Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuwa ''kiongozi mkuu'' na kulipwa mabilioni ya pesa
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza atapewa hadhi ya ''Kiongozi Mkuu'' wa Burundi atakapoondoka madarakani.
Bunge la Burundi limepigia kura muswada wa sheria wa kumpatia Bwana Nkurunziza cheo cha "Kiongozi Mkuu" na kumpatia mabilioni ya faranga za Burundi ($530,000) wakati atakapoondoka madarakani.
Burundi inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwezi Mei ambapo Bwana Nkurunziza aliahidi kuwa hatagombea tena muhula mwingine wa urais.
Muswada huo wa sheria pia utamuwezesha kulipwa mshahara katika kipindi chote cha maisha yake, kupata marupurupu yote anayopewa makamu wa rais aliyeko mamlakani na atapewa nyumba ya kifahar, anayopewa kila rais wa Burundi aliyechaguliwa kidemokrasia.
Ni rais Melchior Ndadaye, aliyeuawa mwaka 1993, na Pierre Nkurunziza wenye vigezo vya kupewa marupurupu hayo.
"Jana wabunge walifanya mjadala juu ya kiwango atakachopewa rais anayeondoka madarakani, huku baadhi apewe milioni 500, huku wengine wakisema apewe franga bilioni moja na wengine wakisema apewe franga bilioni mbili.
"Baadae wakakubaliana apewe faranga bilioni moja na marupurupu mengine'' - mwandishi wa habari ambaye alikua bungeni ameiambia BBC.
Wabunge pia walipendekeza Bwana Nkurunziza anapaswa kupewa cheo cha "Kiongozi Mkuu" na "Bingwa wa Uzalendo".
Pendekezo hili lilipitishwa na kikao cha baraza la mawaziri leo katika jimbo la kisiasa la Gitega nchini Burundi, kwa mujibu wa ujumbe wa Twitter wa msemaji wa rais wa Burundi.
Warundi walijibu kwa hisia tofauti kuhusu muswada huo kwenye mitandao ya kijamii juu ya marupurupu yatakayotolewa kwa Bwana Nkurunziza; huku baadhi wakisema marupurupu ni mengi sana kwa nchi kama Burundi ambayo ni maskini duniani, huku wengine wakisema kiasi hicho kinafaa kwa mtu anayelitumikia taifa mwenye majukumu ya hali ya juu.