Ethiopian Airlines: Baadhi ya mataifa yamesitisha utumizi wa ndege za Boeing 737 Max baada ya ajali ya Ethiopia

Chanzo cha picha, JONATHAN DRUION
Siku moja baada ya ajali ya shirika la ndege ya Ethiopia kuanguka, maswali mengi yameibuka kuhusu usalama wa ndege aina ya Boeing 737 Max ambayo ni ya pili ya aina hiyo kuanguka katika miezi mitano.
Mwaka 2017 Boeing iliuza ndege 763, idadi ambayo imetajwa kuwa ya juu zaidi kuuzwa ndani ya mwaka mmoja.
69% ya ndege hizo ilihusisha uuzaji wa kwanza wa ndege mpya aina ya Boeing 737 MAX ambazo ziliwasilishwa kwa mashirika 17 tofauti ya ndege duniani.
Ndege zote za 737 MAX zilizouzwa zinaweza kutambuliwa kupitia nambari maalum 'B38M'.
Mauzo ya kampuni ya kuunda ndege ya Boeing ilipanda kwa 31% mwaka huu.
Kampuni hiyo ilipata faida ya zaidi ya dola bilioni $100 kwa mara ya kwanza katika historia yake ya miaka 102 baada ya kuongeza uuzaji wa ndege za kibiashara na za kijeshi.
Licha ya ufanisi huo wa kibiashara kampuni ya Boeing imejipata katika njia panda hasa baada ya ajali ya ndege zake mbili zilizopata ajali chini ya miezi mitano.

Chanzo cha picha, Reuters
'Ni pigo kubwa kwa bara letu la Afrika na wenzetu wa Ethiopia wamepata madhara makubwa baada ya kupoteza chombo na watu', anasema, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania, Ladislaus Matindi.
Akizungumza na BBC bwana Matindi alisema kihistoria Bara la Afrika limeonesha mabadiliko makubwa katika bishara ya usafiri wa ndege kwasababu idadi ya ajali ya ndege imepungua pakubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma.
''Ukiangalia ajali na jinsi unavyofanya biashara kuna husiano mkubwa sana'', alisema.
Bwana Matindi, aliongeza kuwa sehemu ambazo zinaripoti ajali nyingi za ndege huathiri biashara ya usafiri wa anga.

Chanzo cha picha, Reuters
Kufikia mwaka 2015 takwimu za usafiri wa anga Barani Afrika zilionesha thulithi mbili za ajali mbaya zilikuwa zikitokea barani humo lakini.
''Wakati huo biashara ambayo tulikuwa tukifanya alikuwa 3% pekee duniani kwasababu tulikuwa hatuaminiki'', anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania,Ladislaus Matindi.
Hali hiyo hata hivyo imebadilika tangu mwaka 2016 kwasababu hakuna ajali mbaya iliyoripotiwa.
Bwana Matinda amesema kila ajali ya ndege hutoa nafasi kwa wataalamu wa usafiri wa anga kuboresha huduma za usafiri huo ili kuzuia ajali isitokee tena.














