Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wapenzi wa jinsia moja waliotoroka kambi ya wakimbizi Kakuma warudishwa
Kundi la wakimbizi walio wapenzi wa jinsia moja waliotoroks katika kambi ya wakimbizi kaskazini magharibi mwa Kenya baada ya kulengwa katika kwa mahusiano yao ya jinsia moja, wanasafirishwa kutoka mji mkuu Nairobi kurudishwa katika kambi hiyo.
Umoja wa mataifa umeahidi kuwalinda wakiwa katika kambi.
Kundi hilo la wanaume, wanawake na watoto 76 wamekuwa wakiishi katika nyumba ndogo mjini Nairobi.
Hapo jana Jumatano jioni, waliagizwa wafungashe vitu vyao kwa safari ya kilomita 740 kurudi katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma.
Mwishoni mwa mwaka jana, maafisa nchini Kenya wanaoisimamia kambi ya kakuma wamesema hawawezi tena kulinda wakimbizi walio wapenzi wa jinsia moja.
Wakimbizi hao walisema walinyanyaswa kimwili katika kambi.
Watu wengi katika kundi hilo waliondoka Kakuma na kuelekea Nairobi mnamo Aprili mwaka huu. Lakini walisakwa na kutimuliwa kutoka sehemu ya kwanza walikoshukia, punde majirani walipotambua kuhusu mahusiano yao ya jinsia moja.
Baada ya hapo walielekea katika nyumba moja ndogo mjini humo na maafisa wa polisi waliojihami walijikita nje kuwalinda.
Mmoja katika kundi hilo aliiambia BBC kwamba kila wanakokwenda wanashambuliwa kwa mahusiano yao.
Ameliomba shirika la Umoja wa mataifa la wakimbizi liwalinde.
Umoja wa mataifa waahidi kuwalinda wapenzi wa jinsia moja Kakuma
Shirika la UNHCR limesema kuwa mipango maalum itawekwa kuhakikisha usalama wa wakimbizi hao.
Shirika hilo la Umoja wa mataifa linasema "litatoa ulinzi" kwa kundi hilo la wakimbizi wapenzi wa jinsia moja wanaorudishwa Kakuma.
Katika taarifa yake UNHCR linasema "baada ya kuwasili, [wakimbizi hao] watakutana na vikosi vya ulinzi vya UNHCR Kakuma.
"Kila mkimbizi atapewa ushauri nasaha na usalama wao utakaguliwa na hatua sahihi zitachukuliwa kwa kila mmoja wao.
"Mipango maalum itafanywa kwa wakimbizi walio na mahitaji maalum na walio katika hatari fulani, wakiwemo wale wanaotambulika kuwa wapenzi wa jinsia moja."
Kuna wakimbizi milioni 70.8 kote duniani kwa mujibu wa UNHCR - wanaotoroka vita, ghasia au mizozo.