza zaidi kwa sababu anahofia kwamba atafutwa kazi.

Clarionta Jones

Chanzo cha picha, Submitted Photo

Katika nchi mbalimbali duniani, wafanyakazi wa sekta ambazo ni muhimu na mara nyingi mshahara wake huwa wa chini ndio wanaathirika zaidi na Covid-19. Nchini Marekani, 'mshahara wa chini' unamaanisha watu weusi ama makundi mengine ya raia ambao si wazungu.

Lakini Clarionta amesema jambo la kushangaza.

"Kwanza nilisikia kwamba watu weusi hawaambukizwi virusi vya corona. Ninachomaanisha ni kwamba China hakuna watu wengi weusi na hata hapo ulipoanza kwa kiasi kikubwa ulikuwa unaambukiza watu wa ngozi nyengine."

Hii haikuwa tu taarifa ya uwongo iliyosambaa New Orleans lakini pia hadi katika maeneo mengine duniani.

Katikati ya mwezi Machi, msanii wa nyimbo za kufokafoka Waka Flocka wa Atlanta, Marekani alikuwa kwenye kipindi kimoja cha redio na kusema: "Watu walio wachache (ikiwemo weusi) hawawezi kupata virusi vya corona. Mtaje mmoja aliyeambukizwa."

Wakati huo, baadhi ya wahudumu wa afya walihisi kwamba watu wangelifahamishwa zaidi kuhusu virusi vya corona mapema zaidi.

Short presentational grey line

'Ubaguzi uliokita mizizi ulaumiwe'

Kama kamishna wa afya katika mji ambao karibia asilimia 40 ya wakaazi wake ni weusi, taarifa ghushi kama hii ni kitu ambacho Dkt Jeanette Kowalik anakabiliana nacho kila siku katika utekelezaji wa kazi yake huko Milwaukee, Wisconsin.

Lakini wakati ambapo idara yake ilikuwa inaunda mikakati ya kukabiliana na kauli kama hizo, ugonjwa huo ukavamia mji wake.

"Wiki ya kwanza, mji ulikuwa na wagonjwa karibia 80, na asilimia 70% ya walioambukizwa walikuwa watu weusi," Dkt Kowalik amesema.

Anasema kile ambacho anadhani ni sababu kubwa ya kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19 kwa watu weusi.

Jeanette Kowalik

Chanzo cha picha, City of Milwaukee

"Raia weusi wa Marekani wana matatizo mengine ya kiafya yenye kuhusishwa na kifo (miongoni mwa walioambukizwa virusi vya corona); magonjwa ya moyo, kisukari, pumu, uzito kupita kiasi," amesema daktari Kowalik.

Mtaalamu huyo anaelezea pia namna ambavyo afya za watu weusi zilivyo mashakani, akirejelea tafiti za kitabibu ambazo zinaonesha kuwa kuwa na kipindi kirefu cha kuchochewa kwa homoni za msongo wa mawazo kama cortisol kunafanya miili ya Wamarekani weusi kuzeeka kabla ya wakati, na hayo ni moja ya vitu vinavyounganishwa na athari za watu hao kukabiliana na ubaguzi.

"Yote haya yanaweza kuunganishwa na ubaguzi uliokita mizizi wa kitaasis, kutoka kwenye sera na utekelezaji wake ambazo zimekuwa katika historia ya nchi hii kwa muda mrefu," amesema.

Presentational grey line

Kilichosababisha dhana potofu - kutoka BBC Monitoring

Uvumi wa kwamba watu wenye rangi nyeusi huenda wana kinga imara ya kukabiliana na Covid-19 umekuwa ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu mwishoni mwa Januari.

Awali, shtuma hizo zilikuwa zinasababishwa na ukosefu wa ripoti za virusi vya corona Afrika na simulizi ya kupona kwa mwanafunzi wa Cameroon nchini China aliyeambukizwa virusi hivyo.

Ujumbe kadhaa ulisambaa kwenye mtandao wa Facebook katikati ya Februari uliokuwa na madai ya kupotosha kwamba mtu mwenye umri wa miaka 21, amepona ugonjwa huo kwasababu ngozi yake ni nyeusi.

Lakini ukweli ni kwamba hakuna uthibitisho kwamba kupona kwake kulihusika kwa namna yoyote ile na rangi ya ngozi yake.

Aidha, madai hayo bandia yalichapishwa na tovuti nyingi za lugha ya Kiingereza na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii katika nchi kadhaa kama vile Nigeria, Kenya, Uganda na Zambia.

Suala la uimara wa kinga ya mwili pia limesambaa pakubwa katika jamii za raia wa Marekani wenye asili ya Afrika ambako hilo limekuwa likifanyiwa mzaha na kusambaa hata zaidi.

Presentational grey line