Je unafahamu kuwa jina ulilopewa linaweza kuathiri tabia yako?

    • Author, Faith Sudi
    • Nafasi, BBC News Swahili

Kila binadamu ana jina ambalo aliitwa wakati alipozaliwa, lakini unafahamu kuwa jina ulilopewa linaweza kuathiri tabia yako, wanasema wataalamu

Ni dhahiri kwamba hakuna kiumbe kisichokuwa na jina, iwapo kiumbe hicho kiliumbwa wakati dunia ilipoanza au hata kimebuniwa hivi karibuni mfano vile vitu vilivyoumba kiteknolojia, mithili ya binadamu na vinginevyo.

Lakini Je ni watu wangapi wanajua maana ya majina yao au hata kile kilichopelekea wao kuitwa majina hayo na ni vipi jina linaweza kuathiri tabia ya mtu?.

Jamii nyingi awali zilikuwa zikiwapa majina watoto kulingana na majira, nyakati, misimu ambayo watoto hao wamezaliwa au namna mtoto alivyozaliwa.

Hata hivyo kuna baadhi ya jamii ambazo ziliwapatia watoto majina ya mababu. Lakini hata hivyo mtu ambaye angetajiwa jina lazima angekuwa ni mtu ambaye jamii ilitambua maadili yake, mfano mtu ambaye alifariki kwa kujiua alipewa jina fulani.

Aggrey ondiege anatoka katika kabila la Luo Magharibi mwa Kenya. Watu kutoka kabila lake huchanganya nyakati na majira.

"Katika kabila letu walikuwa wakitumia wakati kumpatia mtoto jina la kwanza... Kama mtoto amezaliwa, asubuhi au mchana. Kama amezaliwa mchana anaitwa Ochieng akiwa mvulana ama Achieng akiwa msichana. Pia tuliwapatia majina kulingana na majira. Wakati wa mvua au ukame. Tulichanganya majina ya wakati na yale ya majira. Kwa mfano Okinyi au Akinyi wakati wa mvua. Kwa hivyo kama mtoto msichana angezaliwa wakati wa mchana na katika majira ya mvua angeitwa Achieng Akinyi"

Jamii hii hutumia silabi "a" kuanza jina la watoto wasichana na "o" kwa watoto wavulana.Hata hivyo namna mtoto alivyozaliwa pia hutumiwa kama kigezo cha kumpatia mtoto jina.

"Kama mtoto amezaliwa kifudifudi angeitwa Awino ama Owino. Namna ya kuzaliwa ilitumiwa kumpa jina."

Watoto mapacha katika jamii hii hupewa majina teule kulingana na nani anatangulia kuzaliwa.

"Watoto wanaotangulia kuzalliwa kama ni mvulana ataitwa Opiyo, kama ni msichana ataitwa Apiyo na mtindo huu hutumiwa pia na jamii ya Waluhya nchini Kenya ambapo Pacha anayetangulia huitwa Mlongo na wa pili huitwa Mukhwana.

Vigezo vya majina Tanzania?

Nchini Tanzania, Wajita wanaotokea kanda ya ziwa hutoa majina kutokana na majira ya hali ya hewa, mfano vipindi vya kulima basi mtoto ataitwa Malima, kipindi kikiwa na nyasi nyingi basi anaitwa Manyasi, na kuna kipindi cha viazi vingi basi mtoto ataitwa Manumbu inayomaanisha viazi.

Mzee Manyasi Bhusaghwafu ni Mjita kutoka Musoma Mara. Ana watoto 6 na amewapatia majina kulingana na vipindi.

"Mmoja anaitwa Malima yeye alizaiwa kipindi cha kilimo. Kuna kaka yangu alipewa jina la Manumbu kipindi hicho kulikua na viazi vingi sana "

"Kwetu huwezi tu kutoa jina bila kuwa na Maana hata Kama sio kipindi lakini lazima kutakua na maana nyingine "

Unaweza pia kusikiliza:

Kulingana na tamaduni nyingi za Afrika, kuna wakati ambapo mtoto angeitwa jina kisha mtoto huyo alie sana. Hiyo ingesababisha mtoto kubadilishiwa jina.

Katika karne hii ya ishirini na moja, watu wengi ni watumwa kwa sababu hawafuatilii mila wakati wa kupeana majina.

Kinyume na awali, siku hizi watu huwaita watoto kulingana na jinsi mtu anavyopenda. Kuna wale ambao huwaita kulingana na watu kwenye filamu walizotizama au watu waliotajika.

Lakini je majina yako na athari gani Kwa tabia anazokuwa nazo mtu?

Wanasaikolojia wanaelezea jina kuwa kitambulisho muhimu sana Kwa binadamu. Jina hutambulisha jinsia ya mtu, jinsi tunavyojichukulia katika jamii.

"Mbali na kwamba jina hutambulisha kabila au sehemu anakotoka mtu, jina lina nguvu sana katika tabia anayokuwa nayo mtu. Watoto wengi huishia kufuata tabia ya mtu aliyetajiwa jina iwapo ni nzuri au mbaya" Perpetua Wanyugi ni mwanasaikolojia nchini Kenya.

Jina pia linaweza kumbagua au kumdhalilisha mtu hasa kikazi.

" Kijinsia mtu anaweza kubaguliwa kutikana na jina lake. Mfano Mwanamke anayefanya kazi ya kiufundi au ya suluba."

Wanasayansi wanaamini kwamba jina huathiri uamuzi wa mambo mengi maishani Kwa mfano mahali atakoishi mtu, atakayemuoa, na alama atakazopata shuleni.

Unaweza pia kutazama:

" Jamii nyingi za Kiafrika huamini kwamba jina ni kitu Tu cha kumtambulisha mtoto, na haina athari zozote" Perpetual Wanyugi.

Barani Afrika kumekuwepo na visa vingi ambavyo vimeshuhudiwa wakati wa uchaguzi katika mataifa mengi ambapo kabila nyingi hulazimika kuyahama makazi yao kutokana na hofu ya kuvamiwa na makabila yanayodai kumiliki sehemu hizo.

Huenda hii ikawa ndiyo sababu kuu ya kuwafanya watu katika karne hii kuiga mtindo tofauti lakini wanasayansi wanashauri kwamba watoto wapewe majina ambayo Yana maana nzuri ili kuwawezesha kuafikia mambo makuu na kuwafanya kujiamini maishani.