Marekani ina mpango wa kurejesha ushawishi barani Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imekuwa ikipoteza ushawishi barani Afrika- lakini mwanadiplomasia wa juu wa nchi hiyo barani Afrika anataka kubadili hali hiyo.
''Kwa muda mrefu wakati wawekezaji walipokuwa wakibisha milango na waafrika wakifungua, mtu pekee aliyekuwa hapo ni mchina,'' Tibor Nagy, mjumbe wa maswala ya Afrika wa Marekani aliiambia BBC hivi karibuni.
Biashara ya China na bara la Afrika imeifunika Amerika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, na mwaka 2018 ilikuwa kubwa mara tatu zaidi.
Baadhi ya nafasi za kidiplomasia katika miji mikuu ya nchi za kiafrika zimebaki wazi tangu raisi Donald Trump aingie madarakani.
Bwana Nagy anasema anataka kubadili mambo na kurejesha ushawishi wa Marekani kwenye bara la Afrika. ''Kazi yangu ni kuhakikisha kuwa kunapobishwa hodi, kuna mmarekani pia,'' alisema.
Je Marekani inaweza kubadili mawimbi na kupambana na China kwenye bara la Afrika?
Uhusiano wa kidiplomasia
Uteuzi wa mabalozi wa Marekani kwa nchi za Afrika umeendelea kufanyika polepole katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Nafasi zikiwemo nchini Afrika Kusini na Nigeria zimebaki tupu tangu Trump alipowaondoa mabalozi wa Marekani wote duniani baada ya kuingia madarakani.
Baadhi waliteuliwa na raisi, kama balozi wa Afrika Kusini na Nigeria ambao wanasubiri kuthibitishwa lakini kwa nafasi nchini Chad na Tanzania, zimeendelea kuwa wazi.
Bwana Nagy aliteuliwa kwenye nafasi ya mwakilishi barani Afrika , nafasi ambayo awali iliachwa wazi kisha baadae kuwa na uteuzi wa muda.
Wachambuzi wa mambo wanasema, tofauti na China ambayo imekuwa ikipeleka maafisa wake kwenye nchi za Afrika.
''Nchini Afrika Kusini, China ina mwanadiplomasia wa juu- hii inamaanisha kuwa ni eneo muhimu kwa Beijing,'' anasema Lina Benabdallah, mtaalamu wa mahusiano ya China na Afrika katika chuo cha Wake Forest.
Idadi kubwa ya mataifa yanayoibukia kama Uturuki na India, wanatanua uwepo wao katika nyanja za kidiplomasia.
Serikali ya India hivi karibuni iliidhinisha mipango ya kufungua ofisi za kibalozi mpya 18 barani Afrika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lugha ya kidiplomasia
Mahusiano hayajawahi kusaidiwa na taarifa kuhusu Afrika kutoka kwa maafisa wa serikali ya Marekani, ikiwemo raisi, ambazo zimekuwa zikitazamwa kama za kuudhi
Trump ameripotiwa kueleza mataifa ya kiafika kuwa ni ''nchi chafu'' na kuongelea Afrika kama sehemu ambayo marafiki zake wanakwenda kujaribu kutajirika.
Pia aliingia kwenye mvutano na Afrika Kusini alipoeleza kuhusu suala la kunyakua ardhi kutoka kwa wakulima wa kizungu nchini humo, hali iliyosababisha ghadhabu kutoka kwa serikali ya Afrika Kusini.
Marekani imekuwa chanzo kikubwa cha uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika, lakini mchango wake umekuwa ukipungua.
Mwaka 2018, China ilitangaza uwekezaji wa thamani ya dola za kimarekani bilioni 60 kwa ajili ya miradi ya miundombinu.
Bi Benabdallah amesema kuwa biashara kati ya Marekani na mataifa ya Afrika imeshuka kwa sababu ya ongezeko la uhitaji si tu China,lakini nchi nyingine kama vile Urusi na Uturuki.
''Nafikiri ni kwa sababu ushindani kutoka kwa nchi nyingine umeongezeka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita,'' amesema bi Benabdallah.
Ukuaji wa uchumi wa China umeonyesha dalili za kushuka hivi karibuni, hali ambayo itaathiri biashara na uwekezaji katika Afrika siku za usoni.
Lakini kutokana na ushindani kutoka duniani kote kwa kufanya biashara na nchi za kiafrika, Marekani inapaswa kurejesha mahusiano na bara la Afrika ikiwa inataka kujihusisha nchi za uchumi unaochipukia.














