Coronavirus: WHO yatangaza virusi vya corona kuwa janga la kimataifa

Shirika la Afya duniani limeutangaza mlipuko wa virusi vya corona kuwa ni janga la kimataifa, huku mlipuko huo ukiendelea kusambaa katika mataifa mbalimbali duniani.

Mkuu Shirika la Afya Duninai (WHO), Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuwa idadi ya visa nje ya Uchina vimeongezeka mara 13 kwa kipindi cha majuma mawili yaliyopita.

Amesema kuwa "anahofu kubwa " kutokana na "viwango vya maambukizi " ya virusi.

Janga ni ugonjwa ambao unasambaa katika nchi nyingi kote duniani kwa wakati mmoja.

Hatahivyo Dkt Tedros amesema kuwa kuuita ugonjwa janga haimaanishi kuwa WHO inabadilisha ushauri wake juu ya kile mataifa yanapaswa kufanya.

Amezitolea wito serikali kubadili jinsi zinavyoushughulikiwa mlipuko kwa kuchukua "hatua za dharura ".

"Nchi kadhaa zimeonyesha kuwa virusi hivi vinaweza kudhibitiwa ,"amesema.

"Changamoto kwa nchi nyingi ambazo hazuishughulikii idadi kubwa au maambukizi ya jamii sio kwamba haziwezi kufanya hilo - ni ikiwa wataweza."

Ilibidi Serikali "zipate uwiano unaofaa kati ya kulinda afya, kupunguza maambukizi na kulinda haki ya maisha ya binadamu ".

"Tupo katika hili pamoja kufanya mambo yanayofaa kwa utulivu na ulinzi wa raia wa dunia. Inawezekana," amesema.

Awali Ujerumani ilisema kuwa hadi 70% ya watu nchini humo - karibu watu milioni 58 - huenda wakaambukizwa virusi vya corona .

Kansela wa Ujerumani, Bi. Angela Merkel alitoa taarifa kwa wanahabari siku ya Jumatano akiwa na waziri wa afya, Jens Spahn.

Alisema kuwa kwa sababu hakuna tiba iliyopatikana kufikia sasa,mikakati zaidi inatakiwa kuelekezwa katika udhibiti wa kusambaaa kwa virusi hivyo "Cha msingi ni juhudi za kukabiliana nao haraka iwezekanavyo,"alifafanua.

Baadhi ya wataalamu wa virusi nchini Ujerumani wanatofautiana juu ya idadi iliyotolewa na Bi Merkel. Mshauri wa zamani wa serikali ya Shirikisho wa udhibiti wa magonjwa , Prof Alexander Kekulé, ameviambia vyombo vya habari vya Ujerumani kuwa aliona kisa kibaya zaidi ambapo watu 40,000 walipata maambukizi.

Nchini Italia, ambako zaidi ya visa vya maambukizi 10,000 vimethibitishwa, waziri mkuu Giuseppe Conte ametangaza kufungwa kwa shule, maeneo ya mazoezi ya mwili,majumba ya burudani, majumba ya makumbusho ya kihistoria na maeneo mengine nchini humo.

Nini kinachofanyika kwingine duniani?

  • Gavana wa New York ametangaza kuwa wanajeshi watapelekwa katika mji wa kaskazini wa New Rochelle, katika juhudi za kudhibiti mlipuko wa virusi huku visa vya maambikizi nchini Marekani vikipita 1,000 siku ya Jumatano.
  • Athari kubwa imeonekana nchini China. Lakini siku ya Jumapili iliripoti idadi ya chini zaidi ya maambukizI mapya katika siku moja tangu Januari - ishara kwamba kuenea kwa virusi kunapungua.
  • Iran, moja ya maeneo yenye maambukizi mabaya zaidi nje ya China, sasa imethibitisha maambukizi 6,566 na vifo 194.
  • Ufaransa, virusi vinaenea miongoni mwa wabunge. Wabunge wawili walikutwa na maambukizi, maafisa walieleza siku ya Jumapili.
  • Kwa jumla manaibu wanne wameambukizwa. Pia Jumapili Ufaransa iliripoti visa 1,126, ongezeko la 19% kwa siku na idadi kubwa ya maambukizi barani Ulaya baada ya Italia.
  • Serikali ya Ufaransa imepiga marufuku mikusanyiko ya watu zaidi ya 1,000.
  • Nchini Marekani, zaidi ya watu 470 wamekutwa na maambukizi ya Covid-19 na mpaka sasa waliopoteza maisha ni watu 21.
  • Miongoni mwa nchi zilizoripoti ongezeko la maambukizi ni Ujerumani 939, Uhispani 589, Uingereza 273 na Uholanzo 265.
  • Albania, Bulgaria, Colombia, Costa Rica, visiwa vya Maldives, Malta, na Paraguay zimeripoti visa vya kwanza vya maambukizi ya virusi hivyo.