Korea Kaskazini na Marekani zimefufua upya mazungumzo ya nyuklia

Chanzo cha picha, Reuters
Maafisa wa Marekani na Korea Kaskazini wamewasili nchini Uswidi wa duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia yanayolenga kutatua mzozo kati ya mataifa hayo mawili.
Mkutano wa mwisho kati ya rais wa Marekani Donald Trump na rais wa Korea Kaskazini Kim Jong-un yalimalizika bila makubaliano yoyote.
Tangu wakati huo hatua chache zimepigwa lakini pande zote mbili zimesisitiza kuwa zinataka mashuriano kuhusu sula hilo kuendelea.
Mazungumzo haya mapya yanajiri siku kadhaa baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la kurusha aina mpya ya kombora, na pia kufanikiwa kurusha makombora ya masafa mafupi tangu mwezi Mei.
Kombora hilo lililorushwa kutoka kwenye nyambizi chini ya bahari ina maanisha kua Korea Kaskazini ina uwezo wa kufyetua kombora kutoka nje ya ardhi yake.

Chanzo cha picha, KCNA via REUTERS
Kabla ya jaribio la kurushwa kwa kombora hilo, Korea Kaskazini na Marekani zilithibitisha kuwa inajiandaa kufanya mazungumzo kuhusu nyuklia ndani ya wiki hii. Ingawa hakuna uhakika kama mazungumzo hayo yataendela .
Marekani ilikuwa na lengo la kutaka taifa hilo kusitisha matumizi ya nyuklia.
Taifa hilo limepigwa marufuku na kutumia makombora ya masafa marefu na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huku mpango wake wa nyuklia ukiwekewa vikwazo na Marekani na Umoja wa Mataifa.
Majadiliano ya sasa yanafanyika katika kisiwa cha Lidingo, kaskazini mashariki mwa mji wa Stockholm, ambako mjumbe maalum wa Marekani Stephen Biegun na mwakilishi wa Korea Kaskazini Kim Myong Gil wanatarajiwa kukutana.
Kwanini mazungumzo haya yanafanyika sasa?
Uhusiano kati ya Bw. Trump na Kim Jong Un yamekua yakisua sua kwa miezi kadhaa tangu mkutano wa Hanoi ulipomalizika bila mwafaka wowote.
Lakini mazungumzo haya yanakuja wakati ambapo Rais Trump anakabiliwa na kashfa ambayo uchunguzi ukithibitishwa huenda akaondolewa madarakani kupitia kura ya kutokuwa na imani nae au kupoteza uungwaji mkono katika baadhi kura ya maoni.

Chanzo cha picha, Reuters
Korea Kaskazini inafahamu hilo na huenda ikatumia furasa hio kufikia mkataba utakaozingatia maslahi yake na BwTrump kuliko rais mwingine yeyote wa Marekani.
"Pande zote mbili zinafahamu kuwa muda unayoyoma, huku Trump akijiandaa kugombea mhula wa pili wa urais mwaka ujao, licha ya siasa kali inayomkabili kwa sasa nchini Marekani," mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Korea Kaskazini Minyoung Lee aliiambia BBC.
Tutarajie nini?
Ni vigumu kubashiri majadiliano ya nyuklia kati ya Marekani na Korea Kaskazini, anasema Andray Abrahamian, mashauri mkuu na mwanazuoni wa masuala ya Pacific.
"Licha ya taarifa finyu kuhusu majadiliano haya mapya tunajaribu, kubaini kama hatua hii ya sasa itakua na umuhimu wowote hasa wakati huu ambapo utawala wa Trump unakabiliwa na changamoto za kisiasa nyumbani," alisema.
Utakumbuka mazungumzo ya mwisho kati ya viongozi hao mjini Hanoi uliwashangaza watu baada viongozi hao kutofautiana.
Tangu wakati huo Bw. Trump na Kim walikutana katika mpaka wa Korea Kaskazini mwezi Juni.












