AFCON2019: Kenya kutafuta alama muhimu dhidi ya Senegal, Tanzania kumaliza ratiba na Algeria

Olunga

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Kenya watakuwa wanamtegemea mshambuliaji Michael Olunga kuivunja ngome ya Senegal

Ni vita vya kufa na kupona kwa Senegal na Kenya usiku wa leo jijini Cairo pale timu hizo zitakapokutana katika mechi ya mwisho ya Kundi C.

Timu zote zina alama tatu baada ya kucheza michezo miwili, wakishinda mchezo mmoja na kufungwa mmoja.

Iwapo watatoka sare, Senegal itasonga moja kwa moja kama timu ya pili, na Kenya huenda ikasonga pia kama moja ya timu ya tatu kwenye makundi ambayo imekuwa na matokeo mazuri (best looser).

Algeria tayari imeshafuzu hatua ya mtoano kutoka kwenye kundi hilo baada ya kushinda mechi zao mbili za mwanzo.

Awali waliwafunga Kenya 2-0 kisha Senegal 1-0.

Leo hii wanacheza na Tanzania ambao matumaini yao ya kuendelea kusalia Misri ni ya kinadharia zaidi ya uhalisia.

Tanzania inaweza kuwa na nafasi ya kufuzu hatua inayofuata kutokea kundi hilo endapo Kenya watafungwa na Senegal na wao kumfunga Algeria goli 4-0.

Kiuhalisia, Senegal kumfunga Kenya ni jambo linalowezekana, lakini Tanzania kushinda 4-0 ama zaidi mbele ya Algeria ni kitu ambacho hakiyumkiniki, japo mpira unadunda.

Vita ya Maneno

Tayari makocha wa Senegal na Kenya wapo katika vita kali ya maeneno kabla ya mchezo wa leo.

Hata hivyo, ni kocha wa Kenya, Sebastien Migne ambaye ndiye alianza uchokozi huo.

Algeria wakishangilia

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Algeria wanavaana na Tanzania wakiwa wameshafuzu hatua ya mtoano

Migne anaonekana kushangazwa na kiwango cha Senegal na kushindwa kunyanyua kombe hilo japo hata mara moja.

"Tunajua kuwa hawajawahi kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika licha ya kuwa na kiwango sawa cha wachezaji na timu kama Cameroon na Ivory Coast, ambao wamenyanyua kombe hilo mara kadhaa. Kutokana na hilo, inatupasa tujiulize kuhusu nguvu (uwezo) wao wa kiakili," amesema Migne.

Kauli hiyo imeibua majibu ya hasira kutoka kwa kocha wa Senegal Alious Cisse, ambaye alikuwa nahodha wa kikosi cha Senegal ambacho kilifungwa kwa mikwaju ya penati na Cameroon katika fainali ya mwaka 2002.

Cisse amesema hakuna haja ya kuchanganyikiwa baada ya kufungwa na Algeria.

"Kuna mambo ambayo yalienda kombo, lakini hatuwezi kufanya mapinduzi ndani ya siku nne. Tumekuwa namba moja (kwa ubora Afrika) kwa miaka mitatu... ni kipigo chetu cha kwanza ndani ya miaka minne ndani ya Afrika, hivi timu ambayo nguvu ya kiakili inaweza kuwa na matokeo ya namna hiyo."

"Anajua nini kuhusu fikra za Kisenegali? Anawajua ipi watu wetu," ameng'aka Cisse.

Majibu yatakuwa ndani ya dakika 90 usiku wa leo.