Mbio za dunia za riadha: Kenya ilivyonyakua dhahabu kimiujiza kutoka kwa Ethiopia

Chanzo cha picha, AFP
Mwanariadha wa Kenya Conselsius Kipruto alimshinda Lamecha Girma wa Ethiopia katika fainali ya kusisimua ya mbio za mita 3,000 kuruka vizuizi na maji katika mashindano ya Dunia ya riadha yanayondelea mjini Doha Qatar.
Girma aliongoza mbio hizo hadi sekunde ya mwisho lakini Kipruto, ambaye alionekana kama alifanikiwa kumfikia na na kunyakua ushindi uliosaidia kuhifadhi taji la dunia la mbio hizo.
Alifahamu ushindi wake sekunde 30 baada ya wasimamizi wa mashindani hayo kuthibitisha ushindi wake.
Kipruto, 24, alikimbia mbio hizo kwa muda wa dakika 8:01.35.

Chanzo cha picha, Reuters

Mwanariadha huyo wa miaka 18 wa Ethiopia aliweka rekodi mpya ya kitaifa ya mbio hizo kwa muda wa dakika 8:01.36.
Mwanariadha wa Morocco Soufiane el Bakkali aliibuka wa tatu kwa kumaliza mbio hizo kwa 8:03.76.
Akizungumza baada ya mashindano hayo, Kipruto, alielezea mita 100 ya mwisho kama muda ''wa kushangaza zaidi...Si kuamini macho yangu".
Akizungumzia muda wakusubiri matokeo rasmi aliesma: "Nilikua naomba: 'wacha mshindi awe ni mimi.'"
Kenya imetawala mbio hizi tangu mwaka wa 1991 Moses Kiptanui aliposhinda dhahabu katika mbio za dunia mjini Tokyo na kuhifadhi ubingwa huo mwaka wa 1993 na 1995.
Kwa Jumla Kenya imeshinda mbio hizo mara 12 kwenye mashindano ya dunia.
Majirani wa Kenya, Ethiopia wamekua wapinzani wao wakuu katika mashindano ya riadha, huku mataifa hayo mawili yakitawala mbio za masafa ya kadri na ya masafa marefu.
Ushindi wa Kipruto unamaanisha kuwa Kenya imejinyakulia medali tatu za dhahabu katika mashindano hayo ya Dunia ya Riadha wakilinganishwa na mahasimu wao Ethiopia walio na medali moja ya dhahabu.













