Mgogoro kati ya Iran na Marekani Ghuba: Je tunaelekea katika vita vya meli za kubebea mafuta?

Chanzo cha picha, Getty Images
Meli za mafuta zinazochomeka katika Ghuba. Meli za kivita za Marekani zinaingilia kati. Matamshi ya uchochezi yanazua hofu ya mgogoro mkubwa.
Tumekuwa hapa siku za nyuma: Miaka 28 iliopita, Marekani na Iran zilipigana katika maji hayohayo. Meli zilishambuliwa , na wafanyikazi wakauawa na wengine kujeruhiwa.
Kabla ya vita hivyo kuisha, ndege ya abiria ya Iran ilishambuliwa na kuanguka kwa bahati mbaya.
Je hayo yanaweza kutokea tena?
Vita vya meli za mafuta vilisababisha wasiwasi mkubwa wa kimataifa wakati wa vita vya miaka minane kati ya Iran na Sadam hussein wa Iraq.
Mataifa hayo mawili yalishambuliana visima vya mafuta wakati wa miaka ya katikati ya 80.
Na mara meli ambazo hazikuwa zikihusika zilianza kushambuliwa huku mataifa yakiendeleza shinikizo pande zote mbili. Meli za mafuta za Kuwait zilijipata katika hali mbaya.
Marekani chini ya uongozi wa rais Ronald Regan haikutaka kujihusisha.
Lakini hali iliokuwa ikiendelea katika Ghuba ilikua inaendelea kuwa hatari- ikithibitishwa wakati meli ya Marekani ya kivita , USS Stark iliposhambuliwa na kombora lililorushwa na ndege ya kivita ya Iraq -ijapokuwa maafisa wa Iraq baadaye walidai kwamba ilikuwa bahati mbaya.
Kufikia mwezi Julai 1987, meli za mafuta za Kuwait zilizosajiliwa upya , zikipeperusha bendera ya Marekani zilisindikizwa katika Ghuba na meli za kivita za Marekani.
Wakati huo ndio uliokua msafara mkubwa wa wanamaji tangu vita vya dunia vya pili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati huo kama sasa Marekani na Iran walikuwa katika mgogoro.
Kiongozi wa kidini nchini Iran Ayatollah Khomeini, alikuwa akiita Marekani 'shetani mkubwa' tangu mageuzi ya Iran ya 1979.
Washington ilikua bado ikiuguza pigo ililopata kufuatia kutekwa nyara kwa wanadiplomasia wake 52 mjini Tehran kwa siku 444 kutoka 1979 hadi 1981.
Na ijapokuwa Iran na Iraq ndio waliokuwa wakizozana, vita vya mashambulizi dhidi ya meli za mafuta vilikuwa mojawapo ya mgogoro wa muda mrefu kati ya Iran na Marekani.
Ni vita ambavyo havijaisha na ambavyo vimezuka upya kufuatia uamuzi wa rais Donald Trump kuweka shinikizo kali baada ya kujiondoa katika mkataba wa kinyuklia wa Iran wa 2015.
Kwa wakati mwengine tena maji ya mkondo wa bahari wa Hormuz yamekuwa eneo ambalo mgogoro huo unapiganiwa.
Je mambo yamebadilika?
Pande zote mbili zimepanua uwezo wao , kulingana na Dkt. Martin Navias , mwandishi wa kitabu cha vita vya meli za kubebea mafuta.
Iran anasema ina uwezo mkubwa wa kutumia mabomu ya kutegwa ardhini , manuwari na maboti yenye kasi kushambulia na kuharibu meli za kibiashara na hata zile za kivita.
Na sio tu vita baharini: Uwezo wa Iran wa kushambulia ndege za ujasusi za Marekani unaonyesha mwelekeo mpya wa vita hivyo.

Chanzo cha picha, EPA
Je Marekani na Iran zinaweza kushambuliana?
Iwapo mashambulizi dhidi ya meli za mafuta yataongezeka , tunaweza kuona tena meli za mafuta zikipeperusha bendera za Marekani na kusafirishwa na meli za kivita za taifa hilo katika mkondo wa Hormuz.
Mnamo tarehe 24 mwezi Julai 1987 , meli ya mafuta ya Kuwait iliokuwa ikipeperusha bendera ya Marekani ili kuilinda dhidi ya maadui iligonga bomu la ardhini la Iran katika msafara wa kwanza wa Marekani.
Marekani ilipeleka meli zaidi za kivita katika eneo hilo.
Pande hizo mbili sasa zinalumbana .
Mnamo mwezi Septemba, ndege za Marekani zilishambulia meli ya Iran baada ya kuiona ikitega mabomu usiku kucha.
Katika miezi iliofuatia, meli zaidi za mafuta na moja ya kivita ya Marekani zilishambuliwa.
Wanajeshi wa Marekani walijibu kwa mashambulizi makali, wakiharibu kambi za jeshi la Iran na kushambulia meli za Iran za kivita.
Vita hivyo vikaisha lakini baadaye kombora la Marekani kuiangusha ndege ya abiria ya Iran iliodhani kuwa ndege ya kivita na kuwaua abiri wote ndani yake.
Ripoti rasmi kuhusu kisa hicho inasema kuwa huenda uharibifu wa data ndio uliosababisha shambulio hilo.
Wanamaji wa Marekani waliwekeza pakubwa katika teknolojia na mafunzo ili kuzuia makosa kama hayo katika siku za usoni.
Lakini mchanganuzi wa jeshi la wanamaji katika taasisi ya kimkakati Nick Childs anasema kuwa mazingira ya sasa ambapo wapinzani wanatumiana cheche kali za maneno katiika mitandao ya kijamii inazua mazingira ya hofu.
Sekta ya habari imebadilika , anasema. Watu wanakuwa na hofu na kwamba kila upande unafikiria vibaya kuhusu mpinzani wake.
Donald Trump na Hassan Rouhani wote wanasema kuwa hawataki vita. Wale wenye misimamo mikali kutoka pande zote mbili wanaelewa mambo tofauti.
Mbali na vitisho vyote vilivyotokea 1987 na1988, ni meli chache za mafuta ambazo zilizamishwa huku uchukuzi wa meli katika mkondo wa bahari wa Hormuz ukiendelea bila tatizo lolote.
N sasa miaka 30 baadaye , Marekani haitegemei sana mashariki ya kati kwa mafuta . Iran ndio itakayoathirika pakubwa iwapo mkondo wa bahari wa Hormuz utafungwa.
Kwa sasa vita vya meli za mafuta sio rahisi kutokea lakini kwa kuwa pande zote mbili hazitaki vita sio kwamba vita haviwezi kutokea.
Mazingira yaliopo yanaweza kuzua lolote.
















