Je hatua ya serikali ya rais Magufuli kubaini hifadhi za akiba kutatatua uvamizi wa ardhi Tanzania?

Tanzania inapanga kutathmini upya mipaka ya hifadhi na mbuga zake za wanyama pori na misitu katika kukabiliana na ongezeko la matumizi ya radhi.

Rais John Magufuli ameagiza kusitishwa kwa mpango wa kuwatimua wakaazi wa vijiji vilivyopo kwenye hifadhi za wanyama pori na misitu.

Wizara husika zimetakiwa kutambua na kubaini hifadhi zote na misitu ambazo hazina wanyama pori zitakazoweza kugawanya kwa wakulima na wafugaji ambao wameweka makaazi katika baadhi ya hifadhi nchini.

Hatua hiyo imenuiwa kukabiliana na kuongezeka kwa matumizi ya ardhi hususan kwa jamii za wafugaji na wakulima waliojikita katika maeneo hayo ya hifadhi za wanyama pori.

Taarifa zilizopo ni kwamba wizara zote husika zinapaswa kutekeleza agizo hilo pasi kuchelewa.

Jamii tofuati kama ya Wamaasai ambao ni wafugaji, na pia ni wanaohama hama katika kutafutia mifugo yao malisho ni sehemu ya watu wanaoishia kuishi katika hifadhi za wanyama pori.

Mwandishi, mkaazi mjini Arusha, Jane Edward ambaye amekuwa akifuatilia taarifa hii ameieleza BBC kwamba Ngorongoro ni mojawapo ya hifadhi Tanzania ambapo binaadamu wanaishi katika makaazi ya wanyama kwa muda mrefu.

Ameeleza kwamba hilo ni mojawapo ya kivutio kikubwa kinachoitambulisha hifadhi hiyo.

Jamii ya Wamasaai, anasema baadhi wanaishi ndani ya hifadhi hiyo na wengine anaeleza wanapatikana pembezoni mwa wilaya ya Ngorongoro, kwa maana ya Karatu na sehemu nyingine za jirani.

Utamaduni na hali ya maisha kwa jamii za kuhama hama

Ni jambo la kawaida linaloambatana na utamaduni na hulka ya wamaasai kuwa na ujasiri, na katika utamaduni wa jamii hiyo pia tangu wanapokua Morani au vijana, wanafundishwa kuwa na ujasiri ikwemo pia kuishi na wanyama.

Ni sehemu ya ukuaji ambako vijana wanapokuwa wanapelekwa jandoni wanapewa mafunzo hayo ya kuwa na ujasiri kama sehemu ya kijana kukuwa na kuingia katika utu uzima.

Na Jane anasema huenda ndio moja ya sababu kwanini wanaishi ndani ya hifadhi hiyo, na kwa muda imeonekana vigumu kuwatimua kwasababu ni wenyeji na wafugaji wanaoishi kwa kuhama hama, na pia ndio sababu wako hadi leo.

Lakini je hilo ni suluhu?

Wanaharakati wa mazingira wameeleza wasiwasi wao kuhusu operesheni hiyo ya awali ya kuwatimua wakaazi ambayo sasa imesitishwa.

Emmanuel Mtiti mtaalamu wa masuala ya uhifadhi mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kutoka nchini Tanzania, anaeleza kuwa agizo hilo lililandamwa kwa hali ya kukinzana.

'Anayesajili vijiji ni nani? ni serikali, aliyetengeza hifadhi ni nani? ni serikali, kwanini mtu mmoja anafanya mambo mawili yanayokinzana?' anauliza Mtiti.

Baadhi wanaona huenda hatua hii sasa ya serikali isiwe suluhu, kwa maana jamii zinazozungumziwa ni jamii kama hizo za kuhama hama ambazo sio tu wafugaji lakini pia wakulima.

Mtiti anasema, Hata iwapo serikali itawatengea sehemu au kuamua kuwaacha sehemu waliopo hivi sasa, baada ya muda mfupi jamii hizi hazitakuwepo kutokana na hulka yao hiyo ya kuhama hama.

Ametaja mifano ya jamii zilizopo maeneo ya kaskazini mwa Tanzania, ambazo baadhi ya mashirika na taasisi zilidhani kwamba baada ya kuhamia maeneo hayo, ndio zimefika na ni sehemu ambazo wanaweza kuishi.

'Miradi tofuati ya maendeleo imeidhinishwa ikiwemo ujenzi wa shule, na baada ya muda wakaondoka na shule hizo zikasalia porini' amesema Mtiti.

Kilicho muhimu anashauri, ni kujifunza kwa undani ni nini kinacho zisababisha jamii hizo kuhama? na ni kipi hasaa kinachohitajika ili waweze kukaa mahali pamoja.

Kadhalika ameeleza kwamba kuna umuhimu wa kuzielewesha jamii hizo na kuzifanya zikae katika maeneo ambayo yataleta madhara kidogo kwa misitu na wanyama pori, yatakayoweza kuendelea kuwepo katika maeneo mengine.