Chakula kilichozalishwa kwenye 'anga' kinaweza kushindana na soya sokoni

Wanasayansi wa Finland wanaotengeneza protini kutokana na hewa wanasema kuwa mauzo ya bidhaa hiyo yatashindana na soya ndani ya kipindi cha miaka 10.

Protini inatengenezwa kutokana na bakteria wa kwenye udongo ambao wamekula hidrojeni iliyofyonzwa kwenye maji kwa kutumia umeme.

Watafiti wanasema kwamba ikiwa umeme unatoka kwenye nishati ya jua na upepo, chakula kinaweza kukua bila ya uwepo wa uchafuzi wa mazingira.

Ikiwa ndoto zao zitatimia, juhudi hizo zinaweza kusaidia dunia kukabiliana na changamoto nyingi za kilimo.

Mwaka jana, watafiti walikuwa wanatafuta ufadhili kupanua mradi wao.

Na hadi kufikia sasa, wanasema kwamba wamefanikiwa kupata euro milioni 5.5 za uwekezaji na wanakadiria kwamba japo itategeme na gharama ya umeme - gharama yao itakuwa sawa na ya uzalishaji wa soya kufikia mwishoni mwa karne hii - pengine mwaka 2025.

Kwanini Protini haina ladha?

Nilikula kiasi kidogo tu cha unga wa protini mpya unajulikana kama Solein - lakini haukuwa na ladha kabisa, sawa na dhamira ya wanasayansi.

Wanataka uwe wa kawaida tu.

Inaweza kufananishwa na mafuta ya mawese katika utengenezaji wa aiskrim, biskuti, tambi, sosi au mkate.

Wabunifu wanasema inaweza kutumiwa kama njia ya utengenezaji nyana au samaki kwa namna isiyo ya asili.

Pia naweza kupewa mifugo kama ngome na hivyo basi kuepuka wasile zao la soya shambani.

Hata mambo yakifanyika kama ilivyopangwa - ambayo bila shaka itachukua miaka mingi kabla uzalishaji wa protini hiyo kuongezeka kukidhi mahitaji ya watumiaji kote ulimwenguni.

Lakini hii moja ya miradi mingi inayolenga utengenezaji wa vyakula kwa njia isiyo ya asili siku za baadaye.

Mkuu wa shirika hilo Pasi Vainikka, alisomea Chuo Kikuu cha Cranfield Uingereza na kwa sasa ni Profesa wa chuo kikuu cha Lappeenranta .

Wazo la utengenezaji chakula kwenye anga

Aliniambia kwamba wazo lililopelekea teknolojia hii awali ilibuniwa kwa ajili ya viwanda vya anga za mbali miaka 1960.

Anakiri kwamba mmea wake wa mfano umechelewa kukua lakini utakuwa tayari kufikia 2022.

Uamuzi wa kuwekeza katika mradi huu utafikia mwaka 2023 na ikiwa kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa, kiwanda cha kwanza kitakuwa tayari 2025.

Anasema: “Hadi kufikia sasa tunaendelea vizuri. Tukishaanza kupanua kiwanda kwa kutengeneza bidhaa zingine na kutumia teknolojia kama nishati ya jua na upepo, tunaimani tunaweza kushindana na wazalishaji wa soya kuanzia mapema mwaka wa 2025.”

Ili kutengeneza Solein, tunatumia haidrojeni na kaboni dioksidi kutoka kwenye hewa na kisha bakteria wanapewa madini, na baadaye wanatengeneza protini hii.

Cha msingi anasema itakuwa ni bei ya umeme. Kampuni hiyo inatarajia kwamba upatikanaji wa vyanzo vingi vya nishati utapunguza gharama ya uzalishaji.

Teknolojia hii ya pekee imesifiwa sana na George Monbiot, mwanamazingira aliyetengenza makala ya kwenye televisheni, yaliyoangazia athari za mazingira kutokana na viwanda vya nyama.

Matumaini kwa siku za baadaye?

Monbiot amekuwa na wasiwasi kuhusu hatma ya sayari lakini shirika la Solar Foods limempa matumaini.

Anasema: “Uzalishaji wa chakula unaharibu mandhari ya dunia. Uvuvi na ukulima ndio vyanzo vikuu vya kutoweka kwa mimea na wanyama duniani.

Ukulima ni moja ya sababu kuu ya mabadiliko ya tabia nchi.

Lakini ubinifu wa uzalishaji chakula bila kutumia ardhi kumetoa matumaini ya kulinda wanyama na hata sayari ya dunia.

“Kwa kuanza mbinu mpya uzalishaji chakula, kutasaidia kunususru spishi na hata dunia na tutaweza kupata lishe bila kuharibu mazingira.”