Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Liberia yarejesha shehena za takataka hatari za plastiki zilikotoka nchini Ugiriki
Mamlaka ya Liberia imesema kwamba inarejesha shehena nne nchini Ugiriki zilizojaa tani za mifuko ya plastiki ambayo ni hatari kwa mazingira.
Mifuko hiyo ilikuwa imeingizwa nchini humo kimagendo "kwa kisingizio kwamba inaweza kuchakatwa upya".
Maafisa wa kupambana na bidhaa zinazoingizwa kimagendo nchini humo, waliibua malalamishi yao katika bandari ya Monrovia pale mzigo ulipowasili ukiwa unanuka "uvundo", na kutoa harafu mbaya, amesema mkuu wa Shirika la Kulinda Mazingira, Nathaniel Blama,
Aidha uchunguzi umeanzishwa mara moja kuhusu namna mzigo huo ulivyoagizwa.
Baada ya kontena hizo kukaguliwa, shirika hilo limesema kuwa aina ya mifuko ya plastiki iliyoletwa, imepigwa marufuku kuchakatwa na kutumiwa tena nchini Ugiriki.
Inaaminika kwamba mifuko hiyo ambayo haiwezi kutumika ilikotoka, iliuziwa dalali mmoja wa eneo ambaye aliinunua na kupanda usafiri wake.
Maili 350 ya Pwani ya Liberia ina lindwa na maafisa wa kushika doria na mara nyingi meli za uvuvi za kimataifa huingia eneo hilo kinyume cha sheria.
Pia unaweza kusoma:
Marufuku ya Mifuko ya Plastiki Afrika Mashariki
Tanzania, ilianza kutekeleza marufuku ya mifuko ya plastiki Juni 1, 2019 ambapo ni kosa la jinai kutengeneza, kuagiza, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki nchini Tanzania, na wote watakao kaidi marufuku hiyo watakutana na mkono wa sheria.
Mifuko ya plastiki inalaumiwa pakubwa kwa uchafuzi wa mazingira duniani, na harakati za kukomesha matumizi yake yanalenga kulinda mazingira.
Hata hivyo, marufuku hiyo haihusishi vifungashio vya plastiki vya bidhaa mbalimbali.
Kifungu cha nane cha kanuni ya sheria ya usimamizi wa mazingira nchini Tanzania inaorodhesha makosa matano ambayo ni; kuzalisha na kuagiza mifuko ya plastiki, kusafirisha nje ya nchi mifuko ya plastiki, kuhifadhi na kusambaza mifuko ya plastiki, kuuza mifuko ya plastiki na mwisho kumiliki na kutumia mifuko ya plastiki.
Kila kosa lina adhabu yake kwa mujibu wa kanuni hizo kulingana na uzito wa kosa lenyewe.
Nchini Kenya yeyote anayepatikana akitengeneza, kuuza au kutumia mifuko hiyo ya plastiki anaweza kupigwa faini ya hadi dola 40,000 au kufungwa jela hadi miaka minne.