Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ofwono Opondo: Uganda ni salama kushinda Marekani
Msemaji wa serikali ya Uganda amesema kuwa rais wa Marekani anafaa kutatua matatizo ya taifa lake badala ya kuingilia maswala ya Uganda.
Ofwono Opondo alikuwa akijibu chapisho la mtandao wa Twitter kutoka kwa rais Donald Trump ambalo linasema kuwa watu hawatatamani kwenda Uganda hadi pale watekaji nyara wa raia wa Marekani pamoja na mwongozaji wake watakapokamatwa.
Wawili hao waliachiliwa siku ya Jumapili.
Bwana Opondo alijibu kupitia mtandao wa Twitter akisema kuwa kuna vifo vingi vya bunduki nchini Marekani zaidi ya utekaji nyara nchini Uganda.
Aliongezea kuwa Uganda itaendelea kuimarisha usalama wake.
Kufuatia utekaji nyara wa wawili hao rais Trump alisema kuwa utekaji nyara huo huenda ukaathiri utalii nchini Uganda akiongezea kuwa watekaji hao ni sharti wakamatwe kabla ya watalii kuzuru taifa hilo.
Awali rais Musevei alikuwa ametuma ujumbe wa Twitter akisema kuwa taifa lake liko salama kwa raia wa Uganda na watalii.
Aliwalaumu wahalifu wachache kwa visa kama hivyo .
Je kikombozi kilitolewa?
Wawili hao walitekwa wakati walipokua wakitembea katika mbuga ya Malkia Elizabeth jioni ya tarehe 2 Aprili.
Maafisa wa polisi nchini Uganda walisema kuwa watekaji hao walitumia simu moja kuitisha $500,000 (£383,435) kama kikombozi.
Hatahivyo haijulikani iwapo walilipwa.
Operesheni ya kuwatafuta
Operesheni ya pamoja ya usakaji iliofanywa na wanajeshi, mamlaka ya wanya pori Uganda na kitengo cha polisi wa Utalii ilianzishwa ili kumuokoa bi Endicott na bwana Mirenge.
Lakini msemaji wa serikali alituma ujumbe wa Twitter kwamba waliokolewa na vikosi vya serikali ya Uganda nchini DRC na kwamba walikuwa salama salmin katika mpaka wa DRC na Uganda.
Chombo cha habari cha France-Presse hatahivyo kiliinukuu kampuni ya Frontiers Safaris- ikisema kuwa wawili hao waliachiliwa baada ya kikombozi kulipwa watekaji hao.
Baada ya utekaji huo maafisa wa polisi walikuwa wamesema kuwa kundi moja la watu wanne waliokuwa wamejihami kwa bunduki waliwakamata watalii hao na kuwateka wawili wao kabla ya kutoweka nao.
Watalii wengine waliodaiwa kuwa wanandoa wawili waliokolewa baadaye.