Faustin: 'Nilidukuliwa kwenye mawasiliano ya WhatsApp sasa nina hofu kuhusu maisha yangu'

Mwezi Aprili, Faustin Rukundo alipokea simu ya ajabu ya WhatsApp kutoka kwenye namba ambayo hakuitambua.

Alipokea lakini laini ya simu ilikuwa kimya kisha ikakatika.

Alijaribu kuipiga lakini haikupokelewa.

Bila kujua , simu yake ilikua imeathirika.

Akiwa raia wa Rwanda aliyepata hifadhi uhamishoni Leeds, Bwana Rukundo tayari alikuwa tayari na wasiwasi. alitafuta namba ile mtandaoni na kugundua kuwa simu ile ilitoka Sweden.

Ni ajabu, alifikiria, lakini muda mfupi tu alisahau kuhusu tukio hilo.

Kisha namba ile ilipiga tena kwa mara nyingine tena hakuna aliyepokea.

Pia kulikua na namba ambazo ziliita na hazikupokelewa namba ambazo hakuzitambua pia na akaanza kuhofia usalama wa familia yake, hivyo akanunua simu mpya.

Ndani ya siku moja, namba isiyojulikana ilipiga tena.

''Nilijaribu kupokea ikakatwa kabla sijasikia sauti ya aliyepiga,'' Bwana Rukundo aliiambia BBC.

''Kila nilipojaribu kupiga, hakuna aliyepokea. Nikabaini kuwa kuna kitu hakiko sawa nilipoona baadhi ya taarifa faili zangu zinapotea kwenye simu.

''Nilizungumza na wenzangu wa chama cha Rwanda National Congress na wao pia walikua wamekumbana na tukio hilo.

Walikua wanapata namba ngeni kwenye simu zao kama ilivyokuwa kwangu.''

Ilipofika mwezi Mei , Bwana Rukundi alisoma ripoti kuwa WhatsApp imedukuliwa, ndipo alipogundua kilichotokea.

''Kwanza nilisoma taarifa hiyo kwenye BBC na nikawaza aaah taarifa hii inaweza kuwa majibu ya kile kilichonitokea siku za nyuma,'' alieleza.

''Nilibadilisha simu na kugundua kosa langu. walikuwa wanafuatilia namba yangu na kuweka mfumo wa kudukua katika kila simu kwa kupiga namba ileile.''

Kwa miezi kadhaa Rukundo aliamini yeye na wenzake walikuwa kati ya watu karibu 1,400 waliokuwa wamelengwa na wadukuzi kupitia WhatsApp.

Lakini ilithibitishwa juma hili baada ya kupokea simu kutoka maabara ya Citizen mjini Toronto.

Kwa miezi sita, shirika lilikuwa likifanya kazi na Facebook kuchunguza udukuzi na kubaini walioathirika.

Watafiti wanasema ''Katika uchunguzi maabara ya Citizen imegundua visa 100 vya udhalilishaji vilivyowalenga watetezi wa haki za binaadamu na waandishi wa habari katika nchi karibu 20 dunani.

Bwana Rukundo aliyejipambanua kwenye ukurasa wake wa WhatsApp ni mkosoaji wa utawala wa Rwanda, sambamba na wengine wa kaliba yake walikuwa walengwa.

Mtandao wa udukuzi ulijengwa na kuuzwa na kampuni moja yenye makao makuu yake nchini Israel NSO na kuuza kwa serikali mbalimbali duniani.

Wadukuzi walitumia programu za kuwapeleleza waandishi wa habari, wanaharakati wa haki za binaadamu, lakini tukio hilo kwake liliifanya familia yake kuogopa mno.

''Kwakweli , hata kabla sijathibitiha hili, tulipigwa na butwaa na kuingiwa na hofu. Inaonyesha kuwa walikua wakiifuatilia simu yangu kwa karibu majuma mawili na waliweza kufikia kila kitu,'' aliiambia BBC.

''Si tu shughuli zangu wakati huo lakini historia za mawasiliano yangu ya barua pepe na watu ninaowasiliana nao na kuzungumza nao.Kila kitu kilikua kinanaswa, Kompyuta, simu zetu, hakuna kilichokuwa salama.Hata tulipokua tukiongea, huenda walikua wanasikiliza pia.Bado ninahisi siko salama.''

Bwana Rukundo alitoroka Rwanda mwaka 2005 baada ya wakosoaji wa serikali kukamatwa na kutupwa gerezani. Alipambana ili mke wake aachiwe baada ya kutekwa na kushikiliwa kwa miezi miwili.

Facebook, mmiliki wa WhatsaApp, anajaribu kuishtaki kampuni ya NSO.

NSO imekana shutuma dhidi yake.

Programu hiyo ya simu inatumiwa na watu karibu bilioni 1.5 katika nchi 180.

Waathirika wanaweza wasitambue kama wanadukuliwa. Katika baadhi ya matukio vitu walivyotambua ni simu za kushangaza za WhatsApp.

Nyaraka za mahakama zinasemaje kuhusu madai ya Facebook:

-Inaamini kuwa udukuzi umefanyika katika mifumo ya mitandao ya Kompyuta

-Imetaka Kampuni ya NSO kutotumia majukwaa yeyote ya Facebook.

-Facebook imedai kuwa NSO imekuwa ikifanya vitendo vya udukuzi kwa niaba ya wateja wake.

AWS inamilikiwa na Jeff Bezos ambaye anamiliki jarida la Wall Street, jarida ambalo mwanahabari wa Saudia aliyeuawa Jamal Khashoggi alilifanyia kazi.

NSO imeshutumiwa kusambaza programu ya ufuatiliaji iliyofanya wauaji wa Khashoggi kumnasa.

NSO imekana mashtaka dhidi yake na kusema kuwa watapambana dhidi ya madai haya mapya.