Afrika Kusini: Mtoto wa miaka miwili auawa na chui katika mbuga ya wanyama ya Kruger

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtoto wa miaka miwili ameuawa na chui katika mbuga ya kitaifa ya Kruger nchini Afrika Kusini
Chui huyo alifanikiwa kupenyeza katika uzio wa waya uliyotenganisha eneo la mbuga hiyo na maeneo mengine na kumvamia mtoto huyo ambaye ni wa mmoja wa wafanyikazi na kumjeruhi vibaya.
Familia ya mtoto huyo ilimkimbiza hospitali lakini ilifahamishwa tayari alikuwa amefariki walipofika.
Tarifa ya mbuga hiyo imesema kuwa shambuli kama hilo huwa "nadra sana", lakini walinzi walimuua chui huyo ili "kumuokoa mtoto".
Ike Phaahla, msemaji wa mbuga hiyo, alisema chanzo halisi cha kifo cha mtoto huyo bado kinautata.
Alisema kwamba wanyama huogopa binadamu na kwamba hawawakaribii.
"Katika mbuga kama ya Kruger wanyama hawatangamana na watalii na wafanyikazi haliambayo huenda wanyama kama chui kuwazoea watu na kutowaogopa," Bw. Phaahla alisema.
Alisema kuwa wageni wanaozuru mbuga hiyo hufuata muongozo maalum kuhakikisha wanajilinda dhidi ya wanyama, kama vile kufunga milango kama wanasafiri kama kikundi, na kuongeza kuwa chui lazima awe "mkakamavu sana" kumshambulia mtu mzima lakini huenda akafanya hivyo "akimpata mtoto wa miaka kati ya miwili na sita".

Chanzo cha picha, Getty Images
Bw. Ike Phaahla pia alisema wageni na wafanyikazi katika mbuga hiyo humepewa ulinzi wa kutosha dhidi ya wanyama kwa kuwekewa uzio imara lakini nyakati zingine wanyama huwafikia kiajabu.
"Lazima tukubali kuwa hawa ni wanyama pori," alisema.
Afisa mkuu mtendakaji wa mbuga za kitaifa za wanyama nchini Afrika Kusini , Fundisile Mketeni ametuma rsala za rambi rambi kwa familia ya mtoto huyo.
"Hii ndio hatari inayotukabili kila siku tunapojaribu kuhifadhi wanyama hawa kwa maslahi ya wote ," alisema.













