Coronavirus: Je ukipoteza uwezo wa kunusa harufu na ladha ya chakula utakuwa umepata virusi vya corona?

Nose and smell

Chanzo cha picha, Getty Images

Kupoteza hisia ya kunusa na kuonja ladha ya chakula kunaweza kuwa dalili ya coronavirus, kulingana na watafiti nchini Uingereza.

Timu katika Chuo cha King's College London imeangazia matokeo ya watu zaidi ya 400,000 walioripoti kile walichoshuku ni virusi vya corona katika programu moja.

Lakini kupoteza hisia ya kunusa na hamu ya kula pia ni ishara ya kupata maradhi mengine ya kuambukiza kama vile homa.

Na wataalamu wanasema homa na kukohoa bado zinasalia kuwa dalili za msingi za kufuatiliwa kwa karibu na hatua kuchukuliwa.

Ikiwa wewe ama mtu mwengine unayeishi naye amepata kikohozi kinachoendelea, au kuwa na kiwango cha joto la juu, ushauri ni kusalia nyumbani ili kuepuka kusambaza virusi vya corona kwa wengine.

Maelezo zaidi
Banner

Utafiti huu ulibaini nini?

Watafiti kutoka King's College walitaka kukusanya taarifa kuhusu dalili ambazo huenda zinaashiria kupata virusi vya corona ili kusaidia wataalamu kupata uelewa mzuri zaidi na kukabiliana na virusi hivyo.

  • Asilimia 53 ya waliohojiwa walikiri kuwa na uchovu mwingi sana
  • Asilimia 29 walikuwa na kikohozi kinachoendelea
  • Asilimia 28 walikuwa na matatizo ya kupumua
  • Asilimia 18 walipoteza hisia zao za kunusa na kuonja ladha ya chakula
  • Asilimia 10.5 walipata na homa

Kati ya watu 400,000, waliohojiwa, 1,702 walisema wamepimwa ikiwa wanavirusi vya Covid-19, huku watu 579 wakipatikana kuwa na virusi ilihali wengine 1,123 ikabainika kwamba wako sawa.

Miongoni mwa waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya coronavirus asilimia 59 walipoteza uwezo wa kunusa na kuonja ladha ya chakula.

Je kupoteza hisia ya kunusa na kuonja ladha ya chakula vinastahili kuongezwa kama dalili za corona?

Unachohitajika kufanya ili kuzia mambukizi ya virusi hivi

Wataalamu wanasema hadi kufikia sasa bado hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha hilo.

Wizara ya afya Uingereza na Shirika la Afya duniani bado hawajaongeza hoja hizi miongoni mwa orodha ya dalili za corona.

Bodi inayosimamia wataalamu wa tiba ya masikio, pua na koo wanasema, sio jambo la kushangaza kuona baadhi ya wagonjwa wa Corona wakiripoti dalili hizi lakini haimaanishi kuwa zinaashiria Covid-19.

Watafiti wa King's College wanasema kupoteza hamu ya kuonja chakula na hisia ya kunusu zinaweza kuwa dalili za ziada za kufuatilia kwa karibu pengine siyo hizo tuu lakini kwa pamoja na dalili zingine kama vile kukohoa na homa.

Mkuu wa timu ya utafiti Profesa Tim Spector amesema: "Zikijumuishwa na dalili zingine, ukosefu wa hisia ya kunusa na kuonja chakula inaonekana kuwa mara tatu zaidi kwa wagonjwa waliopata Covid-19 kulingana na data yetu, na hivyo basi wanastahili kujitenga kwa siku saba kupunguza usambaaji wa virusi vya Corona."