Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona: Marekani yarekodi vifo vingi zaidi vya virusi vya corona kwa siku
Marekani imerekodi vifo vingi vya ugonjwa wa corona kwa siku huku watu 1,736 wakifariki siku ya Jumanne.
Idadi hiyo inaweka watu waliofariki kutokana na virusi hivyo nchini humo kufikia 12,722 kulingana na data za chuo kikuu cha Johns Hopkins.
Marekani ina wagonjwa 398,000 wa virusi hivyo waliothibitishwa , ikiwa ndio idadi kubwa zaidi duniani .
Visa vyote duniani vimepita watu milioni 1.4. Hatahivyo wakati wa mkutano na vyombo vya habari , rais Donald Trump alisema kwamba Marekani huenda inafikia kilele cha 'upinde'.
Wakati huohuo Mji wa Wuhan nchini China ambapo maambukizi yalianza umekamilisha amri yake ya kutengwa kwa wiki 11.
Takwimu mpya zilizotangazwa siku ya Jumanne zimepita rekodi ya awali iliokuwa na vifo 1,344 kwa siku nchini Marekani ambapo ilitokea tarehe 4 mwezi Aprili.
Idadi ya vifo inatarajiwa kupanda huku baadhi ya majimbo yakiwa bado hayajatoa takwimu zao za jumla.
Familia ya msanii wa Marekani John Prine imethibitisha kwamba msanii huyo alifariki kutokana na virusi hivyo vya corona.
Akiwa maarufu kwa nyimbo kama vile Angel from Montgomery na Sam Stone, Prine alifariki katika mji wa Nashville siku ya Jumanne akiwa na umri wa miaka 73.
Mkewe alikutwa na virusi vya ugonjwa huo na kupona lakini Prine alilazwa hospitalini mwezi uliopita akiwa na dalili za ugonjwa huo na kuwekwa katika mashine ya kumsaidia kupumua.
Baadhi ya wasanii akiwemo Bruce Springsteen na Margo Price wametuma risala za rambirambi.
Je New York imeathirika vipi?
Kiwango kikubwa cha vifo vilivyotangazwa vilitoka katika jimbo la New York. Likijulikana kuwa kitovu cha mlipuko huo, mji huo uliripoti vifo 731 siku ya Jumanne. Linakaribia kupiku taifa lote la Itali kwa idadi ya visa vyake vilivyothibitishwa.
Gavana Andrew Cuomo alisema kwamba Jimbo hilo lilikuwa linakaribia kufikia kilele cha mlipuko wake .
Visa vya wagonjwa katika chumba cha wagonjwa mahututi vimepungua huku wale waliolazwa hospitalini pia wakipungua.
Gavana huyo amewataka raia kusalia majumbani mwao na kuendelea kutokaribiana na watu wengine. ''Najua ni vigumu lakini itabidi tuendelee kufuata maagizo hayo'', alisema.
Kwengineko, Jimbo la Wisconsin liliendelea kufanya uchaguzi wake siku ya Jumanne, licha ya agizo la watu kusalia nyumbani huku mlipuko wa virusi vya corona ukiendelea kuathiri kila sekta duniani.
Je Trump alisema nini kuhusu shirika la Afya Duniani WHO?
Wakati wa mkutano na waandishi habari siku ya Jumanne, bwana Trump alisema kwamba huenda Marekani ikaripoti visa vichache zaidi ya ilivyotabiriwa.
Ilitabiriwa kwamba zaidi ya watu 240,000 nchini Marekani wangefariki kutokana na mlipuko huo , kulingana na jopokazi la rais huyo.
Pia alisema kwamba huenda Marekani inaelekea katika kilele cha upinde wa mlipuko huo.
Wakati wa mkutano huo, pia alilishambulia shirika la Afya Duniani WHO akisema lilitoa ushauri mbaya na kwamba liliaangazia sana China.
Pia alisema kwamba Marekani itaondoa fedha zilizotengewa WHO.