Virusi vya corona: Afrika sio uwanja wa majaribio ya chanjo ya corona - WHO

Chanzo cha picha, Reuters
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amelaani kauli alizoziita za "kibaguzi" kutoka kwa madaktari wawili wa Ufaransa ambao walitaka chanjo ya virusi vya corona kufanyiwa majaribio barani Afrika.
"Afrika sio na haitakuwa uwanja wa majaribio wa chanjo yoyote," amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Matamshi ya madaktari hao waliyoyatoa kwenye mjadala wa runinga yamezua ghadhabu, na wametuhumiwa kwa kuwachukulia Waafrika kama "nguruwe wa kufanyiwa majaribio ya maabara".
Mmoja wa madaktari hao ameomba radhi kwa kauli yake.
Alipoulizwa kuhusu matamshi ya madaktari hao kwenye mkutano na wanahabari juu ya hali ya virusi vya corona ulimwenguni, Dkt Tedros alionekana Dhahiri kuwa mtu mwenye hasira, na kukiita kitendo cha madaktari hao kama "mning'inio kutoka kwenye ulevi wa fikra za kikoloni".
"Ni fedheha, jambo la kushtusha kusikia katika Karne ya 21 kutoka kwa wanasayansi wakitoa kauli kama zile. Tunalaani hilo kwa nguvu zote, na tunawahakikishia kuwa hilo halitatokea," ameeleza Dkt Tedros.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kadri ya namba ya watu wenye virusi vya corona inavyopanda barani Afrika, baadhi ya serikali barani humo zinachukua hatua ngumu na kali za kujaribu kupunguza kasi ya maambukizi.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta hapo jana alipiga marufuku safari zote za kutoka na kuingia Nairobi pamoja na miji mingine mikubwa mitatu kwa kipindi cha wiki tatu.
Madaktari hao walisema nini?
Katika mjadala kwenye runinga ya ufaransa ya channel LCI, Dkt Camille Locht, mkuu wa utafiti kutoka shirika la utafiti wa afya la Inserm alikuwa akiongelea juu ya majaribio ya chanjo barani Ulaya na Australia.
Dkt Jean-Paul Mira, mkuu wa kitengo cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Cochin ya jijini Paris, kisha akasema: "Nichokoze kitu, siyo kwamba tunatakiwa kufanya utafiti huu Afrika, ambako hakuna barakoa, hakuna matibabu wala huduma ya nusu kaputi?
"Kama inavyofanyika kwengineo kwenye taffiti za ukimwi. Kwa kutumia machangudoa tunajaribu vitu kwa kuwa tunajua wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi na hawafanyi kitu kujilinda."
Dkt Locht akatikisa kicha kwa kuashiria kukubalina na pendekezo hilo, kisha akasema: "Upo sahihi. Tupo katika mchakato wa kufikiria utafiti sambamba bararani Afrika."
Dkt Mira awali aliuliza iwapo utafiti huo utaendelea kama ilivyopangwa kwa wahudumu wa afya Australia na Ulaya kwa kuwa wanavitendea kazi vinavyowawezesha kujikinga na maambukizi wakiwa kazini.

Kipindi hicho kilisababisha hasira kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo nyota wa zamani wa kandanda Didier Drogba, ambaye aliyaita matamshi hayo kuwa "yamejaa ubaguzi ". Akaongeza: "Msiwafanye waafrika kuwa binaadamu wa majaribio ya maabara! Ni jambo linalochefua".
Nyota mwengine wa zamani wa kandanda Samuel Eto'o aliwaita madaktari hao kuwa "wauaji".
Matamshi ya madaktari hao yanakuja wakati ambao tayari kuna khofu barani Afrika kuwa watu wa bara hilo watatumika kama majaribio kwa chanjo mpya ya virusi vya corona.
Vituo vya kutibu virusi vya corona katika nchi kadhaa Afrika vimeshambuliwa, tukio la hivi karibuni zaidi ni kuvunjwa na waandamanaji kituo kimoja kilichokuwa kinajengwa jijini Abijan, Ivory Coast.
Picha za video mtandaoni zinaonesha watu wakikiharibu kituo hicho kwa kutumia mikono yao huku wakimwaga chini vifaa vya ujenzi.













