Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bernard Membe: ''...Tulieni! Nitapata muda wa kuongea na wote muda si mrefu!''
Chama tawala nchini Tanzania CCM kimemfukuza uanachama aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Bernard Membe.
Membe alikuwa akikabiliwa na tuhuma za maadili pamoja na viongozi wengine waandamizi wengine wawili makatibu wakuu wa zamani Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, ambao wao hawajafukuzwa.
Makamba amesamehewa, huku Kinana akionywa kwa karipio.
Akisoma taarifa ya maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM hii leo, Katibu Mwenezi wa CCM Humphrey Polepole amedai kuwa mwenendo wa Membe umekuwa si wa kuridhisha toka mwaka 2014.
"Kamati Kuu imeazimia kwa kauli moja kwamba Bernard Membe afukuzwe uanachama wa CCM. Uamuzi huu umekuja baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha," ameeleza Polepole.
Kwa mujibu wa Polepole, uongozi wa chama hicho umeazimia kumsamehe Mzee Makamba kwa kuwa: "...amekuwa mtu muungwana na mnyenyekevu kwa mamlaka ya chama. Na ameomba asamehewe kwa barua."
"Mzee Kinana anapewa adhabu ya karipio kwa mujibu wa kanuni... Atakuwa katika hali ya matazamio kwa mda wa miezi 18 ili kumsaidia katika jitihada za kujirekebisha.
Hatakuwa na haki ya kugombea nafasi ya uongozi kwenye chama, japo ataruhusiwa kupiga kura kama atakuwa na dhamana hiyo," ameeleza Polepole.
'Membeatoa neno'
Kwa kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter unaoaminika kuwa ni wa kiongozi huyo, Membe ameahidi kuliongelea jambo hilo hivi karibuni.
"Watanzania wenzangu nimepata habari ya kufukuzwa kwangu kutoka kwenye Chama changu cha CCM. Simu zinamiminika hadi nashindwa kuzijibu. Tulieni! Nitapata muda wa kuongea na wote muda si mrefu!"
"Kukidhalilisha chama mbele ya Umma"
Membe, Makamba na Kinana walipelekwa katika kamati ya maadili ya CCM mwezi Disemba mwaka jana, na taarifa ya chama hicho ilidai kuwa viongozi hao pamoja na makada wengine watatu ambao walisamehewa walikidhalilisha chama mbele ya Umma.
Makada ambao walitangazwa kusamehewa ni January Makamba, Nape Nnauye na Wlliam Ngeleja ambao wote walimuomba radhi mwenyekiti wa CCM na rais wa Tanzania John Pombe Magufuli.
Baadhi ya mazungumzo ya simu ya wanachama hao sita wa CCM yalivujishwa kwenye mitandao nchini Tanzania wakizungumzia masuala mbalimbali kukihusu chama na mwenyekiti wake.
Sehemu ya mazungumzo yaliyovuja ya Mzee Yusuf Makamba na Kinana ni pamoja na kuandaa taarifa ya malalamiko dhidi ya 'mawanaharakati' Cyprian Musiba ambaye wanamtuhumu kwa 'kuwadhalilisha' bila kuchukuliwa hatua yoyote na kuhoji analindwa na nani.
Membe na tuhuma za kutaka kumhujumu Magufuli
Kwa upande wa Membe, licha ya kusikika kwenye mazungumzo hayo yalivuja, amekuwa pia akituhumiwa na baadhi ya wanchama wa chama hicho kuwa najipanga 'kumhujumu' Magufuli katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Membe amekuwa akihusishwa kwa muda mrefu na mipango ya kutaka kugombea tiketi ya urais kupitia CCM mwaka huu, hatua ambayo baadhi wanaitafsiri kama usaliti.
Japo katiba ya CCM inaruhusu hilo, imekuwa ni ada ya chama kumuachia rais aliye madarakani kupita bila kupingwa kwa awamu ya pili ya urais.
Baadhi ya watu tayari wanatafsiri kufukuzwa kwa Membe ni kutokana na kuhusishwa huko na mipango ya Urais.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe kwa kupitia mtandao wake wa Twitter amepeperusha maoni yake na kuhusisha urais na kufukuzwa uanachama kwa Membe.
"Chama kikongwe kimetekwa na mtu Mmoja. Mwanachama kaonesha nia tu ya kugombea Urais ndani ya Chama kafukuzwa uanachama. Bernard Kamilius Membe wamekutua mzigo hawa. Simamia unachokiamini na historia itakuweka unapostahili- kwamba ulikataa UDIKTETA ndani na nje ya chama chako," ameandika Zitto.