Coronavirus: Jinsi amri ya kutotoka nje inavyotekelezwa na mataifa tofauti duniani kuzuia virusi vya corona

Chanzo cha picha, Reuters
Nchi zote duniani zitachukua hatua ambazo hazijawahi kuchukuliwa kabla ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, kuanzia hatua kali kabisa, za wastani hadi zile za kawaida
Tunatupia jicho baadhi ya hatua ambazo si za kawaida zilizochukuliwa na mataifa mbalimbali kukabiliana na Covid-19.
1) Panama
Nchi ya Amerika ya Kati, ambayo imethibtisha karibia visa 1,000 vya ugonjwa wa Corona, imetangaza sheria kali za karantini ambayo ni kutenganisha watu kwa jinsia zao katika juhudi za kudhibiti usambaaji wa coronavirus.

Kuanzia Jumatano, wanaume na wanawake wataruhusiwa kutoka nje kwa saa mbili pekee kwa nyakati na siku tofauti.
Hakuna atakayeruhusiwa kutoka nje siku ya Jumapili.
"Karantini kama hii bila shaka si kwa ajili nyengine yoyote zaidi ya kulinda maisha yako," waziri wa usalama Juan Pino amesema katika mkutano na wanahabari.
2) Colombia
Katika baadhi ya miji Colombia, watu wanaruhusiwa kwenda nje kwa kuzingatia nambari ya mwisho ya kitambulisho cha taifa.
Kwa mfano, watu wa Barrancabermeja ambao nambari yao ya mwisho ya kitambulisho inaishia na 0, 7 ama 4 wanaruhusiwa kutoka nje Jumatatu, huku wale ambao nambari yao ya kitambulisho inaishia na 1, 8 au 5 wakiruhusiwa kutoka nje siku ya Jumanne.
Nchi jirani ya Bolivia ina sheria kama hizo.
3) Serbia
Wakati fulani, serikali ya Serbia ilianzisha "saa ya kutembea na mbwa" kuanzia 20:00 hadi 21:00 kwa wale walio maeneo ambayo hawaruhusiwi kutoka nje.
Lakini kwasasa hilo pia limeondolewa, na kusababaisha wamiliki wa mbwa kuanza kupinga hatua hiyo kwasababu mbwa wanapiga kelele kwa muda mrefu.
Daktari mmoja wa wanyama amesema kuondoa ruhusa ya wanyama kutembea jioni kunaweza kufanya wanyama hao kuwa na tatizo hasa la njia ya mkojo na kuharibu mazingira ya watu majumbani.
4) Belarus

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amekuwa akishangaza wengi kuhusu namna anavyoshughulikia mlipuko wa coronavirus.
Alichukulia mzaha pendekezo la kwamba nchi hiyo ijaribu kutosambaza virusi vya Corona kwasababu kulingana na yeye hakuna vile virusi hivyo vinaweza kusambaa hadi nchini humo.
Akizungumza na mwanahabari mmoja wakati wa mechi ya mchezo wa magongo, alidai kwamba mikusanyiko katika sehemu kama hiyo haina tatizo kwasababu baridi ndani ya uwanja itasaidia kuzuia virusi hivyo visisambae.
Bado haijathibitishwa kama pengine hiyo ndio sababu virusi vya corona haviwezi kuonekana kwa macho ya kawaida tu.
Tofauti na maeneo mengi ya Ulaya, Belarus haijaweka masharti yoyote katika michezo.
"Hapa hakuna virusi, ," Bwana Lukashenko amesema. "Nina uhakika hujawahi kuviona hapa, au sio? hata mimi pia sijaviona! Hili ni jokofu. Hususan michezo kama ya barafu, hili jokofu hapa, hakuna tiba nzuri kama hii!''
Pia inasemekana kwamba amekuwa akinywa kiywaji cha vodka na kufunga safari mara kadhaa hadi sauna kama njia za kuzuia virusi hivi - jambo ambalo ni kinyume kabisa na ushauri wa kitaalam.
5) Sweden
Tofauti na majirani zao, Uswidi pia nayo haijakuwa na sheria kali linapokuja suala la hatua za kusimamisha shughuli zote, licha ya kwamba visa 4,500 vimethibitshwa. Serikali inatumai kwamba raia watachukua jukumu kuchukua hatua stahiki na kuamini kwamba wanaweza kufanya maamuzi yanayostahili.
Mikusanyiko ya zaidi ya watu 50 ilipigwa marufuku Jumapili lakini shule za watoto chini ya miaka 16 bado zinaendelea kama kawaida.
Baa na migahawa bado inaendesha shughuli zao na idadi kubwa ya watu bado wanatangamana kama kawaida.
Mkakati huo umeibua hisia tofauti nyumbani na nje ya nchi lakini wakati ujao itajulikana ikiwa mpango wa Uswidi umefanikiwa au la.
6) Malaysia
Ushauri uliotolewa Malaysia umefanikiwa kutogawanya raia.
Serikali ililazimika kuomba msamaha baada ya wizara ya masuala ya wanawake kuandika ujumbe mtandaoni wakitoa wito kwa wanawake kwamba wavae nguo zao, wajipambe na kukwepa kukumbatia waume zao wakati ambao nchi hiyo inapitia kipindi cha amri ya kusalia ndani kwa muda fulani.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii walikuwa wepesi sana wa kukosoa ujumbe huo ambao baadae uliondolewa.
7) Turkmenistan
Wakati huohuo, Turkmenistan, inasemekana imechukua mkondo tofauti kabisa wa kukabliana na janga hili la virusi vya Corona...na kupiga marufuku utumiaji wa jina "coronavirus".
Kulingana na tovuti ya Gazeti la independent news, neno corona limepigwa marufuku na likaondolewa katika kijitabu cha taarifa za afya. Wanahabari wa Radio Azatlyk wanasema kwamba wale wanaozungumza kuhusu virusi hivyo au wanaovaa barakoa hadharani huenda wakakamatwa na polisi.
Mamlaka inasema kwamba hakuna kisa hata kimoja cha corona kilichorekodiwa huko Turkmenistan, inayopakana na moja ya mataifa yaliovamiwa vibaya na ugonjwa huo, taifa la Iran.
8) Austria
Shirika la Afya duniani limesema watu ambao hawana tatizo lolote hawastahili kuvaa barakoa labda wawe wanamuuguza mtu ambaye ameugua ugonjwa huo, Austria imelazimisha utumiaji wa barakoa kwenye maduka ya jumla.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sheria hizo mpya zilitangazwa na chansela Sebastian Kurz na zikaanza kutekelezwa Jumatano, huku mamilioni ya barakoa zikianza kutolewa.
Ingawa barakoa ni jambo la kawaida katika bara la Asia, Austria ni ya nne miongoni mwa nchi za ulaya kuhimiza utumiaji wa barakoa katika maeneo ya umma - wakifuata nyayo za Jamuhuri ya Czech, Slovakia na Bosnia and Herzegovina.













