Korea Kaskazini: Huenda taifa hilo limerusha kombora kutoka kwa nyambizi

Baada ya likizo Korea Kaskazini imerejelea majaribio yake ya silaha

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha, Baada ya likizo Korea Kaskazini imerejelea majaribio yake ya silaha

Korea Kaskazini huenda ilirusha kombora la masafa marefu kutoka katika nyambizi yake, hatua ambayo inajiri saa chache baada ya Pyongyang kusema kwamba itarudia mazungumnzo ya kinyuklia na Marekani.

Maafisa wa Korea Kusini wanasema kwamba kombora lililorushwa karibu na bandari ya Wohsan liliruka takriban kilomita 450 na kwenda urefu wa kilomita 910 juu kabla ya kuanguka katika bahari ya Japan.

Iwapo itathibitishwa hiyo itakuwa hatua kubwa iliopigwa na taifa hilo kutoka majaribio ya silaha za masafa mafupi ambayo limekuwa likifanya tangu mwezi Mei.

Habari hizo zilivutia shutuma kutoka maeneo mbalimbali.

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema kwamba huo ni ukiukaji wa maamuzi ya baraza la usalama la umoja wa mataifa ambayo yalipiga marufuku taifa hilo kutotumia makombora ya masafa marefu.

Mapema , Pyonyang ilikuwa imesema kwamba mazungumzo ya nyuklia na Washington huenda yakaendelea wiki hii.

Picha za makombora yalioundwa na Korea Kaskazini

Mazugumzo hayo yalikwama tangu mkutano wa Hanoi kati ya rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un mnamo mwezi Februari ambayo yalikamilika bila mwafaka

Wataalam wanasema kwamba uhusiano wa jaribio hilo na matangazo ya mazungumzo hayo yalifanyika makusudi.

Korea Kaskazini inataka kufanya mazungumzo yake kuwa wazi kabla ya mazungumzo hayo kuanza, kulingana na Harry Kazianis wa kituo cha kitaifa cha maslahi ya Marekani mjini Washington akizungumza na chombo cha habari cha AFP.

Pyongyang inaonekana kuishinikiza Washington kuwacha masharti yake ya zamani ya mipango ya kinyuklia kwa kile ambacho ni ahadi za kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.

Nini kilichotokea baada ya Kombora hilo?

Ripoti za kwanza zilijiri alfajiri wakati mamlaka ziliripoti kwamba makombora mawili yalikuwa yamerushwa huku mojawapo likianguka katika maji ya Japan.

Baadaye waziri mwenye wadhfa wa juu zaidi nchini Japan Yoshide Suga alisema katika mkutano na vyombo vya habari kwamba kombora moja lilipasuka na kutawanyika kabla ya kuanguka majini.

Liliruka urefu wa kilomita 910 ilisema Korea Kusini ambayo ni mara mbili ya urefu wa kituo cha kimataifa cha angani .

Mwaka 2017 Kombora la Korea Kaskazini la Hwasong lilifika urefu wa kilomita 4,500.

Jaribio hilo la siku ya Jumatano litakuwa la 11 kutoka Korea Kaskazini mwaka huu, lakini mamlaka imeonyesha wasiwasi wake kuhusu uwezo wa kombora hilo.

Korea Kaskazini imekuwa ikiunda makombora yanayoweza kurushwa kutoka katika manuwari kwa muda sasa kabla ya kusitisha majaribio yote ya makombora ya masafa marefu.

Baraza la usalama la Korea Kkusini lilionyesha wasiwasi wake na kusema kwamba linaweka uzito wake kwamba kombora hilo lilirushwa kutoka kwa manuwari SLBM, kulingana na chombo cha habari cha taifa la Korea Kusini Yonhap.

Kombora la mwisho la SLBM lililofanyiwa majaribio na Korea Kaskazini linafikiriwa kufanyika mwaka 2016 Agosti kabla ya rais Trump kuchukua madaraka.

Miaka miwili baadaye rais Trump na Kim jong un waliweka historia baada ya kuwa marais wa kwanza wa Marekani na Korea Kaskazini kukutana.

Lakini licha ya mikutano ya ana kwa ana , kumekuwa na hatua chache zilizopigwa kuafikia makubaliano kuhusu kile cha kufanyika kuhusu uwezo wa kinyuklia wa taifa la Korea Kaskazini.