Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mahakamani: Maafisa 2 wakuu wa FDLR washtakiwa kwa kosa la kutekeleza ugaidi Rwanda
- Author, Ripota wa BBC
- Nafasi, Yves Bucyana
- Muda wa kusoma: Dakika 2
Maafisa wakuu wawili wa kundi la waasi la FDLR linalopinga utawala wa Rwanda wamefikishwa mahakamani mjini Kigali kwa mara ya kwanza na kushtakiwa makosa ya ugaidi miongoni mwa mashtaka mengine.
Maafisa hao ni aliyekuwa msemaji wa kundi hilo La Forge Fils Bazeyi na Kanali Nsekanabo Jean Pierre aliyekuwa afisa wa kijasusi wa kundi hilo.
Kwa muda sasa Serikali ya Rwanda imekuwa ikiwahoji na kusema walitoa taarifa muhimu kuhusu mpango wa Uganda wa kusaidia makundi ya waasi kuangusha utawala wa Rwanda. Yves Bucyana.
Mwendeshamashtaka ameiambia mahakama kwamba aliyekuwa msemaji wa FDLR Nkaka Ignace maarufu La Forge Fils Bazeyi na Kanali Nsekanabo Jean Pierre maarufu Abega walishiriki mkutano mjini Kampala mwishoni mwa mwezi wa kwanza mwaka huu uliokuwa na lengo la kusuka mpango wa kuishambulia Rwanda.
Amesema mkutano huo uliandaliwa na utawala wa Uganda ambapo pia ulishirikisha wajumbe wa kundi la RNC ambalo pia linapinga utawala wa Rwanda, la waasi dhidi ya Rwanda.
Kundi la RNC linaongozwa na jenerali Kayumba Nyamwasa aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Rwanda na ambaye anaishi uhamishoni nchini Afrika kusini.
Aidha wameshitakiwa kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kuipaka matope Rwanda dhidi ya jumuiya ya kimataifa.
Wao hawajapewa nafasi ya kutoa hoja zao mahakamani.
Maafisa hao wa zamani wa kundi la FDLR walikamatwa mwishoni mwa mwaka jana kwenye mpaka baina ya Uganda na Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo.
Nchi ya Congo ilisema kwamba walikuwa wametokea mjini Kampala na kuingia Congo kinyume cha sheria.
Baadae walikabidhiwa Rwanda kisirisiri.
Viongozi wa Rwanda walitangaza kwamba maafisa hao walihojiwa vya kutosha na ngazi za upelelezi na kutoa taarifa muhimu kuhusu mkutano huo wa mjini Kampala baina ya makundi ya waasi kuweka mipango sawa kwa lengo la kuishambulia Rwanda.