Mzozo wa Iran na Marekani: Ndege za Kimataifa 'zaepuka' anga la Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashirika kadhaa ya ndege yamefutilia mbali safari zao au kuepuka anga la Iran baada ya ndege ya ujasusi ya Marekani isiokuwa na rubani kudunguliwa na majeshi ya ulinzi ya nchi hiyo.
Iran ilithibitisha kuwa iliangusha ndege hiyo ikisema kuwa ilikiuka sheria za anga lake-Marekani inapinga madai hayo .
Mamlaka ya usafiri wa angani nchini Marekani (FAA) imetoa agizo la kuzuia mashirika ya ndege ya marekani kupaa juu ya angaa la ghuba ya Uajemi na Oman.
Shirika la ndege la United Airlines limefuta safari yake ya kutoka Newark kwenda Mumbai .
Jeshi la Iran lilidungua ndege hiyo ya kijesusi ya Marekani isiokuwa na rubani siku ya Alhamisi, likisema kuwa hatua hiyo imetuma "Ujumbe maalum kwa Marekani".
Hata hivyo Marekani inasisitiza kuwa ndege hiyo ilikua ikipaa juu ya maji ya Kimataifa kabla kudungulia na kulaani hatua hiyo ikisema ni "ni shambulizi la kichokozi" lililofanywa na jeshi la IRGC.
Mamlaka ya FAA ilitoa arifa kwa marubani wanaotumia ndege zilizo na nambari ya usajili ya Marekani wasipae juu ya anga ya Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman.
United Airlines ilisema: "Tukizingatia matukio nchini Iran, United inatathmini upya hali ya usalama kati ya New York/Newark na India (Mumbai) kuanzia usiku huu."
Shirika la ndege la Emirates lenye makao yake Dubai limesema litaepuka kusafari katika "maeneo ambayo henda yakakumbwa na mzozo".
Msemaji wa shirika hilo la ndege amesema: "Tunafuatilia kwa makini matukio kati ya mataifa hayo mawili na pia tunawasiliana na mamlaka husika katika mataifa hayo kuhusu usalama wa ndege zetu na We na pia tutafanya mabadiliko katika huduma zetu endapo tutalazimika kufanya hivyo."
British Airways imesema kuwa itazingatia mwongozo wa FAA, wa kujiepusha na anga la Iran.
Ndege za Shirika hilo zitaendelea na safari zake lakini zitatumia njia zingine.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe

Lufthansa, ambayo husafiri Tehran, inasema illisitisha safari zake katika baadhi ya maeneo nchini Iran.
Shirika la ndege la Malaysia Airlines linasema kuwa limeamua kuepuka kupaa juu ya anga la Hormuz katika asfari zake za kwenda na kutoka London, Jeddah na Medina.
Mchanganuzi wa usafiri wa angani John Strickland ameiambia BBC: "Haya ni mashirika yalio na ushawishi mkubwa katika usafiri wa angani. Bila shaka yakisitisha safari zake au kuepuka anga la Iran yatathiri sio tu wafanyi biashara na usafiri wa Ghuba kwenyewe bali pia itavuruga usafiri wa kwenda India na sehemu zingine za Bara Asia. alisema.
"Ikizingatiwa kuwa njia zingine za ndege zimepigwa marufuku kwa sababu zinatumiwa na wanajeshi, mashirika ya ndege yatakabiliwa na changamoto nyingi ambazo itakuwa vigumu kutatua''.
Ni ndege zipi zilizobzdili mkondo wa safari?
Kwa mujibu wa shirika la Habari la Reuters, haya ndio mashirika ya ndege yaliobadilisha njia za ya ndege zao:
- Cathay Pacific
- Emirates
- FlyDubai
- British Airways
- KLM
- Qantas
- Singapore Airlines
- Lufthansa














