Msikiti uliohusishwa na itikadi kali za Kiislam sasa ni kituo cha amani

Msikiti wa Masjid Musa uliopokatika mji wa pwani ya Kenya wa Mombasa, ambao wakati mmoja ulihusishwa na itikadi kali za kiislamu, umekua kituo cha maridhiano na amani.

Mwaka 2014, polisi waliuvamia msikiti huo, wakisema ulikua ukitoa mafunzo kwa vijana ili wajiunge na kikundi cha wanamgambo wa kiislamu chenye makao yake nchini Somalia cha al-Shabab.

Walikamata gurunedi, video za propaganda, na bendera nyeusi zilizochorwa alama zinazotumiwa na al-Shabab.

Baada ya zaidi ya watu 100, wengi wao wakiwa ni vijana kukamatwa, msikiti huo ulifungwa.

Wazee wa jamii na viongozi wa mkoa huo walikutana na kufanya mabadiliko ya uongozi wa msikiti, wakawafukuza Maimam wenye itikadi kali na kuwaleta wapya wenye misimamo ya kadri.

Baada ya wiki mbili, serikali ilirejesha tena msikiti huo baada ya kuridhishwa na mageuzi , ambayo yalijumuisha mchakato wa kuwarejesha katika maisha ya kawaida viojana waliokua wamepewa mafunzo ya itikadi kali.

Shabi Islam, kiongozi mpya wa msikiti huo, ameiambia BBC kuwa hivi ndivyo walivyoweza kufanikiwa kufanya mageuzi: ''Hatukutumia bunduki. Tuliomba na kutumia maneno ya huruma. Viongozi wa msikiti na wanavijiji walizungumza na jamii nzima kuwashawishi vijana kubadili mienendo yao'' alisema na kuongeza kuwa sasa hakuna hata mmoja anayeweza kusema walirudi kwa njia ya mtutu wa bunduki.

Salim Karama, ambaye anasema alipewa mafunzo ya kujiunga na al-Shabab na kujiunga na maandamano ya ghasia wakati msikiti ulipofungwa, sasa amerejea maisha ya kawaida.

Hata hivyo anasema bila kazi watu kama yeye wataendelea kuwa watu wa kushawishika:

''Tatizo sugu ni…ukosefu wa ajira nakukaa tu bila kufikiria mambo ya maana. Kama mtu ana kazi ataondoka nyumbani mapema, ataenda kufanya kazi na kurudi nyumbani jioni. Serikali inapaswa kuangalia maisha yetu. Juhudi nyingi zinawekwa katika kurekebisha makosa bila kupandikiza mambo mazuri ."

Bado kuna baadhi ya maswali ambayo bado hayajapata majibu juu ya msako wa polisi.

Fundi wa nguo Saddah Suleiman anasema kuwa mume wake alikua ni miongoni mwa watu ambao walikamatwa na ambao hawajaonekana wala kusikika tangu wakati huo.

Uchunguzi wa mahakama ulisema kuwa huenda polisi walimuua. Lakini Bi Suleiman anataka jibu kamili: Bado sijaridhika kabisa. Serikali inapaswa kutuambia alipo kwasababu niwenyewe waliomchukua . Tuliwaona wakimchukua. Kwa hiyo wanahitaji walau kutuambiua yuko wapi. Hatujawahi kuambiwa hilo."

Polisi waliueleza uchunguzi kuwa aliruka kutoka kwenye lori na kukimbia mbali wakati alipokua akipelekwa kwenye kituo cha polisi masjid musa.

Licha ya hayo , miaka sita baadae, watu hawaogopi tena kutembea au kuishi karibu na msikiti wa Masjid Musa na wapangaji wanarejea tena kuishi katika maeneo ya msikiti