Coronavirus: Tanzania yathibitisha mgonjwa wa kwanza wa corona

Chanzo cha picha, Egan Salla- BBC
Tanzania imethibitisha kisa kimoja cha virusi vya corona.
Mnamo tarehe Machi,15, msafiri huyo aliiingia Tanzania majira ya saa kumi jioni.
Mgonjwa aliyetangazwa ni mwanamke wa miaka 46 raia wa Tanzania, ambaye aliwasili kutoka Ubelgiji kwa ndege ya shirika la Rwanda.
Msafiri huyo aliondoka nchini tarehe 3,Machi 2020 ambapo kati ya tarehe 5-13 Machi alitembelea nchi za Sweden na Denmark na kurudi tena Ubelgiji.
Msafiri huyo alipita uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Waziri Ummy Mwalimu amesema msafiri huyo alipofika KIA alifanyiwa ukaguzi na maafisa wa afya na kuonekana kutokuwa na homa.
Baadae alianza kujisikia vibaya akiwa hotelini na kwenda hospitali ya mkoa ya rufaa ya Mount Meru Arusha ambapo sampuli ilichukuliwa na kupelekwa maabara ya taifa ya afya ya jamii iliyoko Dar es salaam kwa ajili ya uchunguzi.
"Vipimo vya maabara vimethibitisha kuwa mtu huyo ana maambukizi ya ugonjwa wa corona, covid -19, Mgonjwa anaendelea vizuri na matibabu."
Waziri Ummy ameongeza kusema," Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba ugonjwa huu unathibitiwa ili usisambae nchini.
Aidha serikali inashirikiana na shirika la afya duniani-WHO na wadau katika kuendelea kutekeleza mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huu".
Raia wametakiwa kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu kadri wanavyopokea taarifa na elimu za mara kwa mara kwa njia mbalimbali.
Unaweza kutazama
Tamko la serikali ya Tanzania
Kwa kuzingatia kanuni ya 46 ya sheria ya afya ya jamii ninaelekeza mambo yafuatayo:
- Kwanza watanzania wasiokuwa na safari za lazima wanashauriwa kwa sasa kusitisha safari zao kwenye nchi zenye maambukizi
- Taasisi zote zikiwemo shule, hoteli, maduka ya biashara, nyumba za kulala wageni, makanisa, misikiti, ofisi za umma na binafsi, vituo vya kutolea huduma za afya, taasisi za fedha, vyombo vya usafiri pamoja na maeneo ya mikusanyiko ya watu kama vile masoko, viwanja vya michezo na vituo vya abiria kuweka vifaa vya kunawia mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni au maji yenye dawa kwa ajili ya kuhakikisha usafi wa mikono.
- Kuweka maji yenye dawa ya chroline katika mageti ya kuingia katika hifadhi zote kwa ajili ya kusafisha mikono ya watalii na waongoza wageni.
- Kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono
- Kukumbatiana , kubusu, kuepuka kushika pua, mdomo na macho.
- Hospitali zote nchini za serikali na zisizo za serikali kuweka zuio la idadi ya watu ambao wanakwenda kuwaona ndugu zao. Kwa maelekezo ya waziri ni kwamba wageni wa kumuona mgonjwa wasizidi wawili kwa siku kwa kila mgonjwa mmoja.
- Wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa vituo vya afya iwapo watamuona na mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Covid- 19.


Maoni ya watanzania katika mitandao ya kijamii
Hali hii imezua taharuki nchini humo kwa baadhi ya wananchi, huku wengine wakijilinganisha na hali hii wanavyoiona katika mataifa ya ulaya kama Italia.
Msaanii wa vichekesho wa Tanzania, Idris Sultan ameandika kwenye kurasa yake ya twitter na kuzua mjadala, watu wakiambiwa wakae nyumbani bila ya kufanya kazi wataweza kujikimu?
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Katika hatua nyingine, serikali ya Somalia imetangaza kuwa na kisa cha kwanza cha virusi vya corona.















