Uchaguzi DRC: Mgombea wa upinzani Martin Fayulu amepinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani

Maafisa wa usalama DRC

Chanzo cha picha, EPA

Muungano wa maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, umetoa wito wa kuundwa kwa serikali ya muungano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mzozo uliokumba matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi uliyopita.

Tangazo hilo limetolewa kupitia taarifa ya rais wa Zambia Edgar Lungu.

Afrika Kusini pia inaunga mkono wazo la kubuniwa kwa serikali ya muungano.

Hatua hii ya SADC inakuja siku moja baada ya mgombea wa upinzani katika uchaguzi mkuu uliyofanyika nchini Jamhuri ya kidemocrasia ya Congo amewasilisha kesi katika mahakama ya katiba kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Martin Fayulu amesisitiza kuwa alishinda uchaguzi huo lakini tume ya uchaguzi ikamtangaza mshindani wake Felix Tshisekedi kuwa mshindi.

Rais wa Zambia, Edgar Lungu, amesema kuwa wamezingatia "mvutano mkali uliyoibuka" kupinga matokeo ya awali.

Martin Fayulu (wa pili kutoka kulia) akiwa mahakamani siku ya Jumamosi

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Martin Fayulu (wa pili kutoka kulia) akiwa mahakamani siku ya Jumamosi

Amesema viongozi wa kikanda wanaonelea njia mwafaka ya kusuluhisha mzozo huo ni kupitia muafaka wa kisiasa ambao utatoa nafasi ya kuundwa kwa serikali ya muungano wa kitaifa.

Bwana Lungu alitoa mfano wa mwafaka wa kisiasa uliopatikana nchini Zimbabwe na Kenya.

Waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini,Lindiwe Sisulu, anapendekeza mchakato wa kisheria ufuatwe DRC kuhusiana na suala hilo huku akitoa wito kuwa watu wa nje wasiwalazimishe Wacongo jambo ambalo hawajaridhia.

Felix Tshisekedi, akiwa na mkewe, jamaa na maafisa wa UDPS (Union for Democracy and Social Progress) baada ya kutangazwa mshindi10 Januari, 2019 (Photo by Caroline Thirion / AFP) (Photo credit should read CAROLINE THIRION/AFP/Getty Images)

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Hata hivyo amesema bwana Sisulu, amesema kuwa serikali ya muungano wa kitaifa huenda ikawa ndio suluhisho kwa mzozo wa kisiasa unaokumba taifa hilo la kanda ya maziwa makuu ambayo inahitaji kupata amani ya kudumu

Pendekezo la SADC tayari limeanza kuvutia hisia mseto.

Baadhi ya watu wanahoji kuwa mtindo huu wa kumaliza mzozo unahujumu demokrasia katika mataifa ya Afrika.