Virusi vya corona: Je vipimo vya kugundua virusi vya corona vinafanya kazi vipi?

Chanzo cha picha, PA Media
Serikali ya Uingereza inataka kuimarisha upimaji wa virusi vya corona kwa hadi watu 100,000 kwa siku kufikia mwisho wa Aprili.
Pia imekuwa ikikosolewa kwa kuchukuwa muda mrefu kuongeza idadi ya wanaopimwa kwa siku.
Ni vipimo gani vya coronavirus vilivyopo?
Kwasasa vipimo vinavyofanyika Uingereza ni kuchunguza ikiwa mtu ameambikizwa Covid-19.
Vipimo hivyo vinafanywa kwa kutumia kifaa mfano wa kijiti kirefu ambacho kinaingizwa katika mfumo wa kupumua kupitia kwenye pua au mdomoni hadi kwenye koo na kuchota majimaji ya kwenye utando ambayo yanapelekwa kwenye maabara kuchunguzwa ikiwa pengine mtu ameambukizwa virusi hivi.
Kipimo kingine ambacho serikali inataka kutumia kubaini ikiwa mtu ameambukizwa virusi vya corona ni kupima kinga ya mwili.
Vipimo hivi vinafanywa kuchunguza ikiwa mtu tayari ameambukizwa virusi.
Vipimo hivi vinafanyakazi kwa kuchunguza kinga ya mwili, kwa kutumia tone la damu linalowekwa kwenye kifaa maalum mfano wake ni sawa na vile mtu anavyopimwa kuangaliwa kama ana ujauzito.

Lakini je vipimo hivi ni sahihi kiasi gani?
Vipimo vinavyofanywa hospitali huwa ni vya uhakika.
Hatahivyo, hii inamaanisha kwamba watafanikiwa kugundua kila kisa cha virusi vya corona.
Mgonjwa ambaye ndio anaanza tu kupata maambukizi haya au ambaye maambukizi yake bado yako chini matokeo yataonesha kuwa mtu hajaambukizwa.
Na pia iwapo kipimo kinachotumika ni kile cha kuchukua majimaji kwenye utando kupitia mfumo wa kupumua, huenda yakaonesha kwamba mtu hajaambukizwa ikiwa majimaji yaliyochukuliwa kwenye koo ni kidogo mno.
Hadi kufikia sasa, vipimo vya kinga ya mwili havijathibitisha kwamba ni vya kutegemewa.
Waziri wa Afya Uingereza, Matt Hancock, juma lililopita alisema kwamba vifaa vya kupimia 15 vinayotumia kinga ya mwili vilipimwa lakini hakuna ambacho kilitosheleza kuonesha matokeo ya uhakika.
Professor John Newton, ambaye anasimamia vipimo hivyo, ameliambia gazeti la The Times kwamba vifaa vya kupima corona vilivyochukuliwa kutoka China vilifanikiwa kugundua kinga mwili kwa wagonjwa ambao wamekuwa wakiuguwa sana kwasababu ya coronavirus lakini hawakuvijaribu vipimo hivyo kwa wagonjwa ambao hawajalemewa na ugonjwa huo.
Serikali ilinunua vipimo vinavyotumia kinga ya mwili milioni tatu na nusu ikiwa na matumaini kwamba itafanikiwa kutambua ni watu wangapi wameambukizwa virusi vya corona, lakini haitaki kuvitumia hadi itakapokuwa na uhakika kwamba vinafanyakazi inavyotakikana.
Lakini kwanini ni muhimu kupimwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuna sababu kuu mbili za kufanyiwa vipimo - kupima kila mmoja peke yake na kuchunguza ikiwa virusi hivyo vimesambaa hadi kufikia wapi.
Kupata taarifa hii kunaweza kusaidia wizara ya afya kupanga kwa ajili ya mahitaji mengine ikiwemo ya wagonjwa mahututi.
Kupima pia ni njia moja ya kujua hatua zitakazochukuliwa hasa zile za kutosongeleana. Kwa mfano, ikiwa kuna idadi kubwa ya watu walioambukizwa tayari, basi kusimamisha shughuli zote kabisa yaani lockdown itakuwa ni muhimu kuchukuliwa.
Na pia kutofanya vipimo vya ugonjwa huu kwa watu wengi zaidi kunamaanisha, idadi kubwa ya watu wanaweza kutengwa pasipo na sababu ya msingi ikiwemo wafanyakazi wa afya.
Je naweza kupimwa?
Hadi kufikia sasa vipimo hivi havijafanyika kwa kila mmoja.
Vipimo vingi vinafanywa kwa wagonjwa walio katika hali mahututi hospitalini.
Inamaanisha wengi ambao wanaonesha dalili hawawezi kubaini ikiwa wameambukizwa virusi vya corona.
Kwasasa, vipimo vinafanyiwa madaktari na wauguzi ambao wameonesha dalili au ambao wanaishi na mtu aliyeambukizwa. Kisha orodha hiyo inafuatiliwa na wale ambao ni wahudumu wengine wa afya.
Karibia wafanyakazi 6500 wa afya na familia zao wamefanyiwa vipimo vya corona kulingana na idara ya afya na
Kufikia Jumapili, jumla ya watu 195,524 nchini Uingreza walikuwa wamepimwa.
Lakini kwanini Uingereza haifanyi vipimo kwa wingi zaidi?
Uingereza haijafanikiwa kuwa na vifaa vya kuwezesha kupima watu wengi kwa wakati mmoja.
Waziri wa Afya Matt Hancock amesema: "Tuna maabara nyingi zaidi za kisayansi duniani lakini hatukuwa na uwezo.
Ujerumani kwa mfano, ilikuwa imeweka maabara 100 tayari na kusubiri tu wakati hali itakapokuwa mbaya zaidi."
Serikali pia inalenga kufanya vipimo 100, 000 kwa siku nchini Uingereza kufikia mwisho wa Aprili. Kufikia Aprili 5, vipimo vya kila siku vimefika karibia 12,000.
Wanaofanyakazi kwenye maabara wamedai kukumbana na changamoto za kupata majimaji ya kwenye utando kupitia njia ya mfumo wa kupumua na vifaa vya kupimia.
Kwanza, wizara ya afya Uingereza ilikuwa inatumia maabara zake nane pekee lakini kwasasa zimeongezwa hadi maabara 40 na kufikia jumla ya maabara 48.
Serikali inasema kwasasa inafanyia kazi suala la kuongeza maabara zaidi katika vyuo vikuu na taasisi za utafiti. Hizo zitatumika na wahudumu wa afya.
Pia imetangaza mipango ya kushirikiana na kampuni zingine kama vile Boots na Amazon, pamoja na kampuni kubwa za kuuza dawa ili kuimarisha uwezo wa kufanya vipimo nchini Uingereza.
Vipi kuhusu nchi zingine duniani?
Korea Kusini ambayo imefanikiwa kupima watu wengi zaidi kuliko Uingereza, ilichukua hatua za haraka na kuidhinisha manunuzi ya vifaa vya kupimia watu pamoja na kuagiza vifaa vya akiba.
Licha ya kuwa na idadi ndogo ya watu kuliko Uingereza, ina maabara mara mbili zaidi na idadi ya wanaopimwa ni mara mbili na nusu zaidi kwa wiki kuliko Uingereza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ujerumani imefanya majaribio zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na Uingereza.
Kufikia Machi 27, ilikuwa imepima watu 1,096 kati ya 100,000, ilihali hadi kufikia Aprili Mosi, Uingereza ilikuwa imepima watu 348 kati ya 100,000.
Hili linalinganishwa na watu 895 kati ya 100,000 nchini Italia, na watu 842 kwa 100,000 nchini Korea Kusini, watu 348 kati ya 100,000 nchini Marekani na 27 kati ya 100,000 nchini Japani.














