Zaidi ya nyangumi 100 wapo kizuizini nchini Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi imeanza kuwafungulia kundi la nyangumi 100 waliopo kizuizini kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Hatua hiyo inafuatia upinzani mkali uliopazwa na wanasayansi wa bahari na watu mashuhuri kutoka sehemu mbalimbali duniani juu ya kile kinachoitwa "jela za nyangumi".
Nyangumi hao wanashikiliwa katika vizimba vidogo vilivyotengenezwa kwenye Bahari ya Japani.
Wtaachiliwa kwa makundi, na kazi hiyo inatarajiwa kuchukua miezi kadhaa mpaka kukamilika.
"Tumechukua uamuzi huu wa busara baada ya kushauriwa na wanasayansi kuwaachilia wanyama hawa kurudi kwenye mazingira yao ya asili ambapo walikamatwa," amesema Naibu Waziri Mkuu wa Urusi Alexei Gordeyev siku ya Alhamisi.
"Operesheni hii itachukua kipindi cha miezi minne hivi mpaka kukamilika," amesema.
Nyangumi nane wataachiliwa kwenye hatua ya kwanza ya operesheni hiyo. Wwili wameshaachiliwa Alhamisi.
Rais Vladimir Putin amesifia hatua hiyo katika hotuba yake ya mwaka ambapo hupokea simu kutoka kwa raia na kujibu maswali yao.
"Nyangumi hao - kwa jinsi ninavyojua- wana thamani ya dola milioni 100," amesema. "Linapokuwa tatizo la pesa nyingi, utatuzi wake huwa mgumu. Nashukuru Mungu mambao yameanza kusonga."
Jela ya nyangumi ni kitu gani?
Nyangumi hao wenye umri mdogo walinaswa mwaka jana kwenye Bahari ya Okhotsk.
Walisafirishwa baada ya kunaswa kwa zaidi ya kilomita 1,300 kusini mpaka katika mji wa bandari wa Nakhodka ambapo wanashikiliwa.
Japo Urusi inaruhusu kunasa nyangumi kwa shughuli za kisayansi, watafiti wana mashaka kuwa wanyama hao walikuwa wauzwe kwenye majumba ya maonesho yaliyopo Uchina.
Nyangumi mmoja mmoja ambao hunaswa kwa njia haramu huuzwa kwa mamilioni ya dola.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kundi moja la wanaharakati wa mazingira nchini Urusi lilipaza sauti juu ya jela hiyo Oktoba mwaka jana.
Wanaharakati hao wanaamini nyangumi wanne wamekufa katika kizuizi hicho.
Inaaminika kuwa baadhi ya wanyama hao wamedhoofika kiafya.
Wakiwa katika mazingira yao ya asili, nyangumi huogelea makumi ya kilomita baharini - na hilo huwafanya miili yao kupata joto - lakini kizuizini huwa wabaridi, hali inayohatarisha maisha yao.
Akina nani wamepigania uhuru wa wanyama hao?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kashfa hiyo ya kuwafungia nyangumi hao iliwashtua watu wengi duniani, kuanzia wanasayansi mpaka waigizaji wakubwa wa filamu.
Nyota wa Hollywood alikuwa ni miongoni mwa watu milioni 1.5 waliosaini waraka unaotaka Urusi kuwaachilia wanyama hao.
Mwanamitindo na mtangazaji Pamela Anderson, alimuandikia barua rais Vladimir Putin, akimuomba kuwaachilia wanyama hao.
Mwanzoni mwa mwezi huu moja ya kampuni ilizonasa nyangumi hao ilitozwa faini ya dola 433,000 kwa kuvunja sheria.














