Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona: Tanzania yatangaza marufuku mpya ya usafiri wa anga kukabiliana na virusi
Mamlaka nchini Tanzania zimetangaza marufuku ya ndege za abiria kutua nchini humo.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na mamlaka ya usafiri wa anga nchini humo (TCAA) ndege za abiria pekee ndizo ambazo zitaruhusiwa kutua.
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt Hassan Abbas ameandika kupitia mtandao wake wa Twitter kuwa: "Hii ni hatua nyengine ya kupambana na ugonjwa wa Covid-19."
Taifa hilo la Afrika Mashariki mpaka sasa limesharipoti wagonjwa 32 wa virusi vya corona, vifo vitatu na wagonjwa watano kupona.
Maeneo ambayo ugonjwa huo umeripotiwa nchini Tanzania ni Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na Mwanza.
Marufuku ya usafiri wa anga inasemaje
Kwa mujibu wa tangazo la TCAA, kutokana na mlipuko wa Covid-19 kuanzia tarehe 11 Aprili, masharti yafuatayo yamewekwa: "Ndege zote za kimataifa za abiria ambazo zilikuwa na ratiba ya kutua na hata ambazo hazikuwa na ratiba zinapigwa marufuku kutua."
Kwa upande wa ndege za mizigo zitaendelea kuruhusiwa isipokuwa, "Rubani na wahudumu wa ndege hizo watatakiwa kukaa kwenye karantini katika maeneo yaliyotengwa na serikali kwa gharama zao binafsi," inaeleza tangazo hilo.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo Tanzania inakosolewa na baadhi ya wachambuzi na vyombo vya habari vya kimataifa.
Msimamo wa rais John Magufuli wa kuruhusu sehemu za ibada kuwa wazi pia unakosolewa vikali katika kipindi hiki ambacho mataifa mengi yametangaza marufuku ya mikusanyiko ikiwemo katika sehemu za ibada.
Juzi Ijumaa, rais Magufuli alisistiza msimamo wake wa kutokufunga nyumba za ibada na mipaka ya nchi hiyo alipokuwa kwenye ibada ya Ijumaa Kuu.
"Sisi tumezungukwa na nchi karibu nane, tuna nchi kama ya Burundi, Rwanda, DRC, Uganda... Tungefunga mipaka wale tungekuwa tumewaua. Maana yake hakuna mafuta yeyote ambayo yangefika kwao. Maana yake hata magari yasingeendeshwa...ambulensi zinazowabeba wagonjwa wala zisingewachukia," amesema Magufuli akiwa kwao Chato na kuongeza: "Nilisema uchumi lazima uendelee na ugonjwa Mungu ataumalizapamoja na sisi tuendelee kuchukua juhudi zetu za tahadhari.