'Hatutishwi na uamuzi wa Facebook'

Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison amesema kuwa serikali yake haitishwi na kitendo cha Facebook kuzuia kupatikana kwa habari nchini humo.
Kampuni ya Facebook imezuia watumiaji wake nchini Australia kuchapisha au kutazama habari katika jukwaaa hilo jambo lililozua wasiwasi mkubwa miongoni mwa watumiaji wa mtandao huo wa kijamii kuhusu namna watakavyopata habari muhimu na kuchangamana pia.
Wale walio nje ya Australia pia hawawezi kusoma au kupata machapisho yoyote ya habari ya Australia kwenye jukwaa hilo la facebook.
Aidha kampuni ya facebook imechukua hatua hiyo baada ya kuwepo sheria ambayo nchi hiyo inapanga kuwatoza pesa wafanyabiashara wanaochapisha habari kwenye jukwaa hilo.
Aidha kampuni kama Google na Facebook wamesema sheria hiyo haielezi wazi jinsi mtandao huo utakavyofanya kazi na hivyo umelenga kuwaadhibu tu.
Lakini serikali ya Australia imesema kuwa inaendelea na sheria hiyo, ambayo ilipitishwa na baraza la bunge siku ya Jumatano.
Waziri wa habari nchini humo Paul Fletcher ameiambia BBC kuwa kampuni hiyo inahitaji kufikiria kwa uangalifu kuhusu hatua walioichukua.












