Marekani imepuuza mapambano dhidi ya ubaguzi wa watu weupe?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka nchini Marekani inachunguza tukio la shambulio la kutumia silaha katika mji wa El Paso ambao uligharimu maisha ya watu 22 shambulio linaloelezwa kuwa "ugaidi wa ndani". Ugaidi huu ni tishio kubwa kiasi gani? na ni kwa namna gani Marekani inapambana kudhibiti vitendo hivyo?
Polisi wanaamini mtuhumiwa mzungu, Patrick Crusius, aliendesha gari umbali wa mamia ya maili mjini Texas kwenda kwenye mji uliokuwa na watu wengi wa wenye asili ya Uhispania kutekeleza shambulio lake.
Anaaminika kuwa mwandishi wa hati iliyotumwa dakika chache kabla ya shambulio ambalo lilisema shambulio hilo ni "majibu ya uvamizi watu wenye asili ya Uhispania katika mji wa Texas".
Katika taarifa yao, FBI ilisema kuwa aina hii ya ghasia ilikuwa ikiongezeka na mengi kati ya matukio haya yalikuwa yakichochewa na itikadi za rangi .
Wachambuzi wanasema wauaji hawa wanashiriki itikadi ya pamoja, moja ya dhuluma, uhasama na chuki, na wanachochewa na watu wanaokutana nao katika jamii za mtandaoni kama vile 4chan na 8chan, sehemu ambazo wameweza kujadili kwa uhuru uzalendo wa watu weupe na aina nyingine mbaya za ubaguzi.
Mamlaka za Marekani zimejaribu vya kutosha?
Maafisa wa FBI wanasema uchunguzi wao umeendelea kukabili tishio linaloibuka kutoka kwa vikundi hivi.
Mwezi Julai, Mkurugenzi wa FBI Christopher Wray aliwaambia wajumbe wa kamati ya bunge la seneti ya Marekani kwamba vikosi vya usalama viliwakamata watu kadhaa wakihusishwa na vitendo vya kigaidi katika kipindi cha miezi tisa iliyopita.
Wray alisema kesi hizi ni pamoja na aina mbili tofauti - "vurugu za nyumbani", neno ambalo yeye na maafisa wengine wa FBI hutumia kuelezea watu ambao wamehamasishwa na makundi ya jihadi" na "msimamo mkali wa ndani", kundi ambalo kulingana na Wray, inajumuisha wale ambao "wamehamasishwa na toleo fulani la kile unachoweza kuita ubaguzi wa weupe.
Takribani watu 100 walikamatwa wakihusishwa na matukio ya mashambulizi.
Wakosoaji wanasema mamlaka za nchi hiyo wamekuwa wakisisitiza zaidi kuwatafuta ''majihadi'' nchini Marekani na kupambana na makundi yanayofanya vitendo vya kibaguzi.
''Gaidi mwenye asili ya mzungu hajatiliwa maanani sana kama ilivyo kwa gaidi wa kundi la wanamgambo wa kiislamu,'' anasema Daniel Benjamin aliyefanya kazi katika idara inayopambana na ugaidi nchini Marekani mwaka 2009 mpaka 2012.
Shambulio la 9/11
Baada ya shambulio la al-Qaeda nchini Marekani mwaka 2001, maafisa wa Washington walitenga rasilimali kubwa katika juhudi za kupambana na ugaidi, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na taasisi ya Stimson , Marekani ilitumia dola trilioni 2.8 mwaka wa fedha wa 2002 mpaka 2017 kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Kwa kipindi chote hicho , kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo, uwekezaji uliofanyika kwa ajili ya azma ya kupambana na vitisho kutoka makundi kama vile al -Qaeda na Islamic State kulisababisha vitisho vingine kutoshughulikiwa, hali iliyosababisha hatari ya makundi ya watu wenye msimamo mkali yaliendelea kukua.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kitafanyika nini sasa?
Watu wengi wanahoji ikiwa maafisa wa Marekani wako tayari katika juhudi za kukabili vitisho vipya kutoka kwa makundi ya watu wa mrengo wa kulia wenye msimamo mkali.
Wengine wanasema kuwa viongozi wanakabiliwa na changamoto hiyo. "FBI imefanya kazi nzuri," anasema Richard Barrett, mkurugenzi wa zamani wa operesheni za kupambana ugaidikatika shirika la kijasusi la Uingereza. "wamekuwa makini katika kuyatolea macho makundi haya kwa muda mrefu.''
Mamlaka inachunguza mashambulizi ya risasi huko El Paso kama kesi ya ugaidi wa ndani. Vile vile wanajaribu kuwazuia wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia kuchochewa na mitandao ya kijamii na mitandaoni na wamelazimisha mtandao mmoja kufungwa.
Siku ya Jumatatu Trump alichukua hatua madhubuti zaidi baada ya mashambulio huko El Paso: "Kwa sauti moja taifa letu lazima likomeshe ubaguzi wa rangi ," alisema.
Wakosoaji wa rais wanangojea kuona ikiwa sasa anaendelea na msimamo huo.
Rais wa Marekani Donald Trump alielezea shambulio hilo kama kitendo cha uoga.
''Najua kwamba tunaungana na kila mtu katika taifa hili kushutumu kitendo hiki cha chuki, hakuna sababu ambazo zinaweza kukufanya kuwaua watu wasio na hatia'' , alindika katika mtandao wake wa Twitter.
Waathiriwa bado hawajatajwa lakini rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador alisema kuwa raia watatu wa Mexico ni miongoni mwa waliofariki, kulingana na chombo cha habari cha Reuters.
"Sisi kama taifa tunaungana kuwaunga mkono waathiriwa na familia zao'' , alisema bwana Abbot.
Lazima tufanye kitu kimoja , leo chengine kesho na kila siku baada ya hili - lazima tushirikiane.












