Polisi wa usalama barabarani aachwa mdomo wazi baada ya mwizi kumuibia fedha za rushwa Kenya

    • Author, Wanyama wa Chebusiri
    • Nafasi, BBC Africa, Nairobi

Katika kisa ambacho kimezua gumzo kwenye vyombo vya habari hasa mitandao ya kijamii nchini Kenya, mwanaume mmoja mwenye ujasiri amewaibia polisi donge walilokuwa wamekusanya kama rushwa kutoka kwa madreva wa magari.

Kwa mujibu wa habari zilizochapishwa kwenye mtandao wa gazeti la Nation, mwizi huyo alizuka gahfla kutoka msituni, akanyakua kifurushi kilichokuwa na pesa kando mwa barabara na kisha kuchana mbuga kwa kasi!

Kisa hicho kisicho cha kawaida kilitokea siku ya Jumatano majira ya saa saba kwenye barabara kuu ya Embu kuelekea Nairobi, katika mkoa wa kati mwa Kenya.

Mbio za polisi hazikufua dafu

Mwendesha gari mmoja aliyeshuhudia kisa hicho alisema polisi wa trafiki mwanaume alijaribu kumfuata mwizi huyo bila mafanikio.

Kwa mujibu wa dreva huyo, mwizi huyo alikuwa anakimbia kwa kasi ambayo ilimwacha polisi akihema baada ya kujaribu kumfuata ili aokoe hela.

Polisi huyo na mwenzake wa kike walibaki vinywa wazi huku donge lao la siku likitoweka wakitazama tu!

Wengi mitandaoni wanawakejeli polisi kwa kuwapendekeza kwamba yafaa wabuni mbinu mpya ya kuhifadhi pesa wanazopokea kama rushwa wakiwa kazini.

Ufisadi kwenye barabara za Kenya

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kupambana na ufisadi- Transparency International, ufisadi kwenye barabara za Kenya umekithiri licha ya juhudi zinazofanywa kutokomeza tabia hiyo mbaya.

Utafiti wa Transparency International unaonesha kwamba si polisi tu wa kulaumiwa bali hata wenye magari wanachangia pakubwa katika kuendeleza ufisadi barabarani nchini Kenya.

Watu wenye magari hutoa hongo kwa polisi ili kukwepa mkono wa sheria kutokana na makosa kama vile kuendesha gari zaidi ya kasi iliowekwa, gari kukosa vidhibiti mwendo, magari ya abiria kubeba watu wengi kuliko inavyotarajiwa miongoni mwa makosa mengine ya barabarani.

Juhudi za kukomesha rushwa barabarani

Wakati alipochukua hatamu ya uongozi mkuu wa polisi nchini Kenya, Hillary Mutyambai alitangaza vita dhidi ya ufisadi barabarani.

Alitangaza kuanzishwa kwa kitengo maalum cha polisi kitakachoshirikiana na vitengo vingine vya kupambana na rushwa, kutokomeza ulaji wa rushwa miongoni mwa polisi wa usalama barabarani.

Katika siku za mwanzo za tangazo hilo la mkuu wa polisi, Kenya ilishuhudia visa kadhaa ambapo polisi walinaswa wakipokea hongo barabarani.

Pia, kipindi hicho kifupi kilishuhudiwa kuondolewa kwa vizuizi vyote vya polisi wa barabarani, hatua ambayo ilionekana kushabikiwa na wengi.

Hatahivyo, vizuizi hivyo vilirejea badaye na baadhi ya wachunguzi wa mambo wanasema hii imechangia sana rushwa barabarani kupamba moto.

Ajali barabarani

Kwa mujibu wa takwimu za idara ya kitaifa ya kushughulikia usalama barabarani - NTSA, zaidi ya watu 3,500 walifariki kutokana na ajali barabarani nchini Kenya mwaka jana.

NTSA inasema ongezeko la ajali linachangiwa na kutozingatiwa kwa sheria na kanuni za barabarani.

Ufisadi pia ni kigezo kikubwa ambacho kimechochea ongezeko la ajali za barabarani nchini Kenya.