Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kamanda wa Polisi Dodoma ameonya waandamanaji wangepigwa mpaka kuchakaa
Chama cha upinzani nchini Tanzania cha ACT-Wazalendo kimetangaza kuahirisha maandamano yaliyopangwa kufanyika Dodoma hii leo.
Maandamano hayo ambayo yalikuwa yanaratibiwa na jumuiya ya vijana ya chama hicho.
Lengo la maandamano hayo ni kushinikiza Bunge la Tanzania kufuta azimio lake la kutokufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa nchi hiyo, Prof Mussa Assad.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma ambapo ndipo Bunge la Tanzania hukaa, Gilles Muroto jana alionya hatua kali zingechukuliwa kwa yeyote abaye angeingia mtaani na kuandamana.
'Wale wote waliopanga kufanya maandamano mnamo Aprili 9, 2019 wasije kuingia barabarani maana watapigwa na kuchakaa," alitahadharisha Muroto.
Awali ACT walipinga vikali kauli hiyo na kutaka "ikemewe na kila Mtanzania maana ni kauli ya vitisho dhidi ya haki za kikatiba."
Pili vijana hao wakandelea kushikili msimamo wao wa kuendelea na maandamano: "Maandamano yapo kama yalivyopangwa na yanafanyika kwa mujibu wa katiba na wajibu wa polisi ni kuyalinda na si kuyazuia au kuwatisha wananchi, wasitekeleza wajibu wao."
Hata hivyo, baadae usiku kupitia ukurasa wao wa mtandao wa twitter, umoja huo wa vijana ulitangaza kuahirisha kwa muda maandamano hayo wakinukuu barua ya polisi kutoka kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya Dodoma, M.J Makanja.
Katika barua hiyo, polisi wametoa sababu tano za kuzuia maandamano hayo ikiwemo za kisheria. Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, maandamano kama hayo yanabidi yaripotiwe saa 48 kablahuku barua ya ACT ikiwafikia polisi saa 22 kabla ya siku tukio.
Pia imewataka ACT na vyama vingine vya upinzani vyenye uwakilishi bungeni kuhoji na kukosoa juu ya suala hilo la CAG ndani ya bunge na si vinginevyo.
"Ngome ya vijana imeazimia kuyasogeza mbele maandamano haya na kushughulikia hoja namba mbili iliyotolewa kwenye barua ya polisi (kuhoji bungeni) kisha kuyarudisha tena maandamano haya katika siku za usoni hasa endapo tarifa ya CAG haitajadiliwa Bungeni na pia bunge kuondoaazimio lake la kutofanya kazi na CAG," sehemu ya taarifa ya chama hicho imeeleza.
Mzozo wa Bunge na CAG
Mnamo tarehe mbili mwezi huu, Bunge la Tanzania liliazimia kutofanya kazi na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali, (CAG) wa nchi hiyo Prof Musa Assad baada ya kumtia hatiani kwa tuhuma za dharau kwa chombo hicho.
Wabunge waliafikia uamuzi huo baada ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutaka waridhie mapendekezo yao dhidi ya CAG.
Kamati hiyo ilimhoji CAG Januari 21 baada ya kufanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York mwezi Disemba 2018 ambapo alisema kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.
Marufuku ya mikutano na maandamano
Mara baada tu ya kuingia Ikulu ya Magogoni, Rais John Magufuli aliweka wazi msimamo wake kuwa hatopenda kuwaona wanasiasa wakizunguka nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara.
Hoja yake kubwa ni kuwa "watu waachwe wafanye kazi na kulijenga taifa" na wanasiasa wasubirie kampeni za Uchaguzi wa 2020 ili kuzunguka nchi kujinadi. Marufuku hiyo pia imejumuisha maandamano na migomo dhidi ya serikali
Vyama vya Upinzani na wanaharakati wa haki za binaadamu kama ilivyotarajiwa walipinga vikali katazo hilo.
Chama kikuu cha upinzani cha Chadema kilitangaza operesheni ya kupinga kile walichokiita Udikteta Tanzania (UKUTA) na kudhamiria kufanya maandamano ya nchi nzima mwaka 2016, lakini waliisitisha kabla ya kuanza.
Mwaka 2018, mwanaharakati Mtanzania anayeishi Marekani, Bi Mange Kimambi aliitisha maandamano makubwa ya nchi nzima ambayo yalikuwa yafanyike Aprili 26, 2018.
Mjini Dodoma kamanda Muroto alitahadharisha kuwa wanaotaka kuandamana kuwa "watapata tabu sana" na wangepokea "kipigo cha mbwa koko".
Maandamano hayo hayakufanyika nchini Tanzania.
Baadhi ya Watanzania wanaoishi ughaibuni waliandamana katika balozi za nchi hiyo.