Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siasa za Tanzania: Je, Azimio la Zanzibar litachagiza chaguzi za 2019 na 2020?
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania walikutana mwishoni mwa mwaka 2018 visiwani Zanzibar kwa mwaliko wa mwanasiasa mkongwe Maalim Seif Sharrif Hamad.
Vyama vya ACT-Wazalendo, CUF, UMD, NLD, Chadema, TLP, NCCR-Mageuzi na Chauma vilijadili na kupitisha makubaliano yaliyobatizwa jina la Azimio la Zanzibar.
Azimio hilo la mwaka 2018 limebebwa na kauli mbiu ya 'kurudisha demokrasia' ambayo inadaiwa kuminywa kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.
Si lengo la makala haya kueleza makubaliano yaliyofikiwa bali kuchambua kile ninachoona namna gani vyama hivi vinatakiwa kusonga mbele baada ya makubaliano hayo.
Inakubalika kuwa ushirikiano miongoni mwa vyama katika siasa za ushindani.
Ni njia mojawpao ya kujenga demokrasia na mshikamano miongoni mwa viongozi,wafuasi na wanachama.
Mazingira ya siasa
Chama cha siasa kinatakiwa kukumbushwa na kujikumbusha kuwa haki yake kisiasa ndio matunda ya ushiriki wa wanachama wake katika sekta hiyo.
Chama cha siasa kinatakiwa kukumbushwa kuwa hata siku moja bakuli la uji likiwa mezani haliendi mdomoni pasipo kutumia mkono kuinyanyua au mkono kutumia kijiko kunywa uji huo.
Kwamba vyama vya siasa vifahamu kuwa katika mazingira ya utawala huu visitegemee kuletewa haki mlangoni kama mgeni mtoka mbali.
Vyama vyetu vya siasa vinatakiwa kuwa na msingi wa hekaheka katika kutafuta haki zao kisiasa na wananchi kushiriki siasa kwa uhuru.
Mwaka 2019 unaelekea kuwa wa hekaheka za kutafuta haki ya kidemokrasia katika kila eneo ambalo limefifishwa au haki zake kudhoofishwa.
Kwa sababu haijawahi kutokea kokote duniani kuwa serikali iliyopo madarakani ikashindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi wake kwa sababu ya kuwepo kwa mikutano ya hadhara.
Rais wa nchi yoyote hashindwi kuzindua mradi kwa sababu nchi yake inafanya mikutano ya hadhara ya kisiasa. Chama kinachotawala katika nchi Tanzania hakishindwi kutekeleza ilani yake kwa sababu vyama 15 vya Tanzania vitakuwa vinafanya mikutano ya hadhara au ndani pamoja na wanachama wake.
Mikutano ya hadhara ni sehemu ya kuwakutanisha wananchi na kuwaelimisha elimu ya uraia,haki na wajibu wao kwa nchi na binafsi. Ni sehemu ya kuwapa maarifa juu ya siasa kuwa ni maisha,elimu,uchumi, utamaduni, michezo na burudani.
Siasa hugusa karibu kila kitu hata kupanda kwa bei ya bidhaa sokoni. Kwahiyo siasa hii inatakiwa kuzalishwa kupitia mikutano ya hadhara.
Ikumbukwe mikutano ya ni sehemu ambayo wananchi wanatumia kusikiliza na kujifunza juu ya sera na kufanya maamuzi ya kuunga mkono chama chochote, kutambua wajibu, kupata elimu ya uraia na kadhalika.
Ndiyo kusema, azimio la Zanzibar kama sehemu ya ukuzaji wa demokrasia ni muhimu sana kuhakikisha mikutano ya hadhara inakuwa katika mipango yao ya kuzungumza na wananchi pamoja na kuwa sehemu ya kutafiti masuala ya haki, sheria na maendeleo.
Nadharia
Kama ni kweli wamedhamiria kutekeleza mipango yao kisiasa kwa kufanya mikutano bila woga basi wanapaswa kufahamu kuwa wanasiasa thabiti husimamia hoja zao na hawatetereki kwa sababu wameambiwa "watafanywa hivi au vile".
Kwanini? Hakuna nadharia yoyote inayosema kuwa mikutano ya hadhara ni chanzo cha nchi kuwa na maendeleo duni.
Hakuna nadharia yoyote inayosema kuwa mikutano ya hadhara ni chanzo cha kuchelewesha miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Hakuna nadharia inayokubali kuwa mikutano ya hadhara ni chanzo cha umasikini wa wananchi.
Kwa kipindi cha miaka 24 ya uongozi wa Mwalimu Nyerere hapakuwa na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, je umasikini wetu ulipungua au kuongezeka?
Pamoja na kutokuwapo kwa mikutano ya hadhara (kwa sababu hapakuwa na vyama vya upinzani baada ya kufutwa) bado hatujaondoka kwenye lindi la umasikini mbali ya hatua zetu kama taifa tulizozifikia. Umasikini sio sifa ya uzalendo.
Msingi mkuu ni kwamba vyama vyote 15 vinatambua haki ya kulilinda taifa la Tanzania. Vinatambua kuwa kuharibika kwa taifa hili ni hasara kwa watanzania na watunza nia ya amani.
Ili kuwe na amani ni muhimu kuwa huru kimawazo na ushirikiano.
Ili mtanzania awe mzalendo ni muhimu kuhakikisha anapata mahitaji yote ikiwemo 'kupumua' (kukutanika na kuzungumza na wengine kwenye mikutano ya hadhara).
Ni mwaka wa hekaheka?
Tafsiri tunayopata ni kwamba vyama vya upinzani nchini vinataka kuufanya mwaka 2019 kuwa wa hekaheka za kisiasa.
Mwaka huu kutafanyika chaguzi za serikali za mitaa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Vilevile vyama vya upinzani vinaweza kuufanya kuwa mwaka wa hekaheka za kisheria kutafsiri sheria mbalimbali ili wapate haki zao.
Kushindwa kesi ni sehemu ya mchakato, lakini kufungua kesi ni njia mojawapo ya kushiriki siasa halali.
Viongozi na wanachama wa vyama wanatakiwa kutumia fursa ya mahakama zilizopo kufafanua sheria katika maeneo mbalimbali; kuhusu dhamana, kesi za kisiasa, kuzuiwa mikutano ya hadhara kwa kisingizio cha intelijensia,udhalilishaji wa wafuasi na wanachama wao,mamlaka za wakuu wa wilaya na mikoa katika kuadhibu watumishi wa umma na raia wengine pamoja na viongozi na sheria za kuwaweka ndani kwa saa 48.
Inawezekana ukawa mwaka hekaheka za kisiasa. Ni mwaka ambao utakuwa unawaweka kwenye mizani ya kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2020.
Hekaheka za madai mbalimbali ya kisiasa, sheria na haki vinaweza kuwa vitu vitakavyotengeneza taswira ya upinzani.
Intelijensia: tafakuri ya pamoja
Mikutano mingi ya vyama vya siasa nchini iwe ndani au hadhara imekuwa ikizuiwa. Kuna mikutano ya ndani ya vyama vya siasa ambayo ni kama vile vikao vya taasisi zozote zile za kitaaluma, siasa na kadhalika.
Chama cha siasa ni taasisi, na kinatakiwa kuheshimiwa kwa uTaasisi wake.
Mara kadhaa vyama vinazuiwa kufanya mikutano kwa sababu zinazoitwa za Kiintelijensia; je kama wenye mamlaka wamebaini hilo, wanatumia mbinu gani kuzuia?
Intelijensia ni pamoja na kuhakikisha inaondoa matishio yote na kuwapa nafasi za kufanya mikutano ya kuzungumza na wafuasi na wanachama wao.
Ni muhimu kwa vyama kutorudi nyuma au kukaa chini na kulalamika, badala yake vinatakiwa kuchukua hatua juu ya hiki kitu 'Intelijensia', na kukifikisha kwenye vyombo vya sheria.
Ni muhimu Mahakama ikatakiwa kufafanua 'Intelijensia ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa' inavyochukuliwa na wajibu wa wanaohofia 'taarifa za kiintelijensia' katika kuzuia madhara.
La pili, ni vile vyama vya siasa vinavyokubaliana na 'intelijensia' hii kama sehemu ya kufifisha aria yao.