Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania: Mwalimu aliyemchapa mwanafunzi Sperius hadi kifo ahukumiwa kunyongwa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba imemhukumu Mwalimu Respicius Mutazangira Adhabu ya Kunyongwa hadi kufa baada ya Kumkuta na hatia ya Kumpiga na Kumuua mwanafunzi Sperius Eradius Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kibeta.
Mtazangira amehukumiwa leo tarehe 6 Machi 2019 huku Mahakama hiyo ikimuachia huru aliyekuwa mshtakiwa mwenza katika kesi ya mauaji ya kukusudia, Mwalimu Herieth Gerald.
Kesi hiyo ilifunguliwa mwishoni mwa mwaka jana na kusikilizwa na Jaji Lameck Mlacha ambaye leo alisoma hukumu ya kesi hiyo.
Walimu hao walishitakiwa kwa kumuua kwa kukusudia Sperius Eradius aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo mwishoni mwa mwaka 2018.
Upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi tisa katika kesi hiyo iliyosikilizwa kwa mwezi mmoja na Jaji Lameck Mlacha, ilianza Februari 6, 2019.
Inadaiwa walimu hao walitenda kosa la kumuadhibu kwa kipigo mwanafunzi Sperius Eradius kwa madai kuwa aliiba mkoba wa mwalimu ukiwa na fedha.
Tukio hilo lilitokea tarehe 27 Agosti 2018, ambapo marehemu Sperius aliyekuwa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibeta (14) alipigwa na mwalimu Mtazangira akituhumiwa kuiba pochi ya mwalimu Herieth.
Mazingira ya kuibiwa kwa mkoba
Baadhi ya wanafunzi walisimulia tukio hilo kuwa wakati mwalimu wao wa nidhamu alipofika shuleni, kuna wanafunzi ambao walimpokea mizigo yake wakati aliposhuka na bodaboda.
Lakini baada ya mwalimu huyo kuingia ofisini kwake alibaini kuwa hauoni mkoba wake na kuanza kuuliza kila mwanafunzi na kutangaza upotevu huo katika mkusanyiko wa wanafunzi wote.
Baadae mwalimu huyo akamuhoji marehemu kwa kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na tabia ya kupokea walimu mzigo yao mara kwa mara na alipoulizwa akakana ndipo akaanza kupigwa viboko.
Dereva wa bodaboda badae alirudi na kusema mwalimu alisahau mkoba katika pikipiki wakati mtoto ameshazimia.